Agenda ya wazee Tanzania imetupwa kapuni, afya zao hatarini

Jacob Mulikuza
 

SERA ya Taifa ya Wazee Tanzania (2003), inaeleza kwamba ‘mzee’ ni mtu mwenye umri wa miaka 60 na zaidi. Zaidi ya hapo, Sensa ya Taifa ya mwaka 2012 inaonyesha kwamba asilimia 5.6 ya watu nchini Tanzania ni wazee ambao asilimia kubwa wako katika mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara, Lindi na Pwani ambapo asilimia ndogo zaidi wapo katika mikoa ya Dar es Salaam na Mjini Magharibi.

Kutokana na takwimu za dunia, inaonyesha ya kuwa bado Tanzania ina idadi ndogo ya wazee kwani kati ya nchi 96 duniani zenye wazee wengi Tanzania ni nchi ya 92.

Japo takwimu hizi zinaonyesha kuwa Tanzania ina idadi ndogo ya wazee lakini bado wazee hao wameshindwa kuhudumiwa ipasavyo. Wazee hawa waliotumikia taifa hili kwa nyakati na nyanja tofauti ndio wamechangia maendeleo kwa kiasi kikubwa lakini baada ya hapo hatuwakumbuki tena kama sehemu muhimu ya taifa.

 

Nimekuwa nikijiuliza kila mara nikutanapo na wazee wetu hawa je, kuna dhamira ya dhati ya serikali na wananchi kwa ujumla kuwajali na kuwatunza wazee hawa? Au tumebaki tukibabaisha tu bila mipango yoyote ya dhati na kulifanya swala la wazee kuwa la kisisasa zaidi?

Wazee wetu Tanzania kila siku utasikia malalamiko yao ni yale yale kuanzia umaskini, kukosa lishe bora, matibabu, malazi mabovu, madai yao ya pensheni na matatizo mengine mengi.

Wazee wengi wa Tanzania ambao hawana uwezo wa kifedha ama wale wanaokosa familia bora zinazowajali wamegeuka ombaomba mijini, vijijini ama kwenye vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuwatunza wazee hao.

Mbaya zaidi, wazee hawa wanaoishi katika vituo vilivyotengwa ndio wanazidi kuteseka maradufu, kwa sababu nyumba na mazingira ni mabaya kupita kiasi, hawana mavazi nadhifu, chakula na matibabu ya shida wamebaki kutegemea hisani za watu mbalimbali.

Hivi karibuni mke wa Rais Janeth Magufuli alitembelea katika makazi ya wazee yaliyotengwa jijini Dar es Salaam na kujionea hali halisi ya wazee hao na kutoa msaada wa vyakula mbalimbali.

Hii bila shaka ilikuwa ni jitihada nzuri kuonyesha ni jukumu letu sote kuwajali wazee wetu ila swali la kujiuliza hisani hii kwa wazee itaendelea hadi lini? Kwanini tusiweke mpango imara utakao hakikisha wazee hawa wanapata chakula kwa uhakika badala ya kusubiri wasamaria wema?

Katika makala zangu mbalimbali nimekuwa nikigusia vile ambavyo ubepari (capitalism) unavyodhoofisha umoja (unity) na kuchochea ubinafsi (individualism) na hii ni kwa sababu penye umoja madhubuti siyo rahisi kuwatawala na kuwanyonya watu unavyotaka.

Na hili wengi wengi wetu tumeshindwa kuliona kama ni tatizo kwani tunadhani hizi dhana zinazoletwa na ubepari kama utanda-wizi na uwekezaji ambazo zote huchochea ubinafsi tunaziona kwamba ndio usasa. Tumeachana na tamaduni zetu kujali jamii zetu tukidhani huo ni ukale na maendeleo ni kila mtu kujijali mwenyewe na kusahau kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Udhaifu huu ndio unazidi kutudidimiza na kutuacha wanyonge pale ambapo ubepari unazidi kushamiri. Leo hii ardhi zetu zinaporwa na wawekezaji tunabaki na ardhi chache tena isiyo na rutuba, mwishowe tunaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe bila kuona chanzo halisi cha matatizo yetu na kudhani jirani yako ndiye mbaya.

Katika suala la wazee na changamoto wanazopata ni matokeo ya uchumi wa soko huria kwa sababu hivi sasa hatuoni kama ni jukumu letu sote kama serikali na wananchi kuwajali bali tunafikiri ni jukumu la mtu mwingine. Mpaka sasa matatizo ya wazee yanakosa ufumbuzi ilhali wakiendelea kuteseka.

Kutokana na ongezeko la wazee pamoja na mahitaji yao, Sera ya Taifa ya Wazee (2003) ilitungwa ikiwa na malengo yafuatayo: Kuwatambua wazee kama rasilimali muhimu katika maendeleo ya Taifa letu, Kuwashirikisha wazee katika maamuzi muhimu yanayowahusu wao na taifa kwa ujumla, Kuwashirikisha wazee katika uzalishaji mali na hivyo kuondoa umasikini miongoni mwao, Kuboresha huduma zinazotolewa kwa wazee, Kutoa ulinzi wa kisheria kwa wazee kama kundi maalum, Kuwaelimisha vijana kuhusu masuala ya uzee na kuzeeka na kuwajengea uwezo wa kufanya maandalizi ya maisha kuelekea uzeeni.

Ukitizama malengo hayo yote hapo juu ni mazuri sana na yangesaidia kwa kiasi kikubwa wazee wetu kuishi katika maisha bora na yenye staha. Lakini, sera hii inakosa nguvu ya kuyatekeleza haya yote kwani mpaka sasa haijatungiwa sheria itakayoipa nguvu ya kutumika ipasavyo.

Inakuwaje mpaka sasa ni mwaka wa 13 tangu sera itungwe na hakuna sheria yake? Kuna nia ya dhati ya kuwasaidia wazee hawa kweli au ndiyo wamebaki kuwa mtaji wa siasa tu? Au tunasubiri msukumo kutoka kwa mabepari ndipo tutunge sheria ya wazee?

Mbona kwenye gesi mswada wa sheria ulikwenda kwa kasi ya ajabu mpaka sheria ikapatikana, inakuwaje mpaka leo sera ya taifa ya wazee haina sheria au kwa sababu huku hakuna ulaji? Nadhani hili ni jipu lingine linalohitajika kutumbuliwa kwani wazee hawa wanakosa mahitaji muhimu.

Katika awamu hii ya tano ya Rais John Pombe Magufuli tuombe kuwe na dhamira ya dhati kuwasaidia wazee hawa ili waache kuishi kwa hisani ya wasamaria wema kwani kwa hali ilivyo sasa bila ya wasamaria wema wazee hawa wanazidi kutaabika.

Ni muda muafaka sasa sheria ya taifa ya wazee ipatikane ili iweze kuhimiza huduma bora za wazee zipatikane kwa mujibu wa sheria na dhana ya kutoa misaada kwa wazee ikome bali ijulikane ni jukumu letu sote kisheria kuwahudumia wazee hao kwa kupitia kodi za wananchi ziweze kuwatunza wazee hao kwenye mambo yote muhimu kuanzia chakula, afya, mavazi, malazi na mengine mengi.

Ukitizama kwa ukaribu makazi wanayoishi wazee hayo yanatia huruma sana ifike mahali sasa shirika la nyumba la taifa (NHC) wajenge nyumba kwa ajili ya wazee hawa waliopigania taifa letu kwenye nyanja tofauti tofauti. NHC wasiishie kujenga nyumba za biashara tu bali wajenge nyumba chache kwenye kila mkoa ama wilaya ambazo zitaweza kuwahifadhi wazee ambao wanakosa pa kuishi.

Ili kuendelea kuwasaidia wazee hawa kuwepo na mpango wa kutumia ujuzi wao mbalimbali walio nao kwa kwenda kwenye sekta zile muhimu kutoa ushauri na maelekezo hii itawasaidia kuweza kupata kipato kidogo cha kujikimu huku tukiendelea kujivunia uzoefu wao. Hii ni namna moja wapo ambayo hutumiwa na nchi za Magharibi kuwasaidia wazee wao ambao huendelea kutoa ushauri katika sekta muhimu na wao wakipata pesa kidogo kwa kujikimu.

Thabo Mbeki alishawahi kusema; “kama waafrika, tunapaswa kufahamu ya kuwa sote tutapoteza yale tunayojivunia kama tutashindwa kubadili bara letu”. Kwa kuazima maneno haya ya Thabo Mbeki kama watanzania fahari ya wazee wetu waliyoiletea taifa letu kwa kulijenga kwa bidii itapotea kama kwa pamoja tutashindwa kuwajali wazee wetu.

Kwa kuhitimisha, tukumbuke ya kuwa sote ni wazee watarajiwa na inatupasa kama jamii kuweza kuonyesha nia ya dhati ya kuweka miundombinu imara ya kuwasaidia wazee hawa. Kuwe na mikakati imara ambayo itasaidia wazee badala ya kusubiri huruma ya wasamaria wema.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *