Bajeti yakwamisha ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kondoa

Jamii Africa

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma kutenga fedha kwenye bajeti ya Mwaka ujao wa Fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Kondoa ili kukabiliana na changamoto za afya zinazowakabili wananchi.

Dkt. Kijaji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini, ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya siku mbili wilayani humo kukagua shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vipya vya afya pamoja na miundombinu ya elimu.

Alisisitiza kuwa atafuatilia na kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa ili kusogeza huduma ya afya karibu zaidi na wananchi hususan waishio vijijini ambao wanakosa huduma ya uhakika kutokana na kukosekana kwa hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Kondoa.

Aidha, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amewataka watendaji wa halmashauri hiyo ya Wilaya ya Kondoa kuhakikisha kuwa wanawatumikia wananchi kwa moyo, umoja na mshikamano ili malengo ya kitaifa ya kuwaletea maendeleo kupitia dhana ya Tanzania ya viwanda yaweze kufikiwa.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Kondoa Vijijini Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Halamashauri ya Kondoa Falesy Kibassa (kushoto) wakati wa kikao na watendaji wa Halmashauro hiyo.

Alisema kila idara, ikiwemo ya kilimo, maji, elimu, afya, maendeleo ya jamii na miundombinu ya barabara ihakikishe inatimiza malengo yake ili wananchi waongeze uzalishaji hususan sekta ya kilimo itakayochangia upatikanaji wa malighafi itakayotumika katika uzalishaji viwandani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Falesy Mohamed Kibassa amesema Halmashauri yake imejipanga kuhakikisha kuwa malengo waliyojiwekea ya kuwatumikia wananchi wa Wilaya ya Kondoa yanafikiwa kwa kuimarisha usimamizi na utendaji kazi katika idara zote.

Alimhakikishia Dkt. Kijaji kwamba watendaji wake,watahakikisha wanaifikisha wilaya hiyo kwenye maendeleo yaliyokusudiwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *