BAJETI KUU 2018/19: Deni la taifa, mapato na mkwamo wa Tanzania ya viwanda

Jamii Africa

Imeelezwa kuwa hazma ya serikali kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa viwanda inaweza isifanikiwe kutokana na ongezeko la deni la taifa na kutofikiwa kwa malengo ya ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani na nje.

Angalizo hilo linakuja siku moja baada ya serikali kutoa tathmini ya mwenendo na matumizi ya bajeti ya mwaka 2017/2018 ambapo kupitia vyanzo ambavyo serikali ilitegemea kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutofikia lengo lililowekwa.

Akizungumza jana mjini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya kiwango na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema serikali ilifanikiwa kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato lakini vyanzo hivyo  havikutoa fedha zote zilizohitajika.

“ Katika mwaka 2017/18, Serikali ilipanga kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 31,712.0 (sh. 32 trilioni). Hadi kufikia mwezi Januari 2018, jumla ya mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia shilingi bilioni 17,401.9 (sh. 17.4 trilioni) sawa na asilimia 85.0 ya lengo la kipindi hicho”, amesema Dkt. Mpango.

Kwa muktadha huo, asilimia 15 ya fedha zilizotakiwa zikusanywe hazikupatikana na matokeo yake yanajidhihirisha kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu na viwanda kukosa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.

Katika vyanzo vyote  ambavyo serikali ilitegemea kupata fedha haikufikia lengo lililowekwa licha ya juhudi zilizofanyika kuvuka nusu ya makusanyo ya kutoka vyanzo hivyo ambavyo ni kodi, mikopo, misaada, dhamana na ushuru.

Chanzo cha mikopo na misaada kutoka nchi wahisani kilikuwa katika nafasi ya chini katika kuchangia mapato kwenye bajeti ya 2017/2018 kutokana na sababu mbalimbali ambazo zilikwamisha nchi hizo kutoa fedha kwa wakati.

“Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilifikia shilingi bilioni 1,408.5 (sh.1.4 trilioni), sawa na asilimia 66 ya lengo la shilingi bilioni 2,145.1 (sh. 2.14 trilioni)”, amesema Dkt. Mpango.

Halmashauri za Wilaya na miji nazo hazikufanya vizuri katika makusanyo ambapo sh.34.5 trilioni sawa na asilimia 74.1 ya makadirio ya bilioni sh.46.6 trilioni Ina maana kuwa uwezo wa Halmashauri kukusanya mapato umeshuka ukilinganisha na miaka iliyopita.

Chanzo kilifanya vizuri na kufikia lengo kwa asilimia nyingi ni mapato yasiyo ya kodi ikifuatiwa na mikopo ya ndani kutoka taasisi za fedha zikiwemo benki na kampuni za mitaji ya hati fungani.

“Mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 1,456.1 sawa na asilimia 98.2 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 1,483.4; Mikopo ya ndani ilifikia shilingi bilioni 3,931.0 ikiwa ni asilimia 95.6 ya kiasi kilichopangwa kukopwa, ikijumuisha shilingi bilioni 3,246.0 zilizokopwa kulipia amana za Serikali zilizoiva (rollover) na mikopo mipya ya shilingi bilioni 685”, amebainisha Dkt. Mipango na kuongeza kuwa mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 10,036.3 sawa na asilimia 88.3 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 11,360.8.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango  (Mb)   akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 Bungeni Dodoma.

 

Sababu kutofikia lengo la makusanyo

Waziri Dkt. Mpango amesema licha ya mafanikio  yaliyopatikana kulikuwa na changamoto za utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2017/18, kutokana na kutofikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mapato kulikosababishwa na mabadiliko ya sera, elimu ndogo ya mlipa kodi na masharti magumu ya mikopo na misaada.

“Kutofikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mapato kulikosababishwa na Mwamko mdogo wa kulipa kodi na hususan kuzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki; masharti magumu ya upatikanaji wa mikopo ya kibiashara kutoka nje; na mabadiliko ya sera za misaada katika nchi zilizokuwa zikitupatia misaada ya kibajeti”, amesisitiza Dkt. Mpango.

Aidha, utekelezaji wa bajeti uliathiriwa pia na uwepo wa malimbikizo ya madai; ugumu wa upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji; matayarisho hafifu ya miradi. Lakini pia mabadiliko ya tabia nchi ambayo yalisababisha uharibifu wa miundombinu ya usafiri kutokana na mvua kubwa katika baadhi ya maeneo.

 

Deni la taifa nalo lapaa

 Kutokana na serikali kuendelea kukopa ili kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu, viwanda na kutoa huduma za jamii, deni  la taifa linaendelea kukua ambapo linatajwa kuathiri utekelezaji wa sera ya viwanda na ukuaji wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali  hadi kufikia Desemba 2017, deni la Serikali limefikia sh. 47.7 trilioni ikilinganishwa na dola za Marekani 19,957 milioni Juni, 2016 ambapo ni sawa na kusema deni hilo limeongezeka maradufu katika kipindi cha mwaka mmoja tu tangu kuingia madarakani kwa serikali ya rais John Magufuli.

Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni sh. 34.1 trilioni, ikiwa ni asilimia 71.5 ya deni lote ambapo deni la ndani lilikuwa sh. 13.6 trilioni sawa na asilimia 28.5 ya deni lote.

Akieleza sababu ya kuongezeka kwa deni la taifa, Waziri Dkt. Mpango amesema,  “Ongezeko la deni kwa kipindi cha Juni 2016 hadi Desemba, 2017 lilitokana na mikopo mipya na mabadiliko ya kiwango cha ubadilishaji fedha (exchange rate fluctuations)”.

 Hata hivyo, serikali imesema uwiano wa deni la ndani na nje kwa Pato la Taifa kwa mwaka 2017/18 ni asilimia 34.4 ikinganishwa na ukomo wa asilimia 56, hivyo deni bado lipo chini ya kiwango cha hatari na uwezo wa kulipa deni bado ni imara.

Tanzania ya Viwanda…

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema sera ya viwanda  huenda isifanikiwe kwasababu bajeti inayopangwa kila mwaka na serikali haikisi kivitendo msukumo dhabiti wa ujenzi wa viwanda vitavyoleta matokeo makubwa kwenye uchumi wa nchi na wananchi.

Wasiwasi huo unatokana na jinsi ambavyo vipaombele vingi vya bajeti ya mwaka 2018/19 vilivyojikita kulipa deni la serikali, madai ya wazabuni, wakandarasi na watumishi wa umma na fedha chache zitaelekezwa kwenye kuandaa mazingira ya uwekezaji wa viwanda na ujenzi wa miundombinu .

Waziri Dkt. Mpango anafafanua katika hutuba yake ya vipaombele vya bajeti ya 2018/19 ambapo anasema, “Maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mgao wa bajeti ni pamoja na: kulipa deni la Serikali na mishahara ya watumishi wa umma; kugharamia ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege; kulipia malimbikizo ya madai ya wazabuni, wakandarasi na watumishi wa umma;

kuendelea na utekelezaji wa miradi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme na kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; kugharamia elimu-msingi bila ada; utekelezaji wa miradi ya maji; na kununua dawa na vifaa tiba”.

Hata hivyo, serikali imesema kwa kuzingatia shabaha, na sera za bajeti kwa mwaka 2018/19, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa sh.32.4 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Mfumo na ukomo wa bajeti ya mwaka 2018/19 umezingatia hali halisi ya upatikanaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali ili kufikisha Tanzania kwenye uchumi wa viwanda.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *