Serikali ya Rais Dk. John Pombe Magufuli imekiri kukabiliwa na ukosefu wa fedha, hali inayoathiri utekelezaji wa shughuli zake za kila siku.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Khatibu Kazungu, wakati akijibu hotuba ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Juma Assad, kwenye Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
“Ukosefu wa fedha haupo kwenu (CAG) tu, upo serikalini kote; nikubaliane na ushauri wa Prof. (Assad), kwamba tunatakiwa kujiongeza kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ya serikali na kusimamia vizuri makusanyo yake,” alisema Kazungu.
Prof. Assad, alisema ofisi yake inakabiliwa na wakati mgumu kiutendaji, kutokana na serikali kuchelewa au kutoipelekea fedha zinazoidhinishwa na Bunge kwenye bajeti hivyo kufanya kazi ya ukaguzi wa fedha kwenye halmashauri kuwa ngumu.
Alitoa mfano wa bajeti ya ofisi hiyo katika fungu la OC kwa Mwaka 2016/17, kwamba ilikuwa Shilingi Bilioni 18 lakini mpaka Agosti mwaka jana kiasi kilichokuwa kimepokewa hakikuzidi Shilingi Bilioni 2.
“Nililazimika kuzungumza na Mheshimiwa mwenyewe (Rais John Magufuli), kwamb bila kupata Shilingi Bilioni 10 wataalamu wasingeenda kufanya ukaguzi, akaahidi kulishughulikia,” alieleza.
Prof. Assad, aliongeza kwamba Mwezi Septemba walipatiwa Shilingi Bilioni 5 na baadaye Oktoba wakapatiwa Shilingi Bilioni 4, ambapo wataalamu walianza ukaguzi kwenye halmashauri mbalimbali mwezi Novemba 2016. CAG ameweka bayana kuwa mpaka Februari mwaka huu baadhi yao walikuwa hawajamaliza kazi hiyo, hali ambayo ni tofauti na kawaida, ambapo Desemba hutakiwa wote wawe wamerejea kutoka kwenye maeneo ya ukaguzi, ili waandae taarifa ambayo huwasilishwa kwenye Bunge la Bajeti.
Prof Assad amesema kuwa mikoa na halmashauri zinazokaguliwa na CAG zimekuwa zikiongezeka; kutoka mikoa 25 hadi 26 na halmashauri 170 hadi 173. Pia bajeti inayowasilishwa na ofisi ya CAG Bungeni imekuwa ikiongezeka lakini kiasi ambacho amekuwa akipitishiwa na kupewa kimekuwa kikishuka kila mwaka.
Prof Assad ameweka bayana kuwa miaka mitatu iliyopita, ofisi yake ilianzisha utaratibu wa kuwaongezea ujuzi wataalamu wake ili waendane na matakwa ya kimataifa, lakini sasa utaratibu huo umekwama kwa ukosefu wa fedha.
“Tumeomba msaada kwa baadhi ya nchi, ikiwemo China, zimekubali kutusaidia kusomesha wataalamu wetu kwa awamu, angalau watano watano lakini ikumbukwe hata kusafirisha mtu mpaka China na kuishi huko kuna gharama, bado serikali imeshindwa kumudu gharama hizo,” alieleza Prof. Assad
Alibainisha kuwa hata watumishi 129 walioajiriwa na ofisi hiyo, hawajapatiwa mafunzo elekezi, hali inayosababisha kufanya kazi bila ufahamu wa hakika wa taratibu za kazi zao.
Miradi ya gesi na mafuta inayoendelea kutekelezwa nchini, pia haiwezi kunufaisha taifa kwa kiwango cha kutosha kutokana na taifa kutokuwa na wataalamu waliobobea katika ukaguzi wa rasilimali hizo.
Prof Assad pia ameiomba Hazina ipeleke fedha kwa wazabuni wanaoidai serikali. Bila kutaja majina ya wazabuni wala kiasi wanachodai, Prof. Assad alisema, “Naomba Hazina mpeleke fedha zinazotakiwa kupelekwa ofisini kwetu, hawa watu walipwe na sitegemei baada ya kutoa kauli hii, nipigiwe simu au nifuatwe tena na wazabuni hawa.”
Kwa mujibu wa maelezo ya Prof. Assad, mmoja kati ya wadai amesema akilipwa ndani ya mwezi huu (Machi) atapokea kiasi anachodai lakini zaidi ya muda huo, ataanza kutoza riba ya asilimia 15 ya deni hilo kwa kila mwezi.
Alisema wameshaandika barua tatu Hazina, kuhusu madai hayo bila kujibiwa; huku fedha zilizoidhinishwa na Bunge mwaka jana kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya ofisi hiyo, Sh. Bilioni 8, haijapekwa hata Shilingi moja.