Askofu: Magufuli kamilisha mchakato wa katiba mpya

Jamii Africa

Serikali imeshauriwa kufufua mchakato wa kupata katiba mpya ili iweze kufanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa na kuboresha maisha ya watanzania.

Mchakato wa katiba mpya ulikwama baada ya kufika kwenye Bunge la Katiba mwaka 2015, ambapo hatua iliyobaki ilikuwa ni kupigiwa kura ya maoni na wananchi. Lakini siku za hivi karibuni Rais John Magufuli amesikika akisema suala la katiba sio kipaombele chake, jambo lililoibua mijadara mbalimbali kutoka kwa wananchi.

Akizungumza katika mdaharo ulioandaliwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Tanzania kuhusu katiba mpya leo jijini Dar es salaam, Askofu wa kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi amesema anatambua juhudi za Rais katika kupambana na ufisadi na kuwatetea wanyonge na ili afanikiwe anahitaji kuwa na katiba nzuri itakayokidhi matakwa ya wananchi.

“Lakini sasa ninafikiri ni muda mwafaka tupate katiba mpya. Mimi  naamini kwamba katiba ya nchi ndio dira kuu,  nchi ikikosa dira nzuri  itaendeshwa vibaya na taifa litapotea. Kama taifa halina katiba nzuri basi  litapotea” amesema.

Anaeleza kuwa katiba ndio dira ya nchi na serikali ikitaka kuboresha maisha ya wananchi ni lazima iweke mifumo imara ya kisheria itakayotoa mwongozo wa jinsi watu wanavyotakiwa kuishi  na kufikia maendeleo yaliyokusudiwa.

“Mtu yoyote mwenye nia njema na nchi  lazima ahakikishe kwamba kuna dira nzuri inayoiongoza.  Kusipokuwa na sheria mama iliyo nzuri basi mambo mengine yote yatakwenda vibaya.  Yeyote anayefanya lolote ili kulielekeza taifa kwenye hali nzuri  asipoongozwa na katiba nzuri juhudi zake nzuri zinaweza kuishia  hewani” ,

Ameongeza na kusema kuwa ili tupate katiba mpya ni lazima tujenge mtengamano wa kitaifa na kuondoa tofauti na migawanyiko ambayo ilijitokeza wakati wa Bunge la Katiba. Na imeitaka serikali kukubali na kuanzisha mchakato wa katiba mpya ili wananchi wahakikishiwe usalama na kuondoa matukio ya watu kuvamiwa na kupigwa risasi.

Kwa upande wake,  Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema  wataendelea kuishawishi serikali kwa njia mbalimbali ili irejeshe mchakato wa katiba na kuwapa fursa wananchi kupata katiba katika kipindi hiki ambacho nchi imetulia na hakuna mihemko ya kisiasa.

“Tuendele kuishawishi serikali iliyoko madarakani kwa kutumia njia za mijadala na amani  ili waone umuhimu wa kupata katiba kipindi hiki cha amani ambacho taifa limetulia hatuna michakato ya kisiasa”, amesema.

Pia amezitaka asasi za kiraia kutumia vizuri mijadala mbalimbali na kutoa mapendekezo  ambayo yatasaidia kufikia lengo la kuishauri serikali kutimiza wajibu wake kwa wananchi.

Mjadala huo wa Asasi za Kiraia unafanyika  ukiwa na lengo la kuandaa mbinu mbadala zitakazotumika kufufua mchakato wa katiba mpya. Hatua hiyo imefikiwa baada ya Jukwaa la Katiba  kuandaa maandamano nchi nzima kuishinikiza serikali kuendelea na mchakato wa kuwapatia  wananchi  katiba mpya inayokidhi matakwa  yao.

Mwezi Novemba, 2015 wakati akizundua  Bunge mjini Dodoma, Rais John Magufuli aliahidi kuendelea na mchakato wa katiba mpya ambapo hatua iliyobaki ilikuwa ni kuipigia kura katiba pendekezwa iliyopitishwa na wabunge wa Bunge la Katiba baada ya mabadiliko makubwa katika katiba ya awali ya Jaji Joseph Warioba iliyokuwa na maoni ya wananchi.

Lakini hivi karibuni Rais alisikika akisema suala la katiba sio kipaumbele chake.  Kauli hiyo iliibua hisia tofauti kutoka kwa wananchi ikizingatiwa kuwa mchakato uliashaanza tangu awamu ya nne ya uongozi wa urais.

Katiba inayotumika sasa ni ile ya mwaka 1977 ambayo inaitambua Tanzania kama nchi inayofuata sera za kijamaa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *