Jiji la MwanzaJiji la Mwanza pichani

Meshack Mpanda (Mwanza) — Wajumbe 27 wa Serikali ya kijiji cha Nyangho’mango katka kata ya Usagara Wilaya ya Misungwi Mkoa wa Mwanza wameuza ikari 80 katika kilima cha Ntende kijiji ni hapo kwa thamani ya shilingi 1,200,000/=

Eneo hilo lenye kilima limeuzwa Desemba 2004 kwa mwekezaji KASCO MINING CO. LTD wa jijini Mwanza kwa lengo la kupasua  mawe ili kuzalisha kokoto, uamuzi wa kuuza kilima hicho ulifikiwa na wajumbe hao siku ya Ijumaa tarehe 24, Desemba 2004 baada ya kufanyika kikao cha Serikali ya kijiji na mwakilishi mwekezaji huyo na wajumbe wote kutia saini  na kugonhwa mihuri wa Halmashauri ya kijiji hicho chenye usajili Namba MZ/VG/389.

Uchunguzi uliofanyika umegundua kuwa siku hiyo ya kusaini makubaliano pia malipo yalifanywa ambapo serikali ya kijiji hicho ilipokea fedha hizo kutoka kwa mwekezaji na kumwandikia mwekezaji huyo stakabadhi Namba 001 ya tarehe 24 Desemba 2004 iliyo sainiwa na Charles Bulugu aliyekuwa Afisa Mtenaji wa kijiji ambaye kwa sasa ni marehemu.
Makubaliano hayo ambayo mwandishi wa habari hizi alipata nakala yake inaonyesha kuwa KASCO MINING CO. LTD amemilikishwa eneo hilo na Serikali ya kijiji kwa miaka 50 hadi mwaka 2054 Ijumaa saa 11 Jioni Mkataba huu utakapokwisha.

Hata hivyo, uongozi wa Serikali ya kijiji katika Muhtasari wa mauziano ulimshauri mwekezaji huyo aweza kushirikiana na Wizara ya Ardhi na makazi il aweze kupata hati miliki inayotambuliwa kisheria kama unavyoelekeza sheria ya ardhi Na 5 ya mwaka 1999 lakini hadi habari zinaandikwa hati hiyo haijashughulikiwa

Mwandishi wa habari hizi alifanikiwa kufanya mahojiano na Mkurugenzi wa Kampuni ya KASCO MINING CO. LTD bwana Nuzrat  Ezat ofisini kwake na hakuweza kuthibitisha kupata hati miliki hiyo kutoka kwenye mamlaka husika “Bwana mwandishi document zote za mradi wa kusaga kokoto Ntende ziko Dar es salaam ambako tuna ofisi” alitabasamu Bwana Nuzrat Ezat. Hata hivyo umilikishwaji huo wa ekari 80 na serikali ya kijiji umefanyika bila kuzingatia sheria Namba 5 ya ardhi ya mwaka 1999 inayohusu ardhi ya vijiji na taratibu za umilikaji wake ambapo sheria hiyo inatambua umilikaji wa kimila wa ardhi na si vinginevyo.  Hivyo umilikaji wa ekari hizo kwa miaka 50 unahitaji kutazamwa upya na serikali.

Mwekezaji huyo amekwisha pata leseni ya madini namba 228/ 2005 iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na madini Daniel Yona ambaye ameshitakiwa Mahakamani na serikali kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishea serikali hasara, kesi hiyo bado iko mahakamani ikiendelea kusikilizwa.

Leseni hiyo amabayo nakala yake ilipatikana  ilitolewa chini ya sheria ya mwaka 1998 kipengele cha 48 cha sheria ya madini kwa mwekezaji KASCO MINING CO. LTD wa S.L.P 271 TABORA ikiwa unamwelekeza eneo lake la leseni hiyo ni kata ya Buhongwa jiji la Mwanza.

Eneo hilo pia lilionyesha kwa Latitudo na Longitudo likiwa na ukubwa Kilomita za maraba 0.3602 katika hali hiyo utata umejitokeza kwa sababu mwekezaji huyu amewekeza katika kitongoji cha Ntende Wilaya ya Misungwi tofauti na leseni yake ya madini aliyoomba na kutaja eneo atakalowekeza.  Mwaka jana serikali iliunda tume kuchunguza Mikataba yote ya madini kwa sababu mikataba mingi  ilionekana ina utata.

Mwandishi wa kabari hizi alifika katka kitongoji cha Ntende na kushuhudia mwekezaji huyo akiwa amejenga nyumba yake ya kuishi na nyumba ya Meneja, pia amevuta umeme kwa gharama ya shilingi 300,000,000/= mwekezaji huyo amechimba kisima kirefu katika eneo lake ambacho kinahudumia wakazi wa eneo hilo bila malipo na kuchimba lambo la kunyweshea mifugo kwa gharama ya shillingi 70,0000,000/=

Pia barabara ambayo ilikuwa haipitiki kutoka Nyashishi kwenda  kitongoji cha Ntende yenye urefu wa kilomita tatu na nusu imekarabatiwa na mwekezaji huyo kwa shilling 40,000,000 na kwa sasa inapitika wakati wote.  Barabara hiyo imewekewa karabati kwenye madaraja na wanachi waliokuwa na mashaba wamefidiwa.

Uchunguzi uliofanyika kwenye mradi huo umegundua kuwa haujafanyiwa Tathimini ya Athari za Mazingira kama sheria Na. 20 ya 2004 ya Mazingira kipengele cha 46 (1). Mkurugenzi wa KASCO MINING CO. LTD alipoulizwa juu ya suala hilo alisema nyaraka zote kuhusu uwekezaji huu ziko Dar es salaam ambakokuna ofisi yake.

Sheria hii pia kipengele S. 81 (2) & (3) cha sheria kinavishauri vyombo vya fedha kama benki kutowapatia mikopo wawekezaji ambao watakuwa hautafanya Tathimini ya Athari za Mazingira kwenye miradi yao ili kuepuka uchafuzi wa Mazingira.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mariam Lugaila amekiri kutofahamu uwekezaji wa KASCO MINING CO. LTD Wilayani kwake.  Na kuongeza kuwa hata suala la uuzaji wa kilima cha Ntende hafahamu. Mkuu wa Wilaya hiyo amesema kuwa kisheria uuzaji wa ekari hizo 80 ulitakiwa uamuzi upitishwe na wakazi wote wa kijiji hicho katika Mkutano mkuu wa hadhara na siyo wajumbe 27 kama ulivyofanyika.

Mkuu wa Wilaya katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi yaliyofanyika ofisini kwake akiwepo kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Shaban Milao alimwagiza Afisa Ardhi na Mazingira katika Wilaya hiyo Mutasingwa Kishashu kumwandikia barua KASCO MINING CO. LTD kusitisha shughuli zake mara moja mpaka atakapo tekelekeza sheria ya Mazingira ya Taifa na kuo hati miliki kutoka Wizara ya Ardhi na Makazi Dar es salaam inayomruhusu kununua Ardhi “Ninakuagiza utekeleze hilo haraka kumwandikia mwekezaji huyo asitishe shughuli zake na nakala ya barua umpatie Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa taarifa” aliagiza mkuu wa Wilaya hiyo Bi Mariam Lugaila.

Mkuu wa Wilaya hiyo alifafanua kuwa Wilaya yake ina migogoro mingi kati ya wawekezaji na wananchi kwa sababu katika hatua za awali za kuanzishwa miradi hiyo hasa ya uchimbaji madini uongozi wa Wilaya yake hauhusishwi. Mara nyingi wanahusishwa unapotokea mgogoro unaotishia amani ndipo wanapoombwa kupelekea jeshi la Polisi kulinda amani.

Hatua hiyo imeleta madhara makubwa baada ya kufanya ulipuaji wa baruti bila ya kutoa tahadhari kwa wakazi wanaozunguka eneo hilo.  Mkazi mmoja Charles Mpogoro ameliambia gazeti hili kuwa siku ya kulipua baruti jiwe la kilo 80 liliangukia juu ya paa la nyumba yake ya nyasi na kutua juu ya ndoo kubwa maarufu kama “diaba” “Bwana mwandishi unaona hili jiwe kubwa lingetua juu ya mtu lingemuua, ila tunashukuru Mungu ametuepusha na janga hili” alifafanua bwana Mpogoro.

Hata hivyo Charles Mpogoro ameongeza kuwa ni umbali wa mita mia nne kutoka walipolipua baruti hadi kwake lakini mawe yalinifikia.  Mwandishi wa habari hizi alishuhudia mawe yakiwa yamesambaa kwenye makazi yake na shambani.  Mawe mengine yalianguka juu ya makaburi sita ya ukoo na kaburi moja kubomolewa.

Charles Mpogoro ameishi kwenye eneo hilo tangu mwaka 1960 akiwa na wazazi wake lakini kutokana  na milipuko hiyo amelazimishwa kuhama na kulipwa shilingi Milioni 3,000,000/= kwa nyumba mbili za nyasi alizokuwa anaishi, makaburi sita ya ukoo na shamba,  mkazi huyu amehamia katika kitongoji cha Mayolwa.

Kaya nyingine ya marehemu Dalahile Shagembe nayo iliathirika na ulipuaji huo wa baruti na mawe kuangukia kwenye kaya hiyo.  Wasiwasi mkubwa umeikumba kaya hiyo.  Leticia Butemi mtoto wa marehemu Dalahile amesema kuwa siku mawe yanaanguka kwao yeye binafsi alikuwepo nyumbani kwa marehemu baba yake ambaye ameishi hapo tangu mwaka 1980.

Malalamiko haya yote yamepelekwa kwa Afisa Mtendaji wa kijiji cha Nyang’homango bwana Seleman Kilasi dhidi ya Kampuni ya KASCO MINING CO. LTD. Katka mahojiano na mtendaji wa kijiji hicho tarehe 18/08/2010 ofisini kwake alikiri kupokea malalamiko hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.

Wataalamu wa Mazingira kutoka jiji la Mwanza Agosti 2008 waliandaa mpango wa kazi wa Mazingira (Environmental Management Plan (EMP) kwa Kampuni hiyo na kushauri itumie teknolojia ya kisasa ya kulipua miamba kwa baruti bila kuleta madhara na kutunza mazingira kulingana na sheria Na. 20 ya 2004 ya Mazingira.

Taarifa hiyo ambayo mwandishi wa habari hii alipata nakala yake inaiagiza Kampuni hiyo itumie teknolojia ambayo ni salama badala ya kutumia teknolojia ya zamani ambayo ilikuwa na madhara, na kuongeza kuwa teknolojia mpya haitoi vumbi ambalo lina athari kwa watu.

Kampuni hiyo pia ilishauriwa kutumia mashine ya kisasa ya kulipa miamba kwa baruti ijulikanayo kama 500E ambayo ndiyo inayokubalika kwa sasa.  Lakini mwekezaji huyu hakuzingatia.  Uchunguzi ambao umefanyika umegundua kuwa Kampuni hiyo haikuwa na mtaalamu wa kulipua miamba kwa kutumia baruti na ndiyo maana madhara makubwa yametokea.

Katika hali hiyo Mkurugenzi mtendaji wa Kampni ya KASCO MINING LTD CO. LTD katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi amekiri kumwachisha kazi mtaalamu huyo bila kutaja jina lake kutokana na tatizo hilo.

Naye kamishina msaidizi wa madini kanda ya ziwa Victoria Bwana Salmu Salim baada ya kufanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake kuhusu tatizo la ulipuaji baruti katika Kampuni hiyo alikiri kutofahamu “Bwana mwandishi mimi ni mgeni katika ofisi hii ndiyo nalisikia hilo kwako na kwa kuwa limetokea nitalifuatilia kupata ukweli” alisisitiza Bwana Salim Salim.

Afisa mtendaji wa kijiji cha Nyang’homango Bwana Seleman Kilasi amekiri kutofahamu malipo ya fidia kwa wakazi walio ondolewa kumpisha mwekezaji huyo na wala ofisi yake haina kumbukumbu zozote. “ Sina kumbukumbu kwa sababu suala la fidia ni la watu wawili na halikuhusisha serikali ya kijiji” alifafanua Afisa Mtendaji huyo wa kijiji.

Hata hivyo, fidia hizo ni ndogo ukilinganisha na thamani halisi ya mali zilizokuwepo.

Kitongoji cha Ntende kina wakazi wapatao 720 ambao ni maskini na wanaishi chini ya dola moja kwa siku.  Nyumba wanazoishi ni za nyasi bila kuwa na huduma ya maji ya uhakika na watoto wao wanasoma kwenye madarasa yasiyo na sakafu wala madirisha.  Wakazo hao hawana huduma ya Afya na nyinginezo kwa ajili ya ustawi wa maisha yao.  Kwa kiasi kikubwa wamekata tamaa na maisha.

Juma Malenge baba mwenye familia ya watu saba mwaka 2006 alilipwa 650,000/= na Kampuni ya KASCO MINING CO. LTD. Fehda hizi zilikuwa fidia ya nyumba mbili za nyasi, ekari moja na nusu ya shamba na miembe minne iliyokuwa inazaa matunda, katika uchunguzi ambao mwandishi wa habari hizi ameufanya amegundua kuwa serikali ya kijiji na Wilaya haikuwasaidia ili walipwe malipo yanayostahili.

Mkazi huyu baada ya kuhama alikwenda kununua shamba jipya la ekari moja kwa shilingi 460,000/= na kujenga nyumba mbili za nyasi zenye thamani ya shilingi 20,000/=.

Kitongoji cha Ntende kiko Kilomita kumi na mbili kusini magharibi ya Jiji la Mwanza, na pia unapopanda mabasi kwenda Shinyanga kwenye barabara ya Lami kutoka jijini Kilomita 12 unafika kitongoji cha Nyashishi na kuelekea magharibi Kilometa tatu na nusu  unafika Kitongoji cha Ntende.

Wakazi hao wa Kitongoji hicho pamoja na kuonja adha ya mwekezaji wa mashine za kusaga kokoto vilevile wanaathirika na harufu mbaya ya dampo la jiji lililopo Buhongwa Kilomita mbili Mashariki mwa kitongoji hicho.  Na kipindi cha masika harufu mbaya ya dampo imekuwa kero kubwa kwao pamoja na moshi unaotoka hapo kutokana na kuchoma taka za viwandani ambazo ni sumu.

Mbali na harufu mbaya wakazi hao wanashindwa hata kula chakula kutokana na inzi wanaotoka kwenye dampo na kujaa kwenye chakula ,wakazi hawa wameiomba serikali kuhamisha dampo hilo kwa sababu lina hatarisha afya zao.  Mwandishi wa habari hizi akiwa kwenye kitongoji hicho alishuhudia harufu kali ya uchafu wa dampo na moshi ambao unatanda anga la dampo na kusukumwa na upepo hadi kitongoji cha Ntende.

Wakazi wa Kitongoji hicho wamebaki kama watoto yatima wasio kuwa na pa kusemea wala serikali ya kuwasaidia kilio chao dhidi ya matatizo ya athari za uchafuzi wa mazingira unaowapata na Mkataba mbovu wa fidia wanazolipwa baada ya ardhi yao kutwaliwa na mwekezaji, hiki ni kilio cha wakazi hawa ambao wamepaza sauti zao na kuomba zisikike na kuwaomba viongozi waliopewa kusimamia maslahi ya wanachi wanyonge kama hawa watoe nta kwenye masikio yao na kusikiliza kilio chao.

By Jamii Africa

JamiiForums' Editorial Website | Tanzania's Online News Portal | Dedicated for Public Interest Journalism

One thought on “Ardhi ya umma yauzwa kwa tajiri kiaina”
  1. si wanakijiji waandamane ama watafute namna ya kuushinikiza uongozi wao ufanye haki? Na mkuu wa wilaya anafanya nini mpaka sasa hivi?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *