Dini, CCM, Mabadiliko na Kingunge

Jamii Africa

MENGI yaliandikwa, yanaandikwa na yataandikwa kuhusu maisha, elimu, kazi, familia na ushiriki wake katika siasa za Tanzania na maeneo mengine.

Anayezungumzwa hapa ni Kingunge Ngombale Mwiru; mwanasiasa na mwanafalsafa kindakindaki wa Tanzania ambaye amefariki dunia Januari 2, 2018.

Katika maandishi ya baadhi ya waandishi na wachangiaji wengine, wapo wanaodai kuwa Kingunge (87) hakuwahi kuamini uwepo wa Mungu. Kwamba hakuamini katika uumbaji wa dunia na viumbe waliomo humo.

Nikiwa mwandishi ambaye, siyo mara moja wala mbili, aliyewahi kuzungumza na Kingunge juu ya habari hiyo pamoja na mambo mengine, mzee huyo amekuwa akikanusha juu ya mtazamo huo na kudai kuwa “analishwa maneno.”

Amekuwa akieleza kuwa hajawahi kutamka kwamba hatambui uwepo wa Mungu, lakini ni kweli kuwa amehoji sana baadhi ya maandiko ya Biblia na si kweli kuwa hakuwa au hakuamini katika dini kama wengi wanavyoamini. Tembelea hapa uone moja ya mjadala – "Inasemekana marehemu Mzee Kingunge hakuwa na Dini, atazikwa kwa Utaratibu upi?"

“Sina ugomvi na uwepo wa Mungu na hili siyo la kuhoji, isipokuwa ndani ya Biblia na vitabu vingine vinavyoitwa vitakatifu, yapo mambo yanayofikirisha na kujenga uwanja mpana wa kuhoji. Binadamu mkamilifu anapaswa kuhoji na kuwaza juu ya kile anachosoma, kuambiwa na hata kufanya na haya ndiyo yanatutofautisha na wanyama wengine,” hii ndiyo imekuwa kauli ya Kingunge mara kwa mara anapotetea msimamo wake.

                                                Kingunge Ngombale Mwiru wakati wa Uhai wake  akiwa kada wa CCM (Picha kwa hisani ya Edwin Mjwazi) 

Anasema kuendelea kuhoji masuala ya Imani ya Kikristo, kupitia maandiko ya Biblia, kulimfanya ajiweke pembeni kidogo ya kanisa ili ajitafakari na kujua zaidi juu ya waandishi wa vitabu vya Biblia, maisha ya manabii na ukweli, ikiwa pamoja na ulinganifu wa maisha ya sasa.

Kingunge aliniambia mtu mwenye akili timamu hawezi kukataa uwepo wa Mungu, ingawa anaweza kuhoji maandishi yaliyoandikwa enzi za Yesu na “wakubwa” wengine wa wakati huo.

Kwa kauli yake, Kingunge alisema; “hivyo vitabu vitakatifu vilinipa shida sana na sikuacha kuvisoma, sasa kuondoa usumbufu, nikaamua kujiweka pembeni kwanza huku nikiendelea kudadavua. Na bado sijamaliza.”

Je, alipanga kumaliza lini kudadavua? “Hii kazi ya kudadavua ni kuchimba na kuchimbua maandiko yale, yapo mengi, so (hivyo) sijui nitamaliza lini, inaweza kuwa kazi ya kufa nayo hii,” alimaliza Kingunge.

Huenda siku chake kabla mauti hayajamkuta Kingunge, bado aliendelea kudadavua maandiko, ingawa familia yake, siku mbili baada ya kufariki kwake, imeeleza kuwa mzee huyo mwanafalsafa alirejea kwenye Imani ya Katoliki, hivyo atazikwa Kikatoliki kesho, Jumatatu.

Kingunge amekuwa akikanusha kuwa yeye ni Mkomunisti na kueleza kuwa anaweza kuwa mwanafalsafa na gwiji wa mawazo huru, ambaye hachoki kuhoji na mwenye kusimamia kile anachokiamini.

Katika maelezo yake, Kingunge anasema aliambukizwa “ukorofi” wa kuhoji Ukristo na maeneo mengine hasa baada ya kusoma kitabu kilichoandikwa na Mjerumani Ludwig Feuerbach (1804-1872) kiitwacho The Essence of Christianity pamoja na maandishi mengine ya wanazuoni wa kale, ambao walinoa ubongo wake kuwa na ncha kali ya kuhoji kila kitu.

Ni kutokana na msimamo huo, huenda Kingunge, aliamua kujiweka pembeni katika harakati za kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), alichokiasisi pamoja na Mwalimu Julius Nyerere na wengine, baada ya kuona mambo mengi hayaendi sawa. Moja ya mambo hayo ni namna ambavyo CCM ilichagua mgombea wake wa urais mwaka 2015.

Kingunge ni mwanachama wa CCM mwenye kadi namba 8. Kadi namba 1 ni ya Mwalimu Nyerere.

Akiwa pembeni ya CCM, Kingunge aliamua kuunga mkono harakati na vuguvugu za mabadiliko zilizoasisiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuonekana majukwani akiwanadi wagombea wa chama hicho cha upinzani na Umoja wa vyama vya upinzani uliopewa jina la UKAWA.

Hata hivyo, hadi umauti unamkuta, Kingunge hakuweka wazi kuwa mwanachama wa Chadema wala vyama vingine vya upinzani.

Katika maisha yake yote ya kuhoji, wakati mwingine akionekana mkorofi, Kingunge alikuwa na sifa moja kubwa; uzalendo na mwenye msimamo usiyoyumbishwa. Amewahi kunukuliwa akieleza msimamo huo.

Hakuogopa kueleza kinagaubaga juu ya uzalendo wake, siyo kwa maneno tu, bali vitendo vyake vilifuata msimamo huo na huenda kuunga mkono wapinzani, aliona uzalendo zaidi kuliko humo alimokuwa tangu ujana wake na siku chache kabla ya kuwa mwanamabadiliko.

Yapo mengi mazuri na mengine yenye changamoto juu ya misimamo ya mwana huyu wa Tanzania ambaye pumzi yake imekata na sasa mwili wake wasubiri kufukiwa ardhini, ikiwa ndiyo mwisho wa kuhoji na “ukorofi” wake.

Ewe Kingunge, lala salama.

 

Makala hii imeandikwa na Simon Mkina

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *