Elimu ya Awali: Ruzuku ya chakula kuchochea uelewa kwa wanafunzi  

Jamii Africa

Mwaka 2010, Serikali  ilitoa agizo kwa shule zote za msingi nchini kuwa na madarasa ya awali ili kuwaandaa watoto kabla ya kujiunga darasa la kwanza. Agizo hilo limetekelezwa na madarasa hayo yameanzishwa lakini changamoto inabaki uwekezaji mdogo wa serikali katika elimu hiyo ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Kutokana na uwekezaji hafifu wa elimu ya awali katika shule za umma imesababisha shule hizo kukosa ushindani unaotakiwa ikilinganishwa na shule za binafsi ambazo zinafanya vizuri. 

Mtaala wa Elimu ya Awali Tanzania toleo la 2013 unabainisha kuwa elimu ya awali ni ngazi ya kwanza katika mfumo wa elimu ya Tanzania ambayo hutolewa kwa watoto wadogo kabla ya kujiunga na elimu ya msingi. Elimu hii hutolewa kwa watoto kuanzia miaka 5 mpaka 6 kwa lengo la kuwapa maarifa, stadi na mielekeo ambayo itawasaidia kupambana na maisha yao ya kila siku na pia kuwaandaa kwa elimu ya msingi.

Mtaala wa elimu ya awali umezingatia masuala mbalimbali ya kijamii ambayo huchochea ukuaji wa mtoto katika nyanja zote. Mambo hayo ni pamoja na lishe bora, afya bora, uangalizi, mahusiano ndani ya familia, vifaa na viwanja vya michezo na mila na desturi. 

Lengo kuu la elimu ya awali ni kuwaandaa watoto kwa elimu ya msingi ambayo ni ngazi ya pili. Hapa ndipo msingi wa mtoto kupata elimu huandaliwa. Kama msingi huu usipojengwa vizuri, elimu ya wanafunzi huwa mashakani.

Licha ya Mtaala wa elimu kubainisha mambo ya msingi ya kuweza kufanikisha elimu ya awali, lakini serikali haitoi ruzuku kwa wanafunzi wa elimu hizo ili kuweza kugharamia mahitaji yao wawapo shuleni. Hali hiyo imesababisha wanafunzi hao kukosa chakula  katika baadhi ya shule jambo ambalo linaathiri mwenendo wa kujifunza na kupokea maarifa mapya.

“Zamani tulikuwa tunakunywa uji shuleni hata wanafunzi wa chekechea pia hawapati uji kwa sasa” Maneno hayo ni ya mwanafunzi Mahimu Athuman, mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Victoria iliyopo jijini Dar es salaam.

Anasema wakati mwingine wanakaa na njaa siku nzima bila kula chochote, ambapo wanafunzi hao hulazimika kununua chakula kwenye magenge yaliyo karibu na shule.

“Hatupewi chakula shuleni sijui kwa nini?, ila tunanunua chakula kinachouzwa kwenye magenge yaliyo pembeni mwa shule wakati wa mapumziko” anasema mwanafunzi Mahimu.

Sio wanafunzi wote wenye uwezo wa kununua chakula hicho. Wengine wanatoka familia maskini ambazo hazina uwezo wa kumudu mahitaji ya watoto hasa wale ambao wanasoma madarasa ya awali katika shule za serikali.

Wanafunzi wakipata chakula

Tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa wanafunzi wanaopata chakula wawapo shuleni, wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika masomo na kuongeza ufaulu katika mitihani yao. Mkoa wa Kilimanjaro umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa huduma ya chakula mashuleni na shule nyingi za mkoa huo zinafanya vizuri katika elimu.

Kutokana na changamoto hiyo, wazazi kupitia kamati za shule katika baadhi ya maeneo wameweka utaratibu wa kuchangishana fedha kwa ajili ya kutoa chakula kwa wanafunzi wa madarasa ya awali ili watulie darasani na kufuatilia masomo.

“Kila mwezi tunatoa shilingi 30,000 kwa ajili ya chakula, ambapo watoto wetu wanakunywa uji na kupata chakula cha mchana”, anaeleza Sara Robert mkazi wa Kijitonyama ambaye mtoto wake Miriam Robert anasoma katika darasa la awali lilipo mtaa wa Alimaua A.

Wazazi wengi hulazimika kuwapeleka watoto wao katika shule za binafsi ambazo zina mazingira rafiki ikiwemo upatikanaji wa huduma ya chakula. Lakini sio wazazi wote wenye uwezo wa kuwapeleka watoto wao katika shule hizo kutokana na gharama kubwa ambazo hawawezi kuzimudu.

Serikali inapaswa kuitazama upya elimu ya awali na kuzifanyia kazi changamoto zilizopo kuwajengea watoto mstakabali mzuri wa maisha.

Wadau wa elimu kupitia Chapisho la ‘Kudidimia kwa Elimu ya Awali; Chanzo nini?’ linalotolewa na shirika la HakiElimu wanashauri kuwa “Wanafunzi wetu wa elimu ya awali wanahitaji mazingira mazuri ya kujifunzia, madarasa na vifaa vya kutosha pamoja na walimu wenye mafunzo maalumu.

“Pia,serikali inapaswa kutoa ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya awali . Yote haya yakifanyika kwa ufanisi wanafunzi wa elimu ya awali watasoma katika mazingira mazuri”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *