Bei ya nafaka yashuka, wakulima waitaka serikali kufungua milango ya kuuza nje ya nchi

Jamii Africa

Imeelezwa kuwa uamuzi wa serikali ya Tanzania kuzuia usafirishaji wa mahindi nje ya nchi umeshuha bei ya zao hilo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kushuka kwa bei ya mahindi kumetokea zaidi katika robo ya kwanza ya mwaka 2018 ambapo kumeongeza upatikanaji wa zao hilo hasa kwenye maghala ya kuhifadhia mazao.

Data za Baraza la Nafaka la Afrika Mashariki zinaonyesha kuwa bei ya mahindi, mihogo na mchele katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika imeshuka kutokana na mavuno mengi.

Taarifa ya mkataba wa biashara wa Afrika Mashariki inaeleza kuwa hadi kufikia Januari mwaka huu, tani moja ya mahindi nchini Tanzania ilikuwa inauzwa sh. 451,242, Uganda (410,220) na Rwanda (950,343). Lakini bei zilishuka zaidi mwishoni mwa robo ya kwanza ya 2018 na kufikia sh. 396,546 kwa tani moja Tanzania, Uganda ( 403,383) na Rwanda (727,001).

Hata hivyo, bei ya muhogo ilipanda zaidi katika nchi za Rwanda na Tanzania ambapo hadi kufikia Machi tani moja iliuzwa sh. 2.231,141 kwa Tanzania, lakini ilishuka nchini Uganda. Bei ya muhogo iliimarika pia Somalia na Ethiopia kutokana na mavuno yaliyotokana na misaada ya kiutu inayotolewa na mashirika ya kimataifa.

Usafirishaji wa muhogo ulipungua nchini Uganda kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya ndani na uzalishaji wa bia. Duru za kibiashara zinaeleza kuwa Uganda na Tanzania ndiyo walikuwa wasafirishaji wakubwa huku Sudan Kusini , Rwanda na Kenya zilikuwa zinaagiza zaidi.

Baada ya Tanzania kuzuia usafirishaji wa mahindi nje ya nchi katika robo ya pili ya mwaka 2017, bei ilishuka kabla ya kuimarika. Hali hiyo ilitokana na kuongezeka kwa mavuno katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki.

Bei ya mahindi ilishuka mwezi Februari na Machi kwasababu ya kuongezeka kwa usambazaji mwishoni mwa mwaka 2017. Kenya ambayo ilikuwa muagizaji mkubwa mahindi katika ukanda wa Afrika Mashariki ilishuhudia kushuka kwa bei ya mahindi kutokana na kuimarika kwa usambazaji wa zao hilo.

Kati ya Julai 2017 na Machi mwaka huu, Kenya iliagiza tani 400,166 za mahindi ambapo Uganda pekee iliiuzia nchi hiyo asilimia 54 ya mahindi yote iliyonunua kutoka Tanzania.

Pia bei ya unga wa ugali nchini Kenya  ilishuka zaidi hadi kufikia Ksh. 115 kwa kilo mwezi Januari mwaka huu. Kutokana na serikali kuanzisha programu ya ruzuku kwa wananchi.

Mahindi yakishushwa tayari kwenye malori

Taarifa ya Mkataba wa biashara wa Afrika Mashariki bado inaonyesha kuwa usafirishaji wa mazao ya nafaka kutoka Tanzania kwenda Kenya unaongezeka licha ya mgogoro wa kibiashara unaoendelea baina ya nchi hizo mbili.

Mwaka mmoja uliopita, usafirishaji mahindi kutoka Tanzania kwenda Kenya uliongezeka kwa asilimia 1,302 hadi tani 76,723 huku usafirishaji kuelekea Burundi uliongezeka kwa asilimia 1,041 hadi tani 1,254.

Usafirishaji wa mchele wa Tanzania kuingia nchini Kenya uliimarika kwa asilimia 16 hado tani 22,792 na uliosafirishwa kuelekea Burundi ulikuwa asilimia 130 hado tani kufikia tani 1,254.

Hata hivyo, Serikali ya Tanzania imeshauriwa kufungua milango kwa wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi ili kufaidika na ukuaji wa bei ya soko katika nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.

Ushauri huo unakuja wakati ikiwa imebaki miezi michache kwa wakulima hasa wa mahindi na maharage kuanza kuvuna mazao hayo katika maeneo mbalimbali ya nchi yanayopata msimu mmoja na mwili ya mvua.

Kulingana na Ripoti ya Mapitio ya Usalama wa Chakula katika nchi za Pembe ya Afrika, inaeleza kuwa bei ya mazao ya chakula itaongezeka mara dufu katika kipindi cha miezi miwili ijayo ya uvunaji kutokana na  mafuriko, wadudu na magonjwa yaliyoripotiwa katika maeneo hayo.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *