Watoto wanaoandikishwa madarasa ya awali hapati maarifa ya msingi kuendelea na masomo

Jamii Africa

Mtaala wa Elimu ya Awali Tanzania toleo la 2013 unabainisha kuwa elimu ya awali ni ngazi ya kwanza katika mfumo wa elimu ya Tanzania ambayo hutolewa kwa watoto wadogo kabla ya kujiunga na elimu ya msingi. Elimu hii hutolewa kwa watoto kuanzia miaka 5 mpaka 6 kwa lengo la kuwapa maarifa, stadi na mielekeo ambayo itawasaidia kupambana na maisha yao ya kila siku na pia kuwaandaa kwa elimu ya msingi.

Mtaala huu umezingatia masuala mbalimbali ya kijamii ambayo huchochea ukuaji wa mtoto katika nyanja zote. Mambo hayo ni pamoja na lishe bora, afya bora, uangalizi, mahusiano ndani ya familia, vifaa na viwanja vya michezo pamoja na mila na desturi.

Lengo kuu la elimu ya awali ni kuwaandaa watoto kwa elimu ya msingi ambayo ni ngazi ya pili. Hapa ndipo msingi wa mtoto kupata elimu huandaliwa. Kama msingi huu usipojengwa vizuri, elimu ya wanafunzi huwa mashakani.

Ili kukidhi matakwa ya Mtaala, mwaka 2010 Serikali ilitoa agizo kwa shule zote za msingi nchini kuwa na madarasa ya awali ili kuwaandaa watoto kabla ya kujiunga darasa la kwanza. Agizo hilo lilitekelezwa na madarasa hayo yameanzishwa lakini changamoto inabaki kuwa mazingira wanayosomea watoto hao sio rafiki kwa wao kupata elimu bora. 

Kutokana na uwekezaji hafifu wa elimu ya awali katika shule za umma imesababisha shule hizo kukosa ushindani unaotakiwa ikilinganishwa na shule za binafsi ambazo zinafanya vizuri. 

Hilo linathibitishwa na ripoti ya Uwezo Tanzania (2017) iliyoko ndani ya taasisi ya Twaweza iliyotathmini ujifunzaji wa wanafunzi shuleni ambapo umebaini kuwa uwekezaji mdogo wa serikali katika elimu ya awali una athari za muda mfupi na muda mrefu kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Katika kupitia athari za muda mrefu imegundua kuwa wanafunzi waliopitia na kupata elimu ya awali kwa uhakika wanafanya vizuri katika masomo yao kuliko wale ambao hawakupata kabisa elimu hiyo au mazingira ya kusomea yalikuwa magumu.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kuna utofauti wa ufaulu katika majaribio ya wanafunzi waliopitia elimu ya awali na wale ambao hawakubahatika kuipata. Wanafunzi waliopata elimu ya awali walifaulu kwa asilimia 56 ukilinganisha asilimia 50 ambao hawakupata.

 UFAULU WA WANAFUNZI WALIOSOMA NA WASIOSOMA ELIMU YA AWALI

                                                            Wasiopitia elimu ya awali                  Waliopitia elimu ya awali

Inabainisha kuwa tofauti ndogo inayojitokeza kwa wanafunzi hao inaweza kueleza ni aina gani na ubora wa elimu ya awali inayotolewa na serikali. Pia muda wa kusoma elimu hiyo na ukosefu wa takwimu za uhakika zinaweza kuwa sababu nyingine za wanafunzi wengi kufeli katika majaribio ya darasani.

Akiwasilisha ripoti hiyo hivi karibuni, Meneja Programu wa Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla alisema wakati tukijivunia mafanikio ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia (MDGs) ya kuongeza uandikishaji wa watoto katika shule za msingi  lakini kuna ushahidi mdogo kwamba watoto wanasoma vizuri.

“Hata hivyo changamoto inabaki ni vipi tunapima ubora wa elimu na kuthibitisha kwa matokeo ya ujifunzaji wa watoto kama inavyotakiwa na lengo la kwanza la Malengo ya Maendeleo Endelevu”.

Anaeleza kuwa Uwezo Tanzania imeonesha kuwa bado watoto wengi waliopo katika madarasa ya awali hawapati maarifa ya msingi ikiwemo kusoma, kuhesabu na kuandika ambapo huathiri ujifunzaji na matokeo ya majaribio wakiingia elimu ya msingi.

                                Wanafunzi wa madarasa ya awali

 

Nini kifanyike

Dkt. Luka Mkonongwa, Mhadhiri wa Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam amesema ili kuboresha elimu ya awali ni muhimu kuboresha mazingira ya walimu ili watekeleza majukumu yao ya kuwapatia wanafunzi maarifa ya msingi yatakayowaanda kuelekea elimu ya msingi.

“Hakuna nchi inaweza kuendelea kuzidi uwezo wa kufikiri wa mwalimu wa nchi hiyo. Elimu haiwezi kuendelea kama walimu wasipoboreshewa mazingira kwanza kabla ya vingine vyote”.

Ameishauri serikali kuboresha miundombinu ya shule itakayovutia wanafunzi kusoma, “Ni kuangalia ni jinsi gani wananufaika na elimu na jinsi gani miundombinu inaboreshwa kuweza kuwasaidia watoto hawa”.

Kwa upande wake, Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dkt. Lulu Mahai amependekeza walimu wapatiwe motisha ya fedha au vitu vitakayochochea hari ya kufundisha wanafunzi na kumudu mazingira wanayofundishia.

“Walimu wapo na Ujuzi wanao lakini itengenezwe namna ya kuwafanya walimu watamani kwenda kufundisha kwenye mazingira magumu”, amesema Dkt. Lulu Mahai.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze amesema kuna muhimu wa kuboresha huduma za jamii zinazozunguka shule ikiwemo upatikanaji wa huduma za maji, umeme, afya ambazo zina mchango kwenye mafanikio ya wanafunzi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *