WAZIRI wa Ujenzi, John Magufuli amemwagiza Mkandarasi anayesimamia ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mission hospitali kwenda mjini Sengerema mkoani Mwanza, kuhakikisha anarudi mara moja kwenye mradi huo, vinginevyo atamfukuza kazi mara moja.
Waziri Magufuli alitoa agizo hilo wakati alipokuwa akizungumza kwenye sherehe za uzinduzi wa Kivuko cha Mv. Kome II, katika Kata ya Nyakarilo Jimbo la Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.
Alisema anazo taarifa za Mkandarasi huyo kutoonekana katika mradi huo kwa muda sasa, kinyume na makubaliano waliyofikiana na Serikali, na kumtaka Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), mkoani Mwanza, Leonald Kadashi kuhakikisha anamwamuru mkandarasi huyo kujerea haraka na kuanza kazi ya ujenzi huo wa barabara yenye kiwango cha llami kutoka Mission hospitali kwenda Sengerema mjini.
Kwa mujibu wa Waziri Magufuli, iwapo mkandarasi huyo hatafuata na kutekeleza mkataba alioingia na Serikali, kamwe hataogopa kumfukuza kazi na kumpa kazi hiyo mwingine, na kwamba hadi sasa Serikali ilishawafukuza kazi makandarasi wapatao 2800, ambao walionekana kwenda kinyume cha sheria, kanuni na taratibu katika makubaliano ya ujenzi wa barabara nchini.
“Wakala wa barabara Mwanza upo?. Nakuagiza mkandarasi tuliyempa kazi ya kujenga barabara hii ya Mission kwenda Sengerema mjini, arudi kwenye site (eneo la mradi), haraka sana. Vinginevyo afukuzwe kazi…maana hatuwezi kubembeleza mtu katika kazi.
“Kisiwepo kisingizio kwamba hakuna fedha. Njooni tuwape hizo fedha zipo…ingawa kilometa moja ya lami inachukua kama milioni 800 hadi milioni 1,000 lakini tutawapa. Nataka barabara hii ikamilike haraka kama tulivyokubaliana kwenye mkataba wetu”, alisema Waziri Magufuli huku akisisitiza kwamba haogopi kumfukuza kazi mtu kama atakwenda kinyume na sheria, taratibu na kanuni za nchi.
Hata hivyo, aliwaonya Wakala wa Barabara nchini, kuacha mara moja tabia zao za kusubiri Waziri aende maeneo yao ndiyo barabara zianze kutengenezwa usiku na mchana, na kusema, tabia hiyo ife mara moja, vinginevyo rungu lake litawashukia kwani hapendi kuona mambo yakifanyika kinyume na taratibu za nchi.
Akikazia hilo Waziri Magufuli alieleza kushangazwa na kitendo cha barabara ya kutoka Sengerema mjini kwenda Buchosa kuanza kufanyiwa matengenezo usiku na mchana wakati alipokuwa katika ziara wilayani humo akipitia barabara hiyo, na kwamba ni heri wamuone mbaya kuliko kulea maovu kama hayo.
“Kuna mtindo mbaya sana wa kungoja hadi Waziri aje au Rais ndiyo barabara zitengenezwe. Tena kama kuna ugeni mkubwa, utakuta njia zinatengenezwa usiku na mchana. Mtindo huu ufe mara moja, maana nimeona hata leo kwenye barabara hii ya Sengerema kwenda Buchosa imejengwa usiku na asuhubi”, alionya Waziri huyo anayesifika kwa misimamo mikali.
Hata hivyo, Waziri huyo wa Ujenzi, Dk. Magufuli alitoa muda wa siku 30 kwa uongozi wa Wakala wa Serikali wa TAMESA kuhakikisha kivuko cha Mv. Kome II kinawekewa paa la kuzuia jua na mvua kwa wasafiri, kuliko ilivyo sasa katika kivuko hicho ambapo kipo wazi, hivyo kuleta adha kubwa kwa watumiaji wa usafiri huo wakati wa masiki na kiangazi.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza