EPA kutawala kikao cha wakuu wa nchi Jumuiya ya Afrika Mashariki, Magufuli kutoa neno

Jamii Africa

Rais John Magufuli amewasili nchini Uganda kushiriki mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kuanza ijumaa na kutawaliwa na ajenda ya kusainiwa kwa Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) na Umoja wa Ulaya (EU).

Mkutano huo unafanyika katika jiji la Kampala na unahudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi za Uganda, Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Inaelezwa kuwa kuwasiri kwa rais Magufuli kulisubiriwa kwa hamu ikizingatiwa kuwa Tanzania itatoa msimamo wake juu kusainiwa kwa mkataba wa EPA ambao unafungua fursa za masoko kwa bidhaa za Afrika Mashariki kuuzwa katika nchi za EU bila kutozwa ushuru.

Nchi nyingine ambayo hazikusaini mktaba huo ulioasisiwa mwaka 2010 ni Burundi ambayo imeitaka EU kuiondolea vikwazo vya kisiasa ambavyo viliwekwa kutokana na hali tete ya kisiasa nchini humo. Lakini nchi za Kenya na Rwanda tayari zimesaini mkataba huo.

 Tanzania nayo ilitoa sababu zake mwaka 2016 kwamba isingeweza kusaini mktaba huo kwa kuwa vipengele vya mkataba vinakwamisha jitihada za serikali kuifanya nchi kuimarisha viwanda vya ndani na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

Kipengele kimojawapo kinataka bidha kutoka nchi za Umoja wa Ulaya ziingie kwenye nchi yoyote ya Afrika Mashariki, jambo ambalo Tanzania ilipinga na kutaka kipengele hicho kibadilishwe ili kuhakikisha inapata fursa ya kushindana kwenye soko la bidhaa za viwandani.

Uwepo wa rais Magufuli kwenye kikao hicho umebeba siri nzito ikiwa Tanzania itaridhia kusaini mkataba huo kama zilivyofanya nchi za Kenya na Rwanda  au itashikiria msimamo wake?

Uganda na Sudan Kusini bado hazijasaini mkataba huo lakini ziko tayari kwa majadiliano ili kubaini manufaa yatakayopatikana. Kenya imesaini kwasababu inasafirisha bidhaa zake za maua na mboga mboga katika nchi za Ulaya na tayari iko kwenye uchumi wa kati.

“Hoja yetu sio kupinga biashara na Afrika Mashariki, tunachotaka ni kuona ubia huu unanufaisha pande zote. Tunazo taarifa nyingi za kitafiti hata kutoka Kituo cha Kimataifa cha Biashara zinazoonesha kuwa mkataba huu utakuwa na hasara kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.”, alisema Marie Arena, mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki ambaye alinukuliwa na chombo kimoja cha habari mwaka 2017.

“Tunaamini mkataba huu kwa namna ulivyo sasa hauko sawa. Ulaya unaitumia Kenya ambayo ndiyo yenye maslahi zaidi katika mkataba huu kama ngao yao. Wakati Kenya ilishaendelea kiviwanda hali sio ilivyo kwa Tanzania, Uganda na Burundi ambazo hazitafaidika”.

 

Viongozi wakuu wa Nchi za Afrika ya Mashariki wakisimama wakati wimbo wa umoja wa nchi hizo ukipigwa katika mkutano wa 17 wa EAC uliofanyika mkoani Arusha, mwaka 2017 

 

Mseveni kutoa mrejesho

Katika kikao hicho rais wa Uganda, Yoweri Mseveni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo anatarajia kutoa mrejesho wa mkutano wake aliofanya na Kamisheni ya EU mwaka 2017 juu ya manufaa ya EPA kwa uchumi wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia ataeleza hatua zilifikiwa na EU katika kuiondolea Burundi vikwazo vya kisiasa kwasababu ni mwanachama wa Afrika Mashariki.

“Burundi naye ni mwenzetu amesema hawezi kujadili masuala ya EPA wakati tayari amewekewa vikwazo. Tunawataka EU waondoe vikwazo kwa Burundi hili sio suala la kuweka saini mara moja wakati bado hatuko pamoja”, alinukuliwa rais Mseveni katika kikao cha wakuu wa nchi wa jumuiya ya Afrika Mashari mwaka 2017.

Hata hivyo, mkutano huo wa wakuu wa nchi unatarajia kujadili ajenda zingine ikiwemo; mafungamano ya biashara ndani jumuiya ambayo yanateteleka, ushuru wa forodha, ujenzi wa miradi ya reli ya kisasa (SGR), bomba la mafuta kutoka Tanzania hadi Uganda, ubadilishaji wa bidhaa na suala la mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.

 

EPA ni nini?

Ni mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi  kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao unatoa fursa kwa bidhaa viwandani za Ulaya kuingia Afrika Mashariki na zile za Afrika Mashariki kwenda Ulaya.

Masharti ya mkataba unatakiwa kusainiwa na nchi zote wanachama wa EAC ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Faida za mkataba huo ni kuondolewa kwa ushuru wa forodha lakini manufaa hayo yatazifaidisha nchi za EU kwasabu zimeendelea kiviwanda na teknolojia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *