Dkt. Mpango: Sekta ya kilimo inakwamishwa na ukosefu wa miundombinu ya umwagiliaji

Jamii Africa

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema nchi inakabiliwa na ukuaji mdogo wa sekta ya kilimo ambao unakwamishwa na ukosefu wa miundombinu ya umwagiliaji na unaweza kuathiri juhudi za serikali kuifikisha serikali kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Dkt. Mpango amesema ukuaji wa sekta ya kilimo unakwamishwa na ukosefu wa mbegu bora, miundombinu ya umwagiliaji na uhakika wa soko la mazao yanayolimwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kulingana na Benki ya Dunia (WB) katika ripoti yake ya Mapitio ya Uchumi ya mwaka 2017 inaeleza kuwa Tanzania ina ardhi kubwa lakini ni asilimia 1.5 ya ardhi ya umwagiliaji ndio inatumika, huku 80% ya ardhi ya umwagiliaji inalimwa kwa njia za kienyeji na maji yanayotumika hayazidi 15% ya maji yote yanayopaswa kutumika katika kilimo hicho.

Amesema sekta ya kilimo imeajiri asilimia 70 ya watanzania wote lakini hajafanikiwa kupunguza umasikini na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana kwasababu ya uwekezaji mdogo ambao hauendani na mahitaji ya sekta hiyo.

“Taifa bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana, kiwango cha umasikini bado kiko juu, ukuaji mdogo wa Sekta ya kilimo ambayo imeajiri takribani asilimia 70 ya watanzania unaosababishwa na ukosefu wa mbegu bora, miundombinu ya umwagiliaji na soko la uhakika, na kupungua kwa mikopo ya benki za biashara kwa sekta binafsi pamoja na mambo mengine,” amesema Dkt. Mipango.

Kutokana na sekta ya kilimo kutofanya vizuri imeathiri ukuaji wa uchumi kwa sehemu kubwa na utoaji wa huduma muhimu za jamii ikiwemo elimu, maji, umeme na afya na kutishia mkwamo wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa kutambua hilo, serikali imeiomba Benki ya Dunia mkopo wa Dola za kimarekani milioni 150 kwaajili ya kutatua changamoto za uchumi na utekelezaji wa mpango wa utoaji wa huduma (Growth and Service Delivery) muhimu kwa wananchi na kuimarisha utendaji wa umma.

“Serikali imedhamiria kwa dhati kujenga uchumi imara kwa kuendeleza viwanda na kuweka mazingira mazuri ya biashara ili kuvutia wawekezaji wa ndani na wale wa nje kuja kuwekeza nchini, kujenga miundombinu ya barabara, reli, umeme, viwanja vya ndege na kuongeza uwekezaji katika utoaji wa huduma za jamii kama vile elimu, afya na maji”, amesema Dkt. Mpango.

Uamuzi huo wa serikali umefikiwa leo wakati Dkt. Mpango alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi mkuu wa Uchumi, Biashara na Uwekezaji wa Benki ya Dunia, Dkt. Carlos Felipe Jaramillo ambaye yuko nchi kwa ziara ya kikazi.

Kwa upande wake, Dkt. Jaramillo amepokea ombi la serikali na ameishauri serikali kuwekeza zaidi katika rasilimali watu na miundombinu ili kulifanya Taifa kuweza kuhimili ushindani wa kimataifa duniani na kujenga uchumi unaokua na endelevu.

Aidha, alieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita uwekezaji kutoka nje umekuwa zaidi katika Sekta ya madini, hivyo ameishauri Serikali kuigeukia sekta hiyo na  kuweka mazingira mazuri ya biashara ili kuwavutia wawekezaji kutoka nje kuwekeza katika sekta za kilimo, viwanda na utoaji huduma ili kuongeza wigo wa shughuli za kiuchumi na kuchochea ukuaji wake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *