Tanzania imeshauriwa kuboresha huduma za usafiri wa anga kwa kulegeza masharti ya upatikanaji wa vibali vya kuingia nchini ili kutanua wigo wa ukuaji wa sekta ya utalii na biashara kwa nchi za Afrika.
Sekta ya usafiri wa anga katika nchi za Afrika inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kuahirishwa kwa safari, wateja kusubiri ndege muda mrefu, uchache na uchakavu wa ndege, miundombinu ya viwanja. Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia inaeleza kuwa changamoto hizo zilisababisha Afrika kupoteza dola 800 bilioni za Marekani mwaka 2016.
Jalida la Quartz Africa linaeleza kuwa changamoto hizo zitakuwa historia ikizingatiwa kuwa Umoja wa Afrika umezindua soko la pamoja la usafiri wa anga (AATM) mapema mwaka huu. Soko hilo ni utekelezaji wa Agenda ya Afrika ya 2063 ambayo ina lengo ya kuiunganisha Afrika kwa kutumia usafiri wa anga ili kuchocha ukuaji wa uchumi, kuzalisha ajira kwa vijana na umoja.
Wazo la kuboresha usafiri wa anga lilitokana na mkutano wa Yamaoussoukro wa mwaka 1999 uliowakutanisha mawaziri wa sekta ya usafiri ambapo walikubaliana na kuzifanyia marekebisho huduma za anga kwa kuunda chombo cha maamuzi kutatua migogoro, kodi na kuiunganisha Afrika.
Ikiwa mkataba huo utatekelezwa, utaziwezesha nchi za Afrika kuwa na soko la pamoja la usafiri wa ndege kama ilivyo kwa Umoja wa Ulaya na Amerika ya Kusini. AU inahamasisha uwekezaji na uvumbuzi, kuimarisha mahusiano ya kibiashara, kuongeza ushindani wa usafiri wa ndege ili kupunguza nauli, kutengeneza ajira, kusaidia mashirika ya ndege kukua na kuruhusu muingiliano wa watu na bidhaa.
Mpaka sasa, nchi 21 za Afrika ambazo zina wakazi wapatao milioni 670 tayari zimesaini makubaliano hayo. Nchi hizo ni Benin, Nigeria na Sierra Leone kutoka Magharibi mwa Afrika; Kenya na Rwanda kutoka ukanda wa Afrika Mashariki; Kusini ni Zimbabwe na Afrika Kusini; Kaskazini ni Misri.
Soko la pamoja linahusisha viwanja 10 vikubwa vya ndege ukiwemo Uwanja wa Kimataifa wa Bole uliopo Ethiopia na uwanja wa O.R Tambo uliopo Johannesburg Afrika Kusini. Mashirika 15 ya ndege ambayo yanaendesha asilimia 70 ya safari zote za ndani za Afrika yamesaini mkataba huo; shirika la ndege la Ethiopia, Kenya, Afrika Kusini na Misri.
NCHI ZILIZOINGIA KWENYE MKATABA WA SOKO LA PAMOJA LA USAFIRI WA ANGA
Hatua ya kuboresha usafiri wa anga ni msukumo wa serikali za Afrika kufungua mipaka na kuhimiza mafungamano ya biashara na utalii. Mwaka jana, waafrika walisafiri kwa urahisi kwenye nchi mbalimbali za Afrika huku nchi za Kenya, Namibia na Ghana zikitangaza kuondoa viza kwa wageni wanaoingia kwenye nchi zao.
Usafiri wa anga umesaidia kukuza sekta ya utalii kwa nchi za Kenya, Tunisia na Afrika Kusini na kuzifanya kutembelewa na wageni wengi huku mashirika ya ndege katika nchi hizo yakipata Umaarufu duniani kwa huduma bora. Shirika la ndege la Kenya (Kenya Airways) tayari limepata kibali cha kurusha ndege zake hadi Marekani bila kutua nchi yoyote.
Hata hivyo, sekta ya anga kwa nchi za Afrika bado ina safari ndefu kufikia malengo yake ikizingatiwa kuwa nchi nyingi ikiwemo Tanzania zinakabiliwa na changamoto ya mtaji wa kuendesha mashirika ya ndege huku yakikabiliwa na madeni. Jawabu ni kulegeza masharti ya upatikanaji wa viza na vibali vya uhamiaji ili kuongeza idadi ya wananchi wanaosafiri katika maeneo mbalimbali ya Afrika.
NCHI ZILIZOLEGEZA MASHARTI YA UPATIKANAJI WA VIZA (AFRIKA)
Chanzo: :AfDB Visaopenness Report
Tanzania imetakiwa kuiga njia ambazo zimetumiwa na nchi za jirani za Kenya na Rwanda kukuza soko la usafiri wa anga kwa kulegeza taratibu za kupata viza.
Hata hivyo, serikali imeendelea na upanuzi na ujenzi wa viwanja vipya vya ndege kikiwemo cha Chato mkoa wa Geita ambacho kitafungua milango ya kibiashara ukanda wa ziwa. Pia imenunua ndege mbili aina ya Bombardier ambazo zinafanya safari za ndani na mchakato wa kuagiza ndege zingine kubwa mbili ambazo zitaweza kutua katika viwanja vikubwa vya Afrika unaendelea. Serikali imekubali kulipa madeni yote ya Shirika la ndege la Tanzania (Air Tanzania)
Kulingana na jalida la Corporate Digest katika makala yake limeeleza kuwa sekta ya usafiri wa anga wa Tanzania ni nyota inayochomoza na itaimarika na kukua kwa zaidi ya asilimia 10 kwa miaka ijayo ikiwa juhudi zilizoanzishwa na serikali za kuboresha huduma hiyo zitakuwa endelevu.
“Nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania zimebadilisha mtazamo kuziona ndege kama za starehe huku wengi wakisafiri na kuongeza mapato kwa kampuni na mataifa yao”, amesema Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la National Aviation Services (NAS), Hassan El- Houry.