Bajeti ya serikali bado ni siri kwa wananchi, bunge lakosa nguvu kusimamia utekelezaji wake

Jamii Africa

Inaelezwa kuwa ukosefu wa taarifa na ushirikishwaji mdogo wa wananchi katika uandaaji na utekelezaji wa bajeti ni kikwazo  katika usimamizi wa rasilimali za umma.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Ubia wa Bajeti (IBP) lilifanya utafiti juu ya uwazi wa bajeti za nchi mbalimbali duniani mwaka 2017 umebaini kuwa taarifa muhimu za bajeti ya Tanzania haziwafikii wananchi kwa wakati ambapo ni changamoto katika kukuza uwazi na uwajibikaji serikalini.

Utafiti huo ulitumia viashiria 109 kupima uwazi wa bajeti. Viashiria hivyo vilitathmini ikiwa serikali kuu inaweka wazi nyaraka za bajeti kwenye mtandao kwa muda muafaka na ushirikishwaji wa wananchi kwenye utekelezaji wa bajeti.  

Viashiria hivyo vimewekwa kwenye madaraja ambapo uwazi wa bajeti ya nchi husika hupimwa kwa viwango kutoka 0 hadi 100. Na wastani wa kawaida uliowekwa ni alama 42 ambapo nchi zilizo chini ya wastani huo zinahesabika kuwa hazina uwazi kwenye bajeti .

Ripoti hiyo inaeleza kuwa mwaka 2017, Tanzania imepata alama 10 ambapo iko chini ya wastani unaotakiwa wa 42 na kujumuishwa kwenye nchi ambazo hazina uwazi kwenye bajeti ya taifa inayotakiwa kuwa wazi kwa wananchi wa kada zote.

Tanzania imeshuka kwa alama 36 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo ilipata alama 46. Alama za Tanzania zimeshuka  kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na utafiti huo wa mwaka 2017 ambapo upatikanaji wa bajeti lazima uwekwe wazi kwenye tovuti za serikali kwa wakati ili ziwafikie wananchi. Upatikanaji wa kimtandao unachukuliwa kama kigezo muhimu cha uchapishaji wa taarifa za serikali.

Kutokana na  mabadiliko hayo, Tanzania haijapata alama za kutosha kwasababu mapendekezo ya bajeti kuu na ripoti za mwaka zinachapishwa kwenye gazeti la serikali pekee na sio mahali pengine. Lakini bajeti iliyopitishwa na bunge ndio huwekwa kwenye tovuti ya wizara ya Fedha na Mipango.

UWAZI WA BAJETI YA TANZANIA
Chanzo: Open Budget Index

Tangu mwaka 2015, Tanzania imeongeza wigo wa upatikanaji wa taarifa za bajeti kwa kusambaza bajeti zilizopitishwa na Bunge lakini imeshindwa kuchapisha  kwa wakati bajeti ya wananchi kwenye mtandao. Pia  haitengenezi mapitio ya nusu mwaka na ripoti ya mwaka ya utekelezaji wa bajeti.

Ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki katika upatikanaji wa taarifa za bajeti Tanzania bado iko chini ikishika nafasi ya 4 ikifuatiwa na Burundi ikiwa imepata alama 8 na ya mwisho ni Sudan ya Kusini ikiwa na alama 5. Nchi ya Uganda imeshika nafasi ya kwanza kwa alama 66 ikifuatiwa na Kenya (46) na Rwanda (22).

Kwa muktadha huo Kenya na Uganda ndio zimekidhi vigezo vya kuwa na uwazi wa bajeti kwa kupata alama za juu zinazohitajika katika uwazi.

 UWAZI WA BAJETI KATIKA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI

                                                                   Chanzo: Open Budget Index

Utafiti huo pia uliangazia ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato wa kutengeneza bajeti tangu ngazi ya kata hadi taifa. Tanzania imepata alama 15 kati ya 100 ikionyesha kuwa inatoa nafasi chache kwa wananchi kushiriki katika mchakato wa uundwaji na utekelezaji wa bajeti. Kiwango hicho kiko juu kuliko wastani wa dunia unaotakiwa wa alama 12 lakini sio cha kuridhisha.

Hata hivyo, alama hizo bado zinaiweka Tanzania miongoni mwa nchi zenye fursa chache kwa wananchi kutengeneza bajeti inayoakisi vipaumbele vilivyopo katika jamii.

 Ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa Bunge la Tanzania kupitia kamati za kudumu zimefanya kazi nzuri ya kusimamia mchakato wa kutengeneza bajeti lakini imeonyesha udhaifu wa usimamizi wakati wa utekelezaji wa bajeti.

Sababu kubwa ni  kuwa Kamati za Bunge kushindwa kupitia na kusimamia utekelezaji wa mwaka wa bajeti na haichapishi ripoti za mapendekezo kwenye mtandao na kukagua ripoti za ukaguzi wa matumizi ya serikali. Pia bunge halishirikishwi kabla serikali haijabadilisha matumizi ya fedha zilizopitishwa na mamlaka hiyo.

USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI KWENYE BAJETI

                                                                       Chanzo: Open Budget Index

 

Nini kifanyike?

Ili kuongeza uwazi kwenye bajeti ya serikali, Tanzania imeshauriwa kuchapisha mapendekezo ya bajeti ikiwemo vitabu vya bajeti vinavyowasilishwa bungeni kwenye tovuti ya wizara ya Fedha na Mipanga. Kuweka ripoti za mwaka na bajeti ya wananchi kwenye mtandao kwa wakati.

Pia kuhakikisha wadau wote nchini zikiwemo asasi za kirai wanashirikishwa kwenye mchakato wote wa kuundwa na utekelezaji wa bajeti.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *