CCM baada ya Igunga, kujivua gamba kutaendelea?

Jamii Africa

MTIHANI wa kihisia unaanza katika ngazi za juu za CCM kuhusu zoezi la ‘kujivua gamba’ ambalo mtihani wake wa kwanza (na labda wa mwisho) ulikuwa ni Igunga katika uchaguzi mdogo wa mbunge kutokana na hatua ya kujiuzulu kwa Rostam Aziz.

CCM ilishinda katika zoezi hilo lakini ilitoka jasho, kiasi cha upinzani kudai kuwa wameshinda kiitikadi kwani walipata asilimia 42 (CHADEMA) katika jimbo ambalo hawakuthubutu kumweka mpinzani kwa Rostam uchaguzi mkuu mwaka jana. Swali hapo ni kuwa hayo ni maendeleo ya chama au kuweka mazingira sawa ya ushindani, anapokuwepo mgombea wa kawaida, tofauti na Rostam Aziz ambaye nguvu yake si ya kawaida?

Ungejaribu kubuni itakavyokwenda, unaona kuwa suala hilo litaishia hapo, kwani mkazo wake ni kama JK atalifuatilia, na kama atapata maneno mengine ya kusema, kwa mfano kusema kuwa CCM haiwezi kutumia kila kipengele cha katiba kwa suala hilo (kuvuliwa uongozi au uanachama kwa masuala ya maadili) kwani hakuna kilichothibitishwa kisheria. Ina maana kuwa atoe rai kwamba suala hilo ni la kiitikadi ndani ya chama kutokana na hisia za watu wengi na sifa ya CCM kuvurugwa kutokana na tuhuma ambazo zinawaandama baadhi ya makada wake. Lakini inakuwa siyo kulazimisha kwani mhusika asipojitolea kuondoka, kumlazimisha inabidi kufungua mashtaka ya kiitikadi ndani ya chama, mteremko ambao utavuruga umoja.

Hisia kuwa mkakati wa kujivua gamba unaishia hapo ni hali ya kuwa suala halisi ni kile alichokiogopa JK, kuwa akiendelea na madai kuwa ‘tunatafuta ushahidi’ wa suala hili au lile, na kampeni ndani ya CCM dhidi ya ‘mafisadi’ zikadumu hadi uchaguzi mkuu 2015, huenda asipate urahisi katika kustaafu. Hawezi kuhakikisha kuwa ataingia madarakani (kwa kuwa mgombea wa CCM) swahiba ambaye hatamgeuka na kumfikisha mahakamani ili apate sifa za haraka miongoni mwa wananchi.

Kati ya walengwa wa masuala la ufisadi, ambaye anamgusa JK moja kwa moja ni Rostam; akishaondoka madarakani au bungeni zaidi ya nusu ya mzigo unaondoka. Suala la kuondoka Edward Lowassa siyo la uzani huo kwani alijiuzulu uwaziri mkuu, na mtu hawezi kuadhibiwa kwa shitaka moja, mara mbili – kama pia ilivyo kwa Andrew Chenge. Haitakuwa rahisi kuwataka nao ‘wajivue gamba.’ Ikumbukwe kuwa tayari Lowassa alishaibeza serikali ya rais Kikwete kuwa ina ubutu katika kutoa maamuzi!

Isitoshe, mkakati wa ‘kujivua gamba’ unaonekana ni wa kada mmoja tu katika sekretariati ya CCM, yaani katibu mwenezi Nape Nnauye, licha ya kuungwa mkono na JK, kwani katika chama hisia za mtu hatungiwi na mwenyekiti; anamsikiliza mwenyekiti na pia anatumia akili yake ya kuzaliwa.

Rais Kikwete akimnadi jukwaani Rostam Aziz wakati wa kampeni Oktoba 2010

Ingekuwa dhana hiyo tayari ni ya chama, Rais Mstaafu  angeenda jimboni kufungua kampeni kwa fikra hiyo, na bila Rostam kando yake, akiwa labda na Nape au Wilson Mukama. Haikuwa hivyo, na hulka au hisia za jadi za CCM ziliendelea kama ilivyo kawaida, hivyo Rostam akawa jukwaani, halafu Mzee Mkapa akafungua kampeni, akitumia ubora wa CCM na serikali yake, na siyo hisia za Mizengo Pinda na wengine kuwa ‘watu wanakihama chama,’.

Ina maana kuwa mzigo kwa JK sasa ni mwepesi, kuwa haitazamiwi kuwa hata akiingia madarakani swahiba wa akina Samuel Sitta ataanza tena kukumbushia Kagoda na hata Richmond. Suala la rada halimhusu JK, na lile la Richmond/Dowans sasa limekwisha baada ya kuondoka Rostam; hivyo kwa upande wa usalama akiwa hana madaraka ya dola, JK anaweza
kuridhika na suala hilo lilipofika. Inakuwa tu suala la ‘withdrawal management,’ kama NATO inavyotafuta mlango wa kutokea Afghanistan, kuwa pasiharibike, NATO isionekane inakimbia, na hata hivyo ifanye mipango ya kuondoka ndani ya miaka miwili.

Rais Kikwete akimnadi Edward Lowassa wakati wa kampeni Oktoba 2010

Chama kimeikana sera ya kujivua gamba, kikawaweka kando maswahiba wa sera hiyo, kikapeleka ‘wasio na makundi,’ yaani wasio karibu sana au mahasimu wa Rostam, hivyo hakuwepo Sitta, wala Lowassa – na hata nafasi ya Mukama ilikuwa ndogo, huku Nape akipigwa PI – prohibited interpreter – wa mkakati mzima wa uchaguzi Igunga, nini CCM imefanya. Suala la Rostam kujiuzulu likabaki ni la vikao vya CCM, na siyo mtaji wa kufanyia kampeni, hivyo Nape kusema kujivua gamba kumekubaliwa, si rahisi kujua anazungumzia CCM ipi – au anazungumzia wafuasi wa Chadema.

Makala haya yameandikwa na Erick Kabendera wa FikraPevu

4 Comments
  • ccm sasa lazima wajifunze kuwa ile dhana ya kujifua gamba haina msingi wowote,maana huweza kumtimua mtu ukimtuhumu kuwa mwizi then baadae anasimama naye kuomba kura.

  • Mwambieni Presidenti wa hili nchi, wananchi tunamashaka na hofu ya machafuko kuliko wakati mwingine wowote tangu uhuru. Hii ni kutokana na siasa za u kambale (wote tuna ndevu) ndani ya chama chake. Ni chama kisichotabirika kabisa any time tunahofu hata yeye kuporwa uenyekiti kisha madaraka tuliyompa. Kama haamini afanye uchunguzi juu ya hofu ya wananchi kwa amani yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *