CCM yajibu mapigo, yamng’oa kigogo CHADEMA

Jamii Africa

Siku chache baada ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kumpa uanachama aliyekuwa Mbunge wa CCM, Lazaro Nyalandu, chama hicho kimejibu mapigo kwa kukubali maombi ya  Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA), Patrobas Katambi kuwa mwanachama mpya.

Hatua hiyo ya Katambi imefikiwa leo katika kikao cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika Ikulu Dar es Salaam ambapo aliungana na wanachama wengine kutoka Chadema akiwemo Laurence Masha na  ACT Wazalendo  ambao ni Samson Mwigamba, Kitila Mkumbo  na Wakili Alberto Msando waliotangaza kuvihama vyama vyao na kuingia CCM wakidai wameridhishwa na utendaji wa serikali ya awamu ya tano. 

Akizungumzia uamuzi wa kuwapokea vigogo hao kutoka vyama vya upinzani, Mwenyekiti wa CCM na rais wa Tanzania, John Magufuli aliungana na wajumbe wote wa kikao kukubali maombi ya vigogo hao ambao rasmi wamekubaliwa kuwa wanachama wapya wa CCM.

“Wajumbe napenda niwaulize wote kwa ujumla mnawakubali au mnawakataa? (wajumbe wakaitikia tunawakubali), kwa hiyo ndugu wanachama wapya mlioamua kurudi wenyewe kwenye Chama  Cha Mapinduzi, hiki ndio kikao kikubwa lakini tuliona tupate ‘endorsement’ ya mkutano huu wa NEC. Mkashiriki vizuri kwenye shughuli za Chama Cha Mapinduzi”, amesema rais Magufuli.

Katambi amekuwa Mwenyekiti wa BAVICHA tangu mwaka 2014 alipochukua nafasi ya John Heche na alikuwa mgombea Ubunge wa jimbo la Shinyanga mjini mwaka 2015 lakini hakuchaguliwa. Amefanya uamuzi  wa kuondoka CHADEMA baada ya kile kinachodaiwa ni ubinafsi wa baadhi ya viongozi katika chama chake ambao wanahubiri mabadiliko lakini wao wenyewe hawabadiliki.


"Naomba ridhaa ya kuwa mwanachama siyo kwasababu ya madaraka bali kwa ajili ya maslahi ya taifa pamoja na kusaidiana na wenzangu kukiendeleza chama. Natambua harakati zilizofanyika kwenye awamu iliyopita”, amesema Katambi na kuongeza kuwa,

“Watu tunapenda mabadiliko lakini hutupendi kubadilika. Ni kwamba kama leo nitaitwa msaliti, basi nasaliti ubinafsi na kundi la wabinafsi kwa ajili ya maslahi ya taifa”.

Kuondoka kwa Katambi na Mwanasheria Laurence Masha kunatajwa kama ni kujibu mapigo kwa CHADEMA ambacho siku chache zilizopita kilikabidhi kadi ya uanachama kwa aliyekuwa Mbunge wa  CCM na Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ambaye alikihama chama hicho na kukimbilia CHADEMA akidai anaungana na watu wengine waliopo upinzani ambao wanapigania mabadiliko na maslahi ya taifa ambayo yanakanyagwa na chama tawala.

Mwenyekiti wa CCM, rais John Magufuli akiongoza kikao cha NEC, Ikulu-Dar es Salaam

Hatua hiyo ya Nyalandu kuondoka CCM ilikuwa ni pigo kwa chama hicho ikizingatiwa kuwa kimepoteza nafasi ya kuongoza jimbo na kitalazimika kwenda kwenye uchaguzi. Hali hiyo pia ilitokea kwa aliyewahi kuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Azizi ambaye kabla ya kumaliza muda wake wa ubunge alijiudhuru nafasi yake mwaka 2011 lakini hakujiunga na chama chochote.

Kwa upande wake aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurence Masha ambaye wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 alijiunga na CHADEMA na sasa ameamua kurudi CCM  akiwa na hoja kuwa CHADEMA hakina uwezo wa kushika dola na kuongoza nchi.

Wadau wa masuala ya siasa watoa maoni yao

Mbunge wa Arusha Mjini, Goodbless Lema kupitia ukurasa wake Twitter ameandika, “Baada ya Lazaro kuondoka CCM, wamekuwa na kisasi kikubwa ambacho kimsingi kitasaidia kuondoa wavulana katika mapambano haya, bado Mameya ? Na kijana mwingine aliyekuwa shupavu 2010-2015. Msiogope kwani wanawaogopa sana ndio sababu ya matendo haya”.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Evalist Chahali amesema kitendo hicho cha wanachama wa upinzani kwenda CCM ni sehemu ya Demokrasia ambapo ameandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa,

“Leo tumesikia Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa kahamia CCM. Tayari wanachadema wameanza kumdhihaki. Ghafla wanalinganisha utendaji wake na wa mtangulizi wake John Heche. Ni kweli Patrobas alishindwa kumudu viatu vilivyoachwa na Heche lakini swali la msingi ni kwamba je kipi kilichofanya CHADEMA isichukue hatua za mabadiliko ya uongozi wa juu wa BAVICHA, na kusubiri mpaka Patrobas ahamie CCM”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *