Vitambulisho vitaondoa adha ya matibabu kwa wazee Tanzania

Jamii Africa

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameagiza Halmashauri zote nchini kuandalia wazee vitambulisho maalum kwa ajili ya kupata huduma za afya mara wanapozihitaji ili kulinda afya zao.

Vitambulisho hivyo vitawasaidia wazee kupata huduma za matibabu bila malipo katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za umma katika maeneo yao.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akizungumza na mmoja wa wazee waliofika kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, Ligula.

Halmashauri hizo zimepewa muda hadi kufikia Desemba 30, mwaka huu wawe wametekeleza agizo hilo.

Kwa kuzingatia na usumbufu ambao wazee wamekuwa wakiupata wanapokwenda kupata matibabu katika vituo vya afya utekelezaji wa agizo hilo la Waziri Ummy litakuwa ni mkombozi kwa wazee ili nao wapatiwe matibabu yanayostahili.

“Baadhi ya wazee wamekuwa wakipata tabu ya kupata huduma bora katika hospitali za umma, natoa wito kwa Wakurugenzi kupunguza kadhia wanayopata wazee hao wanapokwenda kutibiwa, hakikisheni mnawapatia vitambulisho wazee wote wasiokuwa na uwezo,” alisema Waziri Ummy.

Vitambulisho hivyo vitawapa fursa ya kutibiwa bure na hivyo watahamasika kwenda kupata matibabu katika hospitali mbalimbali bila kutoa malipo yoyote.

Kabla ya agizo hilo wazee kuanzia miaka 60 walikuwa wanalazimika kupata barua kutoka kwa watendaji wa Serikali za Mtaa ili waweze kutibiwa bure

Utaratibu huo kwa kiasi kikubwa ulikuwa na usumbufu ambapo walikuwa wanatakiwa kwenda kuchukua barua kwa Watendaji wa Serikali za Mitaa kila wanapoumwa  ambapo barua hizo ziliwawezesha kutibiwa bure kwa wakati huo na endapo wataumwa tena walilazimika kufuata barua tena.

Nia ya Serikali ya kufanya uamuzi wa kuwa na Sera ya Wazee mwaka 1999, katika maadhimisho ya mwaka wa kimataifa wa wazee ulikuwa ni kielelezo cha dhamira ya ya kuweka masuala ya wazee katika agenda za maendeleo ya nchi yetu.

Pamoja na kuwa Serikali inawatambua wazee kuwa ni rasilimali na hazina kubwa katika maendeleo ya nchi yetu, wazee hao wanakabiliwa  na matatizo ya umaskini, kutopata huduma stahiki za afya, pensheni na kutoshirikishwa katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya nchi yetu.

Idadi kubwa ya wazee takribani asilimia 75 wanaishi vijijini, wengi huishi katika hali ya umaskini inayoleta mashaka makubwa kwao.

Taarifa za Umoja wa Mataifa za mwaka 1999, zinaonyesha kuwa  katika Afrika, Tanzania ni nchi ya pili kuwa na sera ya wazee baada  ya nchi ya Mauritius.

Kupitia sera hiyo, Serikali iliahidi kuhakikisha kuwa wazee wanatambuliwa na wanapata fursa ya kushiriki katika maendeleo ya nchi sambamba na wananchi wengine.

Aidha, taarifa zinaonesha kuwa  kumekuwa na ongezeko la  idadi ya wazee duniani na hasa katika nchi zinazoendelea ambapo viwango vya ongezeko havilingani na uwezo wa rasilimali zilizopo kuwahudumia katika nyanja za afya, lishe, na huduma nyingine za msingi kwa maisha ya binadamu.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 1950, Umoja wa Mataifa ulikadiria kuwepo kwa watu milioni 200 wenye umri zaidi ya miaka 60, na mwaka 1975, idadi iliongezeka kufikia milioni 350 na ulitegemea kuongezeka kufikia milioni 625, mwaka 2005 na idadi hiyo itazidi idadi ya vijana na watoto wenye umri wa miaka 24 ifikapo mwaka 2050.

Barani Afrika idadi ilitegemea kuongezeka kutoka milioni 38 za mwaka 1999, na kufikia milioni 212 ifikapo mwaka 2050. Kwa kuangalia ongezeko hilo la wazee ni wakati muafaka wa kuwapatia vitambulisho ili kuwapunguzia adha ya kupata huduma za afya.

Sera ya Taifa ya Afya na Sheria ya Utumishi wa Umma nchini Tanzania zinazingatia umri wa miaka 60 kuwa ndio kigezo cha uzee, hivyo kwa sera hiyo “Mzee ni mtu mwenye wa miaka 60 na kuendelea”.

Madhumuni ya sera hiyo ni pamoja na kuwatambua kama rasilimali muhimu katika maendeleo ya Taifa na kuhakikisha kuwa wazee wanapata huduma zote za msingi zikiwemo huduma za afya.

Nchini Tanzania wazee wapo katika makundi mbalimbali ambayo ni wazee wastaafu, wakulima, wafugaji, wavuvi na wale wasio na ajira ambao kuzeeka kwao ni matokeo ya kupungukiwa nguvu za kufanya kazi.

Mazingira ya wazee hao ni pamoja na matunzo duni, umaskini, magonjwa  ya muda mrefu, lishe duni, huduma za afya kuwa ghali na wao kushindwa kuzimudu, na kuhitaji uangalizi na matunzo maalum  ya kitaalam.

Kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa vitambulisho vya matibabu kwa wazee, Serikali imetekeleza ahadi ya kurekebisha Sera ya kuchangia gharama za afya kwa kurekebisha vigezo vya utambuzi wa umri wa miaka 60 na kuweka utaratibu wa kufuatilia afya za wazee katika jamii.

Wazee wote wenye sifa za kuwa na vitambulisho hivyo ni budi wajitokeze kwa wingi ili waweze kupatiwa na kuwaondolea kabisa adha ya kupata huduma za matibabu katika hospitali za umma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *