Fahamu njia 5 za kukusaidia kukumbuka kila kitu ulichosoma

Jamii Africa

Kwa mujibu wa Jhumpa Lahiri katika kitabu chake cha The Namesake anasema, “ Kusoma kitabu ni kitendo cha kusafiri bila kusogea kutoka pale ulipo”. Naye David Bowie msanii ajulikanaye kama msomaji mkubwa wa vitabu; alipokuwa akijibu maswali mbalimbali aliyoulizwa kwenye dodoso, alipoulizwa kuhusu maana halisi ya “furaha ya kweli ni ipi?”, Bowie alijibu ni kusoma.

Hata hivyo, kuna haja gani kusoma kama huwezi kukumbuka ulichokisoma? Hakuna kitu kinakatisha tamaa kama kuwekeza muda wako kusoma kitabu fulani halafu baadaye ukasahau vyote ulivyosoma. Kuendelea kusoma kitabu fulani ambacho taarifa zake za mwanzo umezisahau ni kama kusoma kitabu kipya kwa kuanzia katikati ya matukio.

Kama tunavyofahamu ufanisi wa ubongo ulivyo, kusoma vitabu vyenye matukio halisi (Non-fiction) inaweza kuwa vigumu zaidi kuliko kusoma vitabu visivyo na matukio halisi (Fiction). Hii huweza kuwafadhaisha wasomaji wa vitabu vya taaluma yoyote ile ikiwemo sayansi, siasa na fasihi, ufafanuzi na vile vya kusaidia kujitambua.

Hii ndiyo sababu watetezi wa vitabu vyenye matukio halisi (Visivyo na fantasia) akiwemo tajiri mkubwa duniani, Bill Gates wametoa njia mbalimbali ambazo pia zimeandikwa kwenye makala hii za kuweza kukusaidia kukumbuka kile unachokisoma kwenye kitabu. Bill Gates husoma vitabu takribani 50 kila mwaka na alitumia njia hizi kuweza kukumbuka yote aliyoyasoma kwenye vitabu hivyo 50;

Tambua kile kinachokuvutia
Mvuto au shauku huwa ndio motisha ya kwanza kwa mtu kuchagua kitabu fulani. Tatizo la kutokukumbuka maudhuhi ya kitabu au makala ambayo haijakidhi shauku yako huja baadaye; Kutokuwa na shauku na kitabu fulani huweza kukuzuia usimalize kukisoma kitabu hicho.

Watu wanatakiwa kutambua kinachowavutia kutoka kwenye maoni mengi ya jamii.

Cha kujifunza ni kwamba kuacha kusoma kitabu fulani ni sawa kabisa bila kujali kitabu hicho ni muhimu kiasi gani. Na inapokuja kwenye vitabu ya kujifunza na vile vya maisha halisia, dhana zake hujengwa na kile ambacho tayari tunakifahamu. Msukumo wa kuiondoa shauku hii ndiyo hupelekea mtu kusoma kitabu.

Tafiti moja ilibaini kwamba wanafunzi ambao walikuwa ni wasomaji wa kawaida ila walikuwa na mapenzi ya dhati na mambo ya mpira wa miguu walionesha uwezo na ujuzi mkubwa sana kwenye maudhuhi zilizohusu mpira wa miguu kuliko wale ambao walikuwa wasomaji wakubwa lakini hawakuwa wapenzi wa mpira wa miguu.

 

“Unapojifunza kitu fulani kipya, unaleta taarifa zote ambazo tayari unazijua zinazohusiana na taarifa hiyo mpya kwenye ufahamu wako. Na kwa kufanya hivyo unaijumuisha taarifa hiyo mpya kwenye ufahamu ambao tayari unao”. -Alison Peston, Mtaalamu wa Saikolojia na Sayansi ya Ubongo

Hivyo basi unaweza kuachana na kile ambacho unajikongoja nacho kukifanya na badala yake chagua kile ambacho kinakuvutia bila kujali kipo kwenye uwanja upi wa kitaaluma.

 

Nakili kile unachojifunza
Katika utafiti wa makala hii, ilihusisha utazamaji wa video nyingi zilizopo Youtube zinazomuhusu Bill Gates au Warren Buffet wakati wakizungumza kuhusu jinsi wanavyokabiliana na kitabu kigumu hasa vile visivyo vya kifantasia.

Kitu kimoja chenye mfanano kutoka kwenye video hizi ni kuwa wakati wote walivaa nguo ambazo hazikuwa na majina ya wazalishaji wa nguo hizo. Pia iligundulika kwamba wote walikuwa wakinakili vitu kadhaa katika shajala zao.

Kunakili baadhi ya taarifa ni hitaji muhimu sana, sio tu kwa ajili ya ubunifu ila hata katika kujifunza. Shajala za Oliver Sack zilikuwa zimeshajaa taarifa mbalimbali zilizokuwa zimeandikwa kwa kalamu za wino wa rangi tofauti tofauti.

Hivyo kunakili baadhi ya taarifa, kuzungushia maduara, kuchora au kupigia mstari katika ukurasa wa kitabu huweza kusababisha uelewa mkubwa na utunzaji wa taarifa iliyopatikana katika ukurasa huo.

Tafiti zinaeleza, wanafunzi wenye tabia ya kupanga kazi zao vizuri na kunakili baadhi ya vitu wanapokuwa wanasoma huwa na uwezo mkubwa wa kukumbuka kile walichojifunza na matokeo yake hupata maksi za juu katika mitihani yao. Hii ni kwasababu kuelewa ujumbe fulani ni jambo la muhimu sana katika kutambua kiini cha ujumbe huo.

Kunakili taarifa sio tuu kuandika herufi fulani; bali ni kuichambua taarifa hiyo na kuiweka kwenye fahamu zetu. Hata hivyo huwezi kunakili kila kitu, ni vyema kutambua vilivyo muhimu kwako ndivyo uvinakili.

Utafiti unaendelea kueleza kuwa wanafunzi ambao wanapangilia kazi zao vizuri na kunakili au kuandika kile wanajifunza wana uwezekano mkubwa wa kukumbuka walichosoma na kupata alama za juu kwenye mitihani yao. Hii ni kwasababu kunakili sio jambo la mazoea lakini ni mfumo mzuri wa uchakataji wa taarifa ambayo mwanafunzi anaisikia na kuitunza kwenye ubongo.

Hata hivyo, sio rahisi kuandika kila kitu lakini mwanafunzi anaweza kuamua kuandika mambo muhimu yatakayomsaidia.

 

Kufikiri na kuunganisha
Tofauti na pointi ya kwanza, waandishi wengi wanaamini kuwa mtu anatakiwa kusoma vitabu asivyovipenda. Wanaamini kuwa kung’ang’ana na jambo unalolichukia inaweza kukusaidia kupata mtazamo mpya au tofauti na ule uliouzoea. Au kusoma kitu usichokipenda kunaweza kuongeza thamani ya mawazo au mtazamo wako ulionao.

Mwisho wa siku, waandishi na wanasaikolojia wanashauri wasomaji kutumia muda mwingi kufikiri zaidi ili kuongeza uelewa wa kile wanachosoma.

Wasomaji wanapaswa kujielekeza kwenye kitabu, na kuyaona matukio kwa mtazamo binafsi na kutambua namna nzuri ya kuhusianisha au kuunganisha na mapendeleo yao.

Mathalani, watunzi wa hadithi wamefanikiwa kuwafikia watu wengi kwasababu wakati wa kutunga hadithi zao, wanatengeneza lugha ya picha ambayo wanaiunganisha na ufahamu wa wasomaji. Ndiyo maana vitabu vingi vya hadithi za kutunga vinavutia kusoma kwasababu inayotumika zaidi ni lugha ya picha ambayo inatafsiriwa katika mazingira halisi ya maisha ya watu.

Picha za hadithi au filamu za maigizo zinatunzwa kwenye kumbukumbu ya muda mfupi na kadri inavyozidi kupata nafasi kwenye ubongo huamishiwa kwenye kumbukumbu ya muda mrefu. Na kama haitanakiliwa vizuri hupotea kwa muda mfupi.

Mchakato wa kuhamisha kumbukumbu unaweza tu kufanikiwa ikiwa mtu atakuwa anapitia au anafanya mara kwa mara yale aliyoyaona au kusoma. Baada ya hapo milango ya fahamu huimarisha picha za matukio na kuzifanya kuwa sehemu ya maisha na haziwezi kufutika kirahisi.

 

Kusimulia na kueleza
Njia nyingine ya kukifanyia kazi kile ulichojifunza ni kumsimulia au kumuelezea mtu mwingine. Kadri wasomi wanavyoongea kwenye umati wa watu, ndivyo wanaongeza maarifa. Ubora na kipimo cha utii wa mtu hupimwa zaidi kwa uelewa na dhana mbalimbali za maisha na jinsi anavyozielezea.

Njia nyingine ya kukumbuka ulichosoma ni ulinganifu wa matukio uliyoyasoma na kuyapa picha tofauti lakini inayotolea maelezo sawia na kumbukumbu ya maandiko uliyosoma.

 

Hali, uchovu na kuhama kifikra
Licha ya matamanio tuliyonayo ya vitabu, wakati mwingine kusoma kunaweza kusivutie ikiwa msomaji hayuko katika hali nzuri. Hali zetu zinaweza kuathiriwa na uchovu. Tumejifunza kuwa kusoma kwa hisia kunaimarisha kumbukumbu, lakini uchovu na mabadiliko ya kihisia katika miili yetu vinaweza kuathiri mchakato wa usomaji wetu.

Hisia na umakini ni kama peda za baiskeli na uchovu unaweza kuvuruga hisia za mtu na kuvuruga hisia za wengine pia. Ukosefu wa usingizi na msongo wa mawazo ni vichocheo vikubwa vya uchovu wa akili na mwili. Ndio maana wanasayansi wanashauri soma ukiwa katika hali nzuri ya kupumzika.

Zaidi, hali ya kihisia inaweza kuathiriwa na mazingira yanayokuzunguka, na hili ni suala binafsi- Mfano Willium anaweza kusoma na kuandika sehemu yenye kelele na fujo lakini Derek hawezi mpaka atafute eneo lenye utulivu.

Mwisho, muingiliano wa kifikra ndio tishio kubwa la usomaji leo. Hata kama jambo lenyewe ni la mtu binafsi lakini mtu anaweza kupoteza hisia za kusoma na kupoteza malengo yake. Hata hivyo, kukubaliano na muingiliano wa mawazo wakati wa kusoma ni kama kucheza kamali. Uwezekano wa kutokuelewa kile ulichosoma ni mkubwa sana.

Kusoma kunahitaji utulivu wa mawazo na umakini wa mtu kufuatilia maandishi na kuyapeleka moja kwa moja katika kumbukumbu za ubongo. Kama mtu atakuwa na mawazo mengi wakati wa kusoma hawezi kufikia lengo lake la kupata maarifa yaliyokusudiwa.

Pia matumizi ya simu za kisasa, kwa kiasi kikubwa yanaathiri usomaji wa mtu hasa kama simu inatumika kupata maarifa. Kimsingi simu zina mambo mengi ni rahisi msomaji kuacha kusoma ili asome ujumbe au apokee simu iliyoingia na hata kupitia mindao ya kijamii.

Inashauriwa kama unatumia simu kusoma ni vema ukapakuwa programu maalum ambazo zinakusaidia kusoma vitabu hata kama haujaunganishwa na intaneti.

Kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya njia ipi ni sahihi ya kusoma; kutumia simu au vitabu vya karatasi za kawaida. Kila mmoja ana sababu zake ambazo zinawaweza kukubaliwa kulingana na mazingira, teknolojia na upendeleo wa mtu juu ya njia rahisi ya kupata maarifa.

Hata hivyo, jambo la muhimu ni kwamba mtu anapaswa kusoma, kusoma chochote chenye manufaa, kwasababu ndio njia pekee ya kuongeza maarifa na wigo wa kuelewa mambo yanaendelea duniani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *