Kadi za maendeleo ya wajawazito na watoto zimekuwa kama kama lulu katika mkoa wa Mara na kusababisha malalamiko kwa akinamama wa mkoa huo.
Janet Amos (25) mkazi wa kijiji cha Nyabehu kata ya Guta, anasema ni mwaka mmoja sasa analazimika kubeba daftari anapoenda kliniki kumpeleka mwanae, badala ya kadi maalum inayotakiwa hii ni kutokana na uhaba wa kadi hizo.
Anasema anatamani kuwa na kadi ila kwa sasa hana pesa ya kununua kwani inauzwa kwa sh 2000 ambayo kwa sasa hana.
Mganga mkuu wa zahanati ya Guta iliyopo kata ya Guta wilaya ya Bunda, anasema kwa muda wa miezi sita sasa zahanati haina kadi kwa ajili ya watoto na wajawazito, kwani ameagiza mara mbili bohari kuu ya dawa (MSD) bila mafanikio.
Anasema kabla ya awamu hizo mbili ambazo hakupata kadi kabisa, aliagiza kadi 300 na akapata kadi 75 tu.
Naye mganga mkuu wa kituo cha afya kilichopo kata ya Nyamunga wilaya ya Rorya anasema hawana kadi za watoto na wajawazito kwa mwaka mmoja sasa.
Kutokana na hali hiyo ya kuadimika kwa kadi hizo, mganga mkuu wa wilaya ya Bunda Rainer Kapinga , anasema kwa sasa ameamua kuzigonga mhuri wenye saini yake, kadi za watoto na wajawazito, ili kuepusha hali yoyote ya udanganyifu inayoweza kujitokeza.