CSI yatoa mafunzo kwa  wakunga, vifaa tiba kukabiliana na vifo vya wajawazito na watoto

Jamii Africa

Kwa mujibu wa Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) linaeleza kuwa watoto wachanga 7000 hufariki kila siku duniani kote ambapo ni sawa na watoto 21,000 kwa mwezi.

Ripoti hiyo inafafanua kuwa sio vifo vyote vya watoto vilivyotokea vilishindikana kuzuiliwa kabla ya kutokea kwake, bali vingine vilisababishwa na sababu ambazo ziliweza kuzuilika kwa wakati huo.

Zaidi ya asilimia 80 ya vifo vya vichanga husababishwa na matatizo au sababu 3 ambazo zinazuilika kabisa. Sababu au Matatizo hayo ni mtoto huzaliwa kabla ya wakati (Njiti) ambao ni watoto milioni 15 duniani kote kwa mwaka, matatizo yatokeayo wakati wa kujifungua na maambukizi ya magonjwa ukiwemo mfumo wa upumuaji.

Kila mwaka kina mama 8000 nchini Tanzania hufa wakati wa kujifungua na watoto 47,000 hufa kabla ya kuzaliwa.

Kwa mwaka 2016 Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya vifo vya vichanga duniani ambapo watoto 46 kati ya 10,000 na watoto 22 kati ya 1000 walikufa.

Tunawezaje kuzuia vifo vya wajawazito na watoto wachanga nchini Tanzania? Ni njia zipi, teknolojia, uvumbuzi, rasilimali zipi ambazo Tanzania inazihitaji ili kuwaokoa watoto wachanga na wanawake? Ni kitu gani kinapungua katika kuhakikisha wanawake na watoto wachanga wanaendelea kuishi baada ya kuzaliwa?

Kujibu maswali hayo, Shirika la Kimataifa la Childbirth Survival International (CSI) ambalo linaendesha shughuli zake katika nchi za Uganda na Tanzania limedhamiria kuboresha afya ya mama na mtoto kwa kushirikiana na wadau wa afya kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye huduma za afya ya uzazi.

Akizungumza na FikraPevu, Mwanzilishi wa CSI, Tausi Kagasheki amesema kilichowasukuma kuanzisha shirika hilo ni kukabiliana na vifo vya wanawake na watoto wachanga kwa kutoa vifaa, elimu ya uzazi, mafunzo kwa wahudumu wa afya na jamii.

“Kilichotufanya tuanzishe shirika la CSI ni vifo vya akina mama vinavyotokea kila siku. Mama ndiye anasimamia kila kitu, namna wakina mama wanavyofariki inabidi mtu au washirika waongeze kasi ili hawa akina mama waweze kupata huduma katika hospitali, msaada katika jamii zao, familia zao ili waweze kupata huduma wakati wa ujauzito na wanapojifungua”, amesema Tausi.

Amesema matatizo ya vifo vya watoto wachanga, yanaanza tangu mtoto akiwa tumboni. Kwahiyo ili kuhakikisha mtoto anazaliwa na kuishi ni lazima jamii iingalie kwanza afya ya mama mjamzito na kumpatia huduma zote anazostahili kwasababu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji nguvu ya pamoja kuzishughulikia.

“Hamna changamoto moja kuna changamoto nyingi. Na hizo changamoto zote ukitazama kwa upande wa hospitali kuna changamoto, katika jamii kuna changamoto lakini yeye mama mjamzito kwa mfano mama wa kijijini yeye ndiye ana changamoto zaidi kwasababu kule hakuna hospitali na hata kama zipo hazina vifaa, hazina wakunga, hazina dawa”, amesema Tausi na kuongeza kuwa,

“Unakuta huyo mama anapata changamoto nyingi, wengine wanachelewa kwenda kwasababu wanajua wakienda hawatapa huduma. Changamoto nyingine ni usafiri, umasikini na hali ilivyo sio Tanzania peke yake”.

Anaongeza kuwa katika kukabiliana na changamoto za vifo vya watoto wachanga, CSI wanatoa vifaa (delivery kits) kwa wajawazito wakati wa kujifungua ili kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa salama kabla na baada ya kuzaliwa.

“Sisi CSI tunawadhamini wakina mama childbearing kits (vifaa vya kujifungulia), hizi kits (vifaa) zina kila kitu, zina grooves, pamba vitakavyomsaidia mkunga kumzalisha huyu mama vizuri. Kwasababu mara nyingi wanatakiwa wanunue vifaa ambavyo hawawezi. Hawawezi hawana fedha  za kununua hivyo vifaa”, amebainisha Tausi.

Mpaka sasa Shirika hilo limefanikiwa kuwasaidia wajawazito 350 nchini Tanzania na Uganda kwa kuwapatia vifaa vya kujifungulia, lakini wametoa elimu kwa wakunga ili kuwaongezea uwezo wa kuwahudumia wajawazito na watoto wachanga ambao hawajafikisha mwezi mmoja.

Ameongeza kuwa, “Tunachofanya tunawaelimisha wakunga kuboresha ujuzi wao katika kuzalisha akina mama, namna gani ya kumsaidia mtoto kama amechoka, kumchangamsha haraka haraka,  wengine amechoka tu kwasababu hapati ile huduma ya haraka katika ule muda sahihi unakuta mtoto anafariki”.

Kwa upande wake Meneja Programu wa CSI , Easter Mponda amesema ili kuhakikisha afya ya mama na mtoto inazingatiwa wanatoa elimu ya uzazi na kujitambua kwa wasichana waliopo shuleni ili kuwaandaa kimakuzi na kisaikolojia kukabiliana na changamoto cha uzazi.

“Tunamuelimisha mtoto wa kike jinsi ya kuwa msafi, kujiweka msafi ili asipate magonjwa, fangasi zinazoweza kuharibu kizazi chake. Pia kuwafanya wakajitambua tunapokuwa katika mafunzo huwa wanauliza vitu ambavyo hawawezi kuwauliza wazazi wao”, amesema Easter.

CSI ni shirika lisilo la kiserikali na lilianzishwa mwaka 2013 na wanawake wawili, Stella M. Mpanda na Tausi Suedi Kagasheki ambao wana uzoefu wa muda mrefu kwenye sekta ya afya ambapo wanaamini upatikanaji wa huduma bora za uzazi ni haki ya msingi ya mwanamke na mtoto.

Siku ya leo wanatarajia kuadhimisha miaka 5 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo ambapo Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi. Pia ataongoza mazungumzo ya wadau wa afya ili kutengeneza mpango kazi na mikakati itakayosaidia kupunguza vifa vya wanawake na watoto wachanga nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *