Dalili zaonesha Magufuli, Kagame, Museveni kukosa tuzo za Mo

Jamii Africa

Zaidi ya shilingi trilioni 10 zinazotolewa bure kwa rais mstaafu wa nchi ya Afrika aliyetenda vyema kwenye uongozi wake, huenda zikachukua miaka mingi kuchukuliwa na viongozi wa Afrika Mashariki.

Hali hiyo inatokana na viongozi wa eneo hilo la Afrika kuwa na aina ya uongozi unaopingana na misingi ya utawala bora.

Viongozi hao wanatajwa kupenda kung’ang’ania madaraka, kuminya demokrasia, kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na kibaya zaidi kushindwa kukabili rushwa hata kama majukwani wanajisifu au kusifiwa kutokomeza rushwa.

Fedha hizo hutolewa kila mwaka na bilionea Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, mwenye asili ya Afrika, kutoka nchini Sudan, akiwa anaishi na kufanya biashara zake maeneo mengi duniani na mwenye makao makuu, London, Uingereza. Ndiye mwanzilishi wa kampuni za simu za mkononi ikiwamo Celtel.

Dalili za viongozi wengi wa Afrika Mashariki zinaonesha itawachukua muda mrefu, hata kufikia miongo miwili au zaidi, kuibuka washindi wa tuzo za tajiri huyo zinazoambatana na zawadi ya dola za Marekani milioni 5 (zaidi ya shilingi za Tanzania trilioni 10).

Tangu kuanza kwa tuzo hizo, ambazo miongoni mwa majaji ni Mtanzania, Dk. Salim Ahmed Salim, miaka 10 iliyopita, hakuna kiongozi wa Afrika Mashariki mstaafu aliyeshinda. Majaji wengine ni Martti Ahtisaari, Aïcha Bah Diallo, Horst Köhler, Dk Graça Machel, Festus Gontebanye Mogae, Mohamed ElBaradei na Mary Robinson.

Wachambuzi wa masuala ya siasa na demokrasia wa eneo hilo na hata nje ya Afrika, wanaeleza kuwa viongozi walioko madarakani sasa; Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Pierre Nkurunziza wa Burundi, Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), tayari wamekosa sifa za kufikiriwa kupata tuzo hizo kwa namna wanavyoongoza nchi zao.

Rais John Magufuli (kulia) akisalimiana na rais wa Rwanda, Paul Kagame (kushoto) na anayeshuhudia ni rais wa Uganda, Yoweri Mseveni (Katikati), wakati rais Magufuli akiapishwa mwaka 2015 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya viongozi hawa wamekuwa wakitajwa kuwa na “harufu” ya udikteta na wapinzani wao, wanaharakati na hata viongozi wa dini.

Inaelezwa kuwa utawala bora ambao ni mhimili wa tuzo hizo, hauonekani kuwamo katika kamusi ya viongozi hao, hata kama yapo baadhi ya maeneo wanaonekana kufanya vyema.

Tayari Rais Kagame, kama ilivyo kwa Nkurunziza, Museveni na Kabila ameshindwa kuenzi na kuheshimu katiba ya nchi yake kwa “kulazimisha” kuongezwa muda wa wao kukaa madarakani.

Viongozi hawa wamekuwa wakiieleza dunia kuwa wananchi wenyewe ndiyo wameamua wao waendelee kuongoza.

Ukiacha Rais Magufuli wa Tanzania ambaye ametangaza, kama hao wengine walivyotangaza awali; kwamba hataki kubadili katiba ili ajiongezee muda wa kuwepo madarakani.

Rais Magufuli tangu kuingia madarakani amejipambanua kuwa ni kinara wa kupambana na rushwa na maovumengine katika nchi yake, lakini anatajwa kushindwa kabisa kuruhusu kukua kwa demokrasia na kumea kwa uhuru wa vyombo vya habari. Hizi ni sababu za kumuweka pembeni katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo hiyo yenye heshima kubwa.

Katika Tanzania, Mbunge wa  Chemba (CCM), Juma Nkamia alianza kumpigia debe Rais Magufuli ili aendelee kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka miwili zaidi – iwe saba badala ya mitano ya kikatiba, hata baada ya kumaliza muda wake wa kikatiba kukaa Ikulu ya nchi hiyo iliyopo Magogoni, Dar es Salaam.

Msimamo huo wa Nkamia, akiwa amewasilisha muswada binafsi bungeni, umeonekana kuungwa mkono na baadhi ya wanachama wa chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye yeye alikwenda mbali zaidi akitamani Rais Magufuli aongoze milele.

Inaelezwa kuwa sababu kubwa ya viongozi hao kuendelea kubaki Ikulu, kutokana na uchu wa madaraka na kushindwa kuamini maisha yao “yatakuwaje” baada ya kuachia madaraka. Hawaamini mwingine zaidi ya wao wenyewe.

“Viongozi hawa hawaamini wanaoweza kuwaachia madaraka kwa kuwa wamewahi kufanya madudu mengi, sasa wanaogopa mkondo wa sheria, ingawa wengine wamejijengea mazingira ya kutoshitakiwa wakiachia madaraka,” anasema Isaya Khalesi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kutathmini Maendeleo Tanzania akizungumza na FikraPevu.

Khalesi anasema baadhi ya viongozi wanaotajwa kukosa sifa za kupata tuzo hizo, waliingia madarakani kwa mtutu wa bunduki, hivyo hawataki kuyaachia “kirahisirahisi.”

Nchini Tanzania, Rais Benjamin Mkapa (1995 – 2005) aliwahi kutajwatajwa kuwa huenda angepata tuzo hiyo, lakini haikuweza kutokea na wachunguzi wa mambo walisema kiongozi huyo wakati wa uongozi wake, pamoja na kupunguza sana rushwa, alihusishwa na tuhuma za kutumia vibaya madaraka yake. Mkapa aligundulika kushirikiana na mkewe, Anna kuanzisha kampuni iliyoitwa AnBem ambayo ilinunua kiwanda cha makaa ya mawe cha Kiwira kwa bei ya kutupa.

Rais Jakaya Kikwete (2005 – 2015) pamoja na kutoa uhuru mkubwa kwa vyombo vya habari na kuwapa fursa wanasiasa na vyama vyao kufanya shughuli zao, alishindwa kudhibiti rushwa na katika kipindi chake, Tanzania iligubikwa na rushwa kubwa ambazo zilitikisa nchi. Rushwa zilizizoibuliwa na wabunge na vyombo vya habari ni pamoja na Richmond, Escrow, EPA na Rada.

 

Washindi wa Mo Ibrahim

Viongozi wastaafu wa nchi za kusini mwa Afrika, wameendelea kuzoa tuzo ya Mo kwa kuwa wameonekana kuzingatia utawala wa sheria, kuimarisha demokrasia na kutoa uhuru mkubwa wa habari.

Waliopata tuzo hizo kutoka eneo hilo ni pamoja na marais Joacquim Chisasan wa Msumbiji (2007), Festus Mogae wa Botswana (2008) na Hifikepunye Pohamba wa Namibia (2014). Mwaka 2011 mshindi alikuwa ni Rais Pedro Verona Pires wa  Cape Verde, nchi iliyoko kaskazini magharibi mwa Afrika.

Mwaka 2009, 2010, 2012, 2013, 2015 na 2016, kamati ya kuchagua washindi haikuona kiongozi mstaafu aliyekuwa akistahili tuzo hiyo na kuibuka na kitita cha trilioni 10/-.

Mwaka 2017, mshindi wa tuzo ya mwaka ya ‘Mo Ibrahim’ imeenda kwa mwanamama Ellen Johnson Sirleaf ambaye ndiyo kamaliza awamu yake ya pili ya urais nchini Liberia. Ellen Johnson, mwanamke wa kwanza kuwa rais kwa nchi za Afrika ameondoka madarakani kwa kuiacha Liberia kwenye hali nzuri ya uchumi, haki za binadamu, utawala bora na demokrasia.

Kiongozi anayepata fedha hizo yuko huru kuzitumia anavyopenda na habanwi na taratibu za tuzo hiyo inayotimiza miaka 10 sasa tangu kuanza kwake.

Je, katika Tanzania, nani ategemewe kupata tuzo hiyo? Ni Rais Magufuli kama ataamua kubadilika au tuendelee kusubiri kwa miaka mingine mitano, saba  au kumi kabisa?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *