Anguko la elimu lawatesa viongozi wilayani Tunduru. Wahaha kuanzisha midahalo na makongamano kuwanusuru wanafunzi

Jamii Africa

Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera ameitaka Idara ya elimu ya msingi na sekondari kuandaa mitihani kila baada ya miezi mitatu ili kukabiliana na anguko la elimu Wilayani humo.

Mitihani hiyo itawahusu wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha pili na nne ambao watakuwa wanaifanya kila baada ya miezi 3 ili kuwajengea uwezo wa kitaaluma na kujiandaa vema na mitihani ya kitaifa. 

Akitoa tathmini ya matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2017, Homera alisema kwamba katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2017 Halmashauri ya Tunduru imeshika nafasi ya tano kati ya Halmashauri nane za mkoa wa Ruvuma na katika nafasi za kitaifa wilaya ya Tunduru ni ya 179 kati ya Halmashauri 185.

Matokeo ya kidato cha nne yanadhihirisha wazi kuwa hali ya elimu wilayani humo sio ya kuridhisha na juhudi za makusudi zinahitajika kutengeneza mazingira wezeshi kwa wanafunzi ili wapate maarifa na stadi muhimu za maisha.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema mitihani hiyo itakayotolewa kwa wanafunzi itawasaidia kujipima ili shule husika ziwajibike kuhakikisha zinainua ufaulu, kwa walimu kufundisha kwa bidii na kujenga miundombinu ya madarasa ili kuwavutia wanafunzi wengi kuwepo shuleni.

“Niwaombe walimu mtuandalie vipaumbele vya mahitaji ya upungufu wa miundombinu ikiwa ni pamoja na nyumba za watumishi, matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari.” alisema Juma Homera

Ameongeza kuwa watendaji kata, vijiji na Maafisa Elimu Kata wanapaswa kufuatilia idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza, awali na kidato cha kwanza ambao bado hawajaripoti shuleni mpaka sasa ili wazazi au walezi wachukuliwe hatua kwa kushindwa kutimiza wajibu wao.

“Watendaji wa Kata, Vijiji na Maafisa Elimu kata fuatilieni taarifa za kuandikisha wanafunzi wa awali na darasa la kwanza na watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka 4-5 waende shule na mfanye kazi kwa nafasi zenu kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma na msisubiri kusukumwa” alisema Juma Homera.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa huduma za jamii katika wilaya hiyo, Abasi Ngajime alisema anguko la elimu wilayani humo linatokana na wazazi wengi kuwatumikisha watoto kwenye shughuli za kilimo muda ambao watakakiwa kuwepo shuleni. 

Wadau wa elimu wilayani Tunduru waliishauri idara ya elimu kuanzisha klabu za midahalo, michezo na makongamano ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali ili kubadilishana uzoefu, uwezo wa kujiamini na kujifunza lugha ya kiingereza.

Hata hivyo mikakati hiyo inaweza isiwe mbadala wa tatizo la elimu wilayani humo kwasababu matatizo ya msingi ya kukwama kwa elimu nchini yanajulikana ambayo ni; uhaba wa walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na miundombinu ya madarasa na shule.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa huduma za kijamii kama maji, umeme katika mazingira ya shule. Kulingana na ripoti ya utafiti wa Uwezo Tanzania (2017) inayoendeshwa na taasisi ya Twaweza iitwayo : Je, Watoto wetu wanajifunza? Imebainisha wazi kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja juu ya upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile maji na umeme, chakula na vyoo katika mazingira ya shule na ufaulu wa wanafunzi.

Ili wanafunzi wa wilaya ya Tunduru wapate elimu bora ni muhimu viongozi wa Halmashauri hiyo kuwekeza nguvu kubwa katika uboreshaji wa miundombinu na maslahi ya walimu kwa kuwapa motisha ya kufundisha.

Naye, Meneja Programu wa Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla ameishauri serikali kuziangalia wilaya za pembezoni mwa nchi na kuboresha huduma muhimu za kijamii ili kuinua elimu ya watoto hao. “Habari njema ni kwamba sasa tuna mifano hai ya nini kinachopaswa kufanyika ili kurekebisha hali hii. Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa watoto na wilaya za mwisho haziachwi nyuma”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *