Bodaboda zasababisha vifo 6,700, majeruhi 36,700 katika miaka 10

Jamii Africa

DAUDI Maliyatabu (35) amelala kitandani katika wodi Namba 4 Kibasila katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam huku akiugulia maumivu makali.

Hana uwezo wa kujigeuza kwa namna yoyote kwa sababu mguu wake wa kulia umevunjikia kwenye paja na mkono wa kushoto umevunjika pia huku kiwiko kikiwa kimesagika kutokana na ajali mbaya ya pikipiki (bodaboda) aliyoipata katika Kijiji cha Mtanana, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Anaieleza FikraPevu kwamba, kinachomuumiza zaidi siyo maumivu anayoyasikia, bali ni taarifa kuwa anatakiwa kukatwa mguu wa kulia kwa kuwa mfupa wake hauwezi kuunganishwa tena kutokana na kuvunjika vibaya.

Walau mkono wake wa kushoto utasalimika, ingawa atalazimika kufungwa vyuma maalum kwa sababu kiwiko kimesagika.

Daudi ni miongoni mwa maelfu ya watumiaji wa usafiri wa pikipiki, maarufu kama bodaboda, ambao wamepata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali huku wengine wakipoteza maisha.

FikraPevu inafahamu kwamba, katika kipindi cha miaka 10 tangu mwaka 2006 hadi 2015 watu 6,743 wamefariki dunia kutokana na ajali 37,937 za bodaboda huku wengine 36,722 wakijeruhiwa na wengi wakipata ulemavu wa kudumu.

 “Nashukuru niko hai, lakini kwamba kuanzia sasa nimekwishakuwa mlemavu ni jambo ambalo linanitia simanzi kweli. Shughuli zangu zote zitasimama kwa sababu zilikuwa zinahitaji niwe na viungo kamili kuweza kuzitekeleza,” anasema Daudi, mkulima na mfanyabiashara wa nafaka katika Soko la Kibaigwa.

Akielezea namna ajali hiyo ilivyotokea, Daudi alisema kwamba, kubaki kwake hai ni majaliwa ya Mungu tu kwani aliamini siku kwamba ulikuwa ndio mwisho wake.

“Nilikuwa natoka nyumbani kwangu Kibaigwa nikiwa naendesha mwenyewe pikipiki yangu kuelekea Kongwa ili kwenda kununua karanga kwa wakulima. Nilipofika Mtanana, yapata kilometa tatu kutoka Kibaigwa nikakutana na lori ambalo liliacha njia na kuja upande wangu,” akaieleza FikraPevu.

Akaongeza: “Sikujua kilichoendelea, lakini walioshuhudia walisema kwamba niliingia chini ya uvungu wa lori ambako ndiko walikonitoa wakidhani nimekufa, lakini walipoona ninapumua kwa mbali wakanikimbiza Hospitali ya Wilaya ya Kongwa kabla ya kuletwa huku Muhimbili.”

Janga la taifa

Usafiri huo wa bodaboda, ambao awali ulionekana kama mkombozi kwa watumiaji wake kutokana na kupenya hata kwenye vichochoro na kuepuka foleni hivi sasa umegeuka janga kubwa la kitaifa badala ya unafuu wa ajira kwa vijana wa vijijini na mijini.

FikraPevu inatambua kwamba, tangu Aprili 2009 Serikali iliporuhusu pikipiki (bodaboda) zifanye kazi ya kusafirisha abiria na kurahisisha usafiri hasa kwenye misongamano kama mijini, vyombo hivyo vya usafiri vimekuwa balaa kwa kuongeza idadi ya ajali na vifo vinavyotokana na ajali hizo.

Ni nzuri kwa ajira na rahisi kwa usafiri, lakini kwa sasa zimeonekana kuwa hatari zaidi kwa uhai wa binadamu.

Wakati mauzo yakiendelea kupaa, idadi ya vifo vinavyohusiana na bodaboda nayo imeendelea kuongezeka kutoka vifo 89 mwaka 2006 hadi 971 mwaka 2015 huku idadi ya watu waliojeruhiwa kwenye ajali hizo nayo ikiongezeka kutoka 873 hadi 2,491 kwa kipindi hicho.

Takwimu ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kwamba, mwaka 2013 ndio uliokuwa na ajali nyingi za pikipiki, vifo pamoja na majeruhi ikilinganishwa na miaka mingine, ambapo jumla ya ajali 7,061 zilitokea na kusababisha vifo 1,138 na majeruhi 6,779 nchini Tanzania.

Chanzo cha ajali za bodaboda

Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani linaeleza kwamba, chanzo kikubwa cha ajali za bodaboda ni ukosefu wa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki na kukosa sifa ya kumiliki leseni ya udereva inayothibitisha kuhudhuria mafunzo katika vyuo vinavyotambulika na serikali  na kufuzu mafunzo ya uendeshaji wa pikipiki. 

“Tatizo hili limesababisha waendesha pikipiki kutozijua sheria na kanuni za Usalama Barabarani sambamba na kutozijua alama za barabarani, uendeshaji wa hatari kwa kupenyeza katikati ya magari na kuyapita (careless overtakings), mwendo kasi, kutovaa kofia ngumu, na upakiaji wa abiria zaidi ya mmoja (mshikaki),” zimefafanua ripoti nyingi za Hali ya Uhalifu nchini zinazotolewa na Jeshi la Polisi kila mwaka. 

Ripoti hizo, ambazo FikraPevu inazo nakala zake, zimeeleza vilevile kwamba, ajali zitokanazo na waendesha pikipiki zimekuwa zikisababishwa na udhibiti hafifu wa uagizaji na uingizaji wa pikipiki hapa nchini kwa mamlaka zinazohusika.

“Hakuna Sera ya kudhibiti vyombo hivi, jambo ambalo limepelekea kuwa na wafanya biashara wengi wa pikipiki na wingi wa pikipiki unaosababisha kila mtu kuwa na uwezo wa kumiliki hasa kwa vijana wasio na ajira na kuzitumia kibiashara baada ya serikali kuruhusu vyombo hivyo kutumika kusafirisha abiria,” zinaeleza ripoti hizo.

FikraPevu inafahamu kwamba, uagizaji wa pikipiki umeongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka uingizaji wa pikipiki 20,117 mwaka 2006 hadi pikipiki 113,610 mwaka 2010 na idadi hiyo imeendelea kuongezeka kila wakati.

Aidha, miundo mbinu nayo imetajwa kuwa chanzo kingine kwani haikidhi matumizi ya vyombo vya moto kwa nafasi.

“Hii inatokana na barabara nyingi za mjini kuwa nyembamba sana na kusababisha ajali za magari kugongana na pikipiki kutokea mara kwa mara na waathirika wakubwa wakiwa ni wapanda pikipiki,” zinaongeza ripoti hizo kila wakati.

Mathalani, katika kipindi cha mwaka 2011 kulikuwa na ajali za pikipiki 5,384 ikilinganishwa na ajali 4,363 zilizotokea mwaka 2010 sawa na ongezeko la 23%, ambapo vifo vilikuwa 945 ikilinganishwa na vifo 683 sawa na ongezeko la 38%, na majeruhi 5,506 ikilinganishwa na majeruhi 4,471 sawa na ongezeko la 23%. 

Kati ya Januari na Juni tu mwaka 2012, jumla ya ajali 2,641 zilikuwa zimetokea zilizosababisha vifo 487 na majeruhi 2,706, huku wengi wa waathirika wakiwa ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Ingawa takwimu zinaonyesha kwamba idadi ya ajali hizo imekuwa ikipungua, lakini bado haijaleta matumaini chanya kwani bado roho za wengi zinaendelea kupukutika huku wengine wakiachwa na ulemavu wa kudumu.

Mwaka 2015 kwa mfano, idadi ya ajali ilikuwa 2,749 kulinganisha na ajali 4,304 mwaka 2014 ikiwa ni upungufu wa ajali 1,555 sawa na asilimia 36.1.

Hata hivyo, ajali hizo kwa mwaka 2015 zilisababisha vifo 971 ikilinganishwa na vifo 957 mwaka 2014 , likiwa ni ongezeko la vifo 14, sawa na asilimia 1.5.

Majeruhi kwa mwaka 2015 walikuwa 2,491 kulinganisha na majeruhi 4,016 mwaka 2014, ukiwa ni upungufu wa majeruhi 1,525, sawa na asilimia 38.

Mnamo Mei 2011, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Ally Mwema, alikiri kwamba bodaboda zimekuwa janga kubwa la taifa kutokana na kuwa chanzo kikuu cha ajali nchini Tanzania.

“Pikipiki kama chombo cha usafirishaji, kimekuwa kikitumiwa na wananchi katika shughuli mbalimbali kama njia rahisi zaidi katika kusafirisha abiria na mizigo kote mijini na vijijini. Licha ya nia njema ya Serikali ya kuwapunguzia wananchi adha ya usafiri, pikipiki hizi zimekuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani,” alikaririwa akisema.

Tofauti na miaka ya nyuma ambapo vituo vya polisi vilijaa magari yaliyokamatwa kwa makosa mbalimbali, hivi sasa vituo hivyo vimesheheni bodaboda kana kwamba ni karakana au mahali pa mauzo.

Bodaboda zilizokamatwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo ajali zikiwa katika kituo cha polisi.

Aidha, hospitali nyingi nchini idadi kubwa ya majeruhi wa ajali inaelezwa ni wale waliopata ajali za bodaboda, ambao kwa sasa wamekuwa wengi kuliko uwezo wa hospitali zenyewe.

Zinauzwa kama ‘toi’, kwetu biashara

Uchunguzi unaonyesha kwamba, pikipiki nyingi zilizozagaa nchini zimeingizwa kutoka China zikiuzwa kwa bei nafuu zaidi na zimekuwa kama ‘toi’, ambapo yeyote anaweza kuzipata hata kwa Shs. 1.5 milioni.

FikraPevu inafahamu kwamba, pikipiki hizo ambazo zimejaa kwenye soko kwa bahati mbaya ziko kwenye mikono isiyo sahihi, kwani wengi wa madereva ni vijana ambao hawana mafunzo sahihi ya udereva, achilia mbali kuwa na leseni.

Mara nyingi wanaendesha bila kuvaa kofia ngumu ambazo wamezifunga kama mapambo, wanavunja sheria zote za usalama barabara, wanachojua ni kuwasha na kuvuta mafuta, na wengi wanabeba abiria zaidi ya mmoja (mishikaki), mambo ambayo yanatokea mbele ya macho ya askari wa usalama barabarani.

Uhusiano wa kiuchumi kati ya China na Tanzania umeongeza kasi ya uingizaji wa bidhaa mbalimbali nchini Tanzania, zikiwemo bodaboda kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita.

FikraPevu inafahamu kwamba, usafirishaji na uingizaji wa bidhaa kati ya China na Tanzania kwa mwaka 2001 ulikuwa Dola za Marekani 93.4 milioni tu, lakini kufikia mwaka 2010 ulikuwa Dola za Marekani 1.65 bilioni, ambalo ni ongezeko kubwa na limezidi kukua kadiri miaka inavyosonga mbele.

Aidha, miaka 15 nyuma kulikuwa na makandarasi 12 tu kutoka China na mameneja na wahandisi 240 wa Kichina, lakini kufikia mwaka 2010 pekee kulikuwa na kampuni zaidi ya 30 za Kichina zilizokuwa na wataalam takriban 3,000 kutoka China na wafanyakazi wa Kitanzania zaidi ya 30,000 zikishughulika na ujenzi wa barabara, madaraja, huduma za maji, majengo, mawasiliano na miradi mingine ya miundombinu.

Mwishoni mwa karne iliyopita, migahawa na gereji za Kichina ilikuwa ikihesabika jijini Dar es Salaam, lakini kwa sasa kuna wawekezaji takriban 300 kutoka China waliowekeza zaidi ya Dola 200 milioni wakiwa na viwanda vinavyotengeneza viatu, vyombo vya plastiki na kadhalika.

Hali hiyo haishangazi kuona wingi wa bodaboda nchini, kwani Watanzania nao wameona milango ya kufuata bidhaa China iko wazi na huko wananunua vitu kwa bei nafuu, vingi kati ya vitu hivyo vikiwa havina ubora stahiki kwa kuwa vimetengenezwa katika viwanda vidogo ambavyo vimetapakaa katika miji mingi huko China.

FikraPevu inaona kwamba, jambo pekee ambalo linapaswa kufanyika kudhibiti wimbi la ajali ni kwa Jeshi la Polisi kusimamia sheria na kuwakamata wahalifu na kuwafikisha mahakamani, lakini pia kuwahimiza vijana kwenda kupata mafunzo ili kujiajiri kupitia bodaboda, biashara ambayo imewanufaisha wengine wengi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *