Athari za ubinafsishaji zinavyoligharimu taifa

Jacob Mulikuza

Hivi karibuni  Rais John Pombe Magufuli aliweka bayana namna anavyochukia ubinafsishaji wa nyenzo za uzalishaji kama ilivyofanywa na watangulizi wake. Akieleza wazi ya kuwa, watangulizi wake walifanya kosa kubwa sana kuachia nyanja kuu za uzalishaji mali kwa wawekezaji ambao wameishia kuziharibu na kuziua kabisa.

Kwangu mimi hii ni kauli bora kabisa niliyoisikia kutoka kwa Rais Magufuli, japo kunaweza kukawa na mijadala mitaani kwetu kutokana na hili. Ilihali wengine wakiamini ubinafsishaji ni kitu kizuri na wengine tukiamini ubinafsishaji sio kitu kizuri.

Tukianza na wale wanaofikiri ubinafsishaji ni kitu kizuri, wanaamini kabisa ubinafsishaji umeleta fursa nyingi katika maisha ikiwemo urahisi wa upatikanaji wa bidhaa na huduma. Pia wanaamini kumekuwa na uwezekano wa watu kufanya yale watakayo kama soko huria linavyojipambanua.

Wakati Rais Mwinyi akiingia Madarakani mwaka 1985 alipewa jina la ‘Mzee Ruksa’ kwa kile watu walichoamini ahueni ya kufanya vile watakavyo na kukaribishwa kwa soko huria. Watu walishangilia kwani waliona tofauti ya maisha ukilinganisha na enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Lakini swali la msingi la kujiuliza hapa, Je, soko huria tunalolishangilia na kuliimbia ngojera za kulisifu kupitia ubinafsishaji na wawekezaji limeleta tija mpaka sasa?

Hoja mbalimbali zitaibuka katika swali hili ikitegemea uko katika kundi gani na unafaidika vipi, ukitokea kundi la walala heri utaona soko huria lina tija za kutosha ila ukitokea kundi la walala hoi hautoona tija za soko huria.

Rais Magufuli alitukumbusha madhila ya ubinafsishaji kwa kugusia kidogo swala la mitumba na akieleza bayana ni kwa namna gani viwanda vyetu vya nguo vilikufa kwa kuwa tulishakuwa na uhakika wa kupata nguo za gharama rahisi kutoka kwa mabepari.

Ubinafsishaji na soko huria unapigiwa kelele na Benki ya Dunia pamoja na IMF kwa kuwa una manufaa kwa nchi zao za kibepari ambazo zinataka kuendelea kunyonya nchi za Afrika katika kila nyanja.

Nchi za Afrika ikiwamo Tanzania zilipewa masharti magumu na mashirika hayo ya fedha ikiwamo; sharti la ubinafsishaji, kufungua masoko kwa wawekezaji kutoka nje, kupunguza thamani ya fedha zake, kubinafsisha huduma za jamii kama elimu na afya, kuua vyama vya ushirika na kuleta stakabadhi ghalani, kukaribisha wakulima wakubwa, kuleta wachimbaji wenye mitaji mikubwa na kuwaweka kando wachimbaji wadogo na kukaribisha benki za kigeni.

Ukitafakari kwa makini utagundua baadhi ya masharti tuliyopatiwa na mabepari hao yalikuwa na lengo la kuwanufaisha wao na nchi zao na kupora rasilimali za watanzania.

Nia ya nchi za Magharibi na Ulaya ni kuhakikisha ya kuwa wanapata masoko ya kutosha kutoka Afrika, mitaji na faida inarudi kwao.  Kutoa ajira za kutosha kwa watu wao kwa jina la wataalamu, kuendeleza majaribio yao ya kisayansi kwenye  kilimo, afya, na sera mbalimbali za maendeleo hazina manufaa kwa taifa.

Ubinafsishaji umeendelea kufanya maisha ya wananchi wa kawaida kuzidi kuwa maskini kila kukicha huku kundi dogo la walala heri wakiendelea kuneemeka kila kukicha. Hebu tizama vile huduma za jamii muhimu kama afya na elimu zilivyogeuka na kuwa bidhaa ya gharama sokoni ambapo wanaoweza kunufaika na huduma hizi ni wale wanaotoka katika familia bora.

Tukienda mbali zaidi, tizama namna ambavyo mashamba makubwa wamepewa matajiri kwa kauli ya ubinafsishaji ili hali baadhi ya mashamba hayo hayajaendelezwa na wananchi wamebaki na sehemu ndogo wanavyogombania kila kukicha. Vile vile kwenye sekta ya madini, wawekezaji wamepewa maeneo makubwa ya kuchimba  madini kwa sababu ya kutumia teknolojia ya kisasa.

Ukitafakari kuhusu viwanda tulivyovigawa kwa wawekezaji, baadhi havizalishi tena. Hebu tafakari viwanda vilivyokuwapo Arusha, Moshi, Morogoro, Musoma, Mwanza, Tanga na kwingineko vimeishia wapi?

Mwaka 2016 Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alikiri kujutia ubinafsishaji wa viwanda wakati wa mjadala na Wanazuoni wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, kwenye ukumbi wa Nkurumah,  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alisema,

 “Hilo nakiri kwamba nilifanya makosa ambayo ndiyo yamepelekea viwanda vingi kufa kwa kuwa wengi waliopewa walishindwa kuviendesha wakati sisi lengo letu lilikuwa ni kuwawezesha Watanzania kiuchumi.”,

“Hivyo kulihitaji ufuatiliaji wa namna viwanda hivyo vinavyoendeshwa ili serikali iingilie endapo wangeshindwa”.

Nyanja zote kuu za uzalishaji zimebinafsishwa ambapo tunaagiza zaidi ya asilimia 70 ya bidhaa muhimu ambazo tungeweza kuzalisha katika nchi yetu na kuuza katika mataifa ya nje.

Madhila ya ubinafsishaji ni mengi mno ukilinganisha na faida tunazozipata. Sera ya Ujamaa na Kujitegemea iliweka bayana ya kuwa uchumi imara utajengwa na watu wake na sio kutegemea misaada kutoka nje ambayo inakuja kwa nia ya kudhoofisha taifa na sio kulisaidia.

Kwa kuhitimisha, ni wakati sasa taifa likatafakari upya na kurudisha nyanja kuu za uzalishaji kwenye umiliki wa wananchi. Wananchi warudishiwe viwanda, mabenki, vyama vya ushirika, migodi, mashamba ili taifa lijengwe kwa nguvu ya watanzania na sio kwa nguvu ya mabepari.

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *