WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikitamba kujivua gamba kwa kupanga safu mpya ya uongozi, Katibu wa chama hicho mkoa wa Kagera Faustin Kamaleki ametangaza kustaafu nafasi yake mwishoni mwa mwezi huu FikaPevu imebaini.
Alibainisha hayo wakati wa mapokezi ya mjumbe mpya wa kamati kuu ya chama hicho Costansia Buhiye ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera akiwa ni miongoni mwa sura mpya katika kamati hiyo.
Aliwaambia wanachama wachache waliokutanika katika ofisi za chama hicho mjini Bukoba kuwa kwa mujibu wa taratibu mwishoni mwa mwezi huu atastaafu nafasi yake kulingana na umri mkubwa alionao.
“Nitastaafu ifikapo tarehe moja sitakuwa tena ofisini,naamini katibu atakayekuja atawafaa zaidi yangu inawezekana yupo hapa miongoni mwetu”alisema Kamaleki aliyedai umri wake wa kustaafu ulishapita miaka mingi na alikuwa akiendelea na nafasi hiyo kwa makubaliano maalmu na chama chake.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho Costansia Buhiye alisema kila mwanachama anatakiwa kutekeleza wajibu wake katika harakati za kukisafisha chama hicho na kuwa moto wa mabadiliko utafika hadi ngazi za matawi.
Pia alifananisha uamuzi uliochukuliwa kuwa ni sawa na keki isiyooza ambayo kila mtu anatakiwa kuitunza sehemu yake,na kuwaonya wale watakaoichafua keki ya mabadiliko aliyodai itafika hadi ngazi za chini za uongozi.
Aidha aliwaomba wanachama kuwaeleza wapinzani wao tafsiri halisi ya kujivua gamba ambapo kwa walio wengi hatua iliyochukuliwa inaonekana kama njia ya kujikosha kwa wananchi baada ya chama hicho kuandamwa na malalamiko ya kuwabeba watuhumiwa wa ufisadi wanaodaiwa kuifikisha nchi hapa ilipo.
Katika mapokezi hayo aliambatana na mjumbe wa halmashauri kuu ya chama (NEC) hicho na mbunge wa jimbo la Bukoba vijijini Jasson Rweikiza ambaye alipongeza mabadiliko ya uongozi yaliyofanyika ndani ya chama hicho.
Katika historia ya chama hicho mkoa wa Kagera hii ni mara ya pili kutoa mjumbe wa halmashauri kuu baada ya Samwel Kasano aliyekuwa mjumbe hadi mwaka 1974.
Habari hii imeandikwa na mwandishi wa FikraPevu aliye mkoani Kagera
hongera sana mama BUHIYE