Dkt. Slaa afunguka Lissu kupigwa risasi, apinga rais kuongezewa muda wa uongozi

Jamii Africa

Balozi Mteule na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Wilbroad Slaa amesema tukio la Tundu Lissu kupigwa risasi na watu ‘wasiojulikana’ ni jambo la kawaida na ameitaka jamii kuliacha Jeshi la Polisi kukamilisha upelelezi na kutoa majibu.

Dkt. Slaa ametoa kauli hiyo wakati akihojiwa na kituo cha runinga cha Clouds juu ya hali ya kisiasa ya Tanzania na mustakabali wa maisha yake baada ya kuondoka CHADEMA, amesema hafurahishwi na baadhi ya watu kuwataja hadharani watuhumiwa wa tukio hilo kwasababu linaharibu uchunguzi wa polisi.

“Mimi kinachoniudhi ni hii watu kusema hadharani kwamba kuna hiki na hiki tunasuspect (tunahisi) waliofanya ni fulani. Sheria inasema ukihisi nenda polisi katoe taarifa sio unaenda kwenye vyombo vya habari”, amesema Dkt. Slaa.

Amesema hawezi kuzungumzia kwa undani suala la Lissu kupigwa risasi, ikizingatiwa kuwa watu wengi wamepigwa risasi nchini na kazi ya kuwabaini wahalifu waliomshambulia ni ya polisi sio viongozi wa siasa au wananchi.

“Lakini kama binadamu hakuna anayependa binadamu yeyote aumizwe lakini matukio haya ya kuumizwa yametokea nchi hii kwa watu wengi sana. Na mimi sio chombo cha dola kujua kwamba unanyoosha kidole kwa kitu ambacho hatukiamini; mimi ni msomi”, amesema Dkt. Slaa.

Dkt. Wibroad Slaa

Ikumbukwe baada ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kupigwa risasi na watu ‘wasiojulikana’ mjini Dodoma Septemba 2017, baadhi ya wanasiasa wa upinzani walijitokeza na kudai kuwa wanahisi kuwa tukio hilo lina mkono wa dola.

Lissu amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais John Magufuli hasa kwenye masuala ya sheria na utawala bora, mara kadhaa ametishiwa kufuatiliwa na watu ‘wasiojulikana’ na kutakiwa kuacha msimamo wake wa kuhoji mamlaka za nchi.

Amebainisha kuwa huenda upelelezi wa tukio la Lissu umeharibika kwasababu baadhi ya wanasiasa wamekimbilia kwenye vyombo vya habari kutoa taarifa ambazo zingesaidia kuchunguza na kuwakamata waliompiga Lissu risasi.

Dkt. Slaa ameongeza kuwa hata Canada ambako alikuwa anaishi baada ya kuingia kwenye mgogoro na Chama chake cha CHADEMA, matukio ya watu kuumizwa na kupigwa risasi yanatokea kila siku lakini taarifa za matukio hayo hazitolewi hadharani mpaka upelelezi ukamilike.

“Ukitoa taarifa za upelelezi unaharibu upelelezi. Mimi niko Canada mauaji yapo kila siku na watu wanapotea, wanapigwa risasi wakiulizwa polisi wanakwambia suala hilo liko kwenye upelelezi tukifikia hatua nzuri tutatoa taarifa”, amefafanua Dkt. Slaa.

Lakini alipotakiwa na watangazaji wa kipindi hicho kumuelezea Lissu kwa undani, Dkt. Slaa amekataa kutoa maoni yake. Akizungumzia usalama wake wakati akiwa CHADEMA, amesema alikuwa na mtandao mpana wa kumlinda dhidi ya wabaya wake lakini kwa sasa hana mtandao huo.

Pia amezungumzia suala la rais kuongezewa muda wa kuongoza kutoka miaka 5 hadi 7, “Katiba isichezewe kabisa ibakie hivi ambavyo ilivyo sikubaliani na jambo la kuongeza muda kwa Uongozi wa Rais”. Amevitaka vyama vya upinzani kujikita kwenye siasa za masuala na kuachana na mivutano isiyokuwa na tija kwa maendeleo ya taifa.

“Mimi ni muumini wa Demokrasia, Napenda uwepo wa vyama vingi lakini si utitiri wa vyama hali ya muelekeo wa kisiasa nchini kwasasa haunifurahishi kabisa. Sioni mikakati na uelekeo wa vyama vya siasa kwasasa, Haiwezekani vyama vijikite katika kuchambua kauli ya mkubwa wa nchi sababu haya mambo hayana tija kwa Wananchi. Vyama vya upinzani vije na sera mbadala”, amesema Dkt. Slaa.

Rais John Magufuli alipokutana na Balozi Mteule, Dkt. Wilbroad Slaa ikulu jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.

Dkt. Slaa aliondoka nchini mwishoni mwa mwaka 2015 baada ya Lowassa kuingia CHADEMA na kupewa nafasi ya kugombea urais ambapo alikimbilia nchini Marekani na baadaye akapata hifadhi nchini Canada. Inaelezwa kuondoka kwake kulikuwa njia mojawapo ya kujilinda dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa ikizingatiwa kuwa chama chake hakikumpa nafasi ya kugombea urais.
“Nilikimbilia tu Canada kwasababu ni nchi yenye rekodi nzuri ya kulinda haki za binadamu”.

Tangu wakati huo ameendelea kuishi nchini Canada mpaka alipopata taarifa Novemba 23, 2017 za kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa balozi akisubiri kuapishwa na kupangia kituo cha kazi.
Hata hivyo, Dkt. Slaa amerejea nchini Januari 28 mwaka huu na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo aliipongeza serikali ya awamu ya tano kwa uongozi bora wenye maono na uthubutu wa kutekeleza mambo makubwa yenye maslahi kwa nchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *