MATUMAINI ya wakazi wa Dar es Salaam, Lindi na Mtwara kuanza kutumia gesi asilia majumbani mwao Julai, mwaka huu, hayapo tena.
Kukosekana kwa matumaini hayo kunatokana na kushindwa kukamilika kwa baadhi ya taratibu kuhakikisha zoezi hilo linaanza.
Aprili 5, mwaka huu, mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani aliwaeleza Watanzania kupitia Bunge kuwa uhakika wa wananchi wa mikoa hiyo kuanza kupata huduma hiyo upo.
Aliahidi kuwa Julai, mwaka huu, wananchi watapata neema ya gesi asilia majumbani mwao, tayari kwa matumizi ya kupikia.
Gari linalotumia mfumo wa gesi.
Hata hivyo, FikraPevu limejiridhisha kuwa ahadi hiyo haiwezi kutekelezwa kwa muda uliopangwa, kwa kuwa jitihada za kutekeleza hilo hazionekani kwenda kasi.
Katika kuthibitisha hilo, FikraPevu iliamua kuutafuta ukweli wa kauli hiyo ya serikali na kufanikiwa kuzungumza na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Injinia Kapuulya Musomba.
Injinia Musomba amesema bado kuna kazi ngumu na itakayochukua muda kufikia hatua ya kuwawekea gesi wananchi. Hakusema ni muda gani.
Amesema dizaini ya kiinjinia kwa mradi wa kusambaza gesi asilia majumbani katika mkoa wa Lindi na Mtwara bado haijafanyika.
“Mradi huu bado upo kwenye hatua ya upembuzi yakinifu. Upembuzi yakinifu ukikamilika ndipo hatua ya dizaini ya kiinjinia itafuata,” Musomba ameiambia FikraPevu.
Kuhusu gharama za kuingiza gesi hiyo majumbani mwa wananchi, wengi wakiwa masikini wa mikoa ya Lindi na Mtwara, Musomba anasema, “zitabebwa na serikali.”
Amesema gharama za awali katika mradi huu zinabebwa na Serikali kupitia TPDC, hata hivyo baada ya kuhakikiwa na wathaminishaji, mtumiaji wa mwisho hulipia gharama zote zilizogharamiwa katika mradi huo.
FikraPevu imeelezwa kuwa gesi asilia inayoelezwa kuingizwa majumbani, itachakatwa eneo la Madimba, Mtwara na kusafirishwa Lindi na Dar es Salaam, wakati eneo la kuchakata gesi la Mnazi Bay, litawahusu wananchi wa Mtwara na Lindi pekee.
Magari ya kutumia gesi
TPDC imezungumzia kuwepo kwa magari yanayotumia gesi, na hapa ni swali aliloulizwa Injinia Musomba na FikraPevu.
Swali: Inasemekana kuwepo magari 50 yanayotumia gesi nchini badala ya mafuta yako wapi? Je, yanaendelea vyema?
TPDC: Hadi sasa kuna jumla ya magari 60 ambayo yameongezewa mfumo wa kutumia gesi asilia. Magari hayo ni ya watu binafsi ambao ni wakazi wa Dar es Salaam.
Mradi huu ulipungua kasi tangu miaka ya 2008 baada ya gesi kutopatikana kutosha. Hata hivyo kwa sasa gesi ya kutosha itaanza kupatikana baada ya bomba kubwa la kusafirishia gesi kukamilia tangu 2015.
Swali: Je, TPDC ina magari mangapi ya mfano?
TPDC: Hivi sasa sisi tuna magari mawili ambayo yanatumia gesi asilia, magari hayo bado yanafanya kazi mpaka sasa.
Inachokijua FikraPevu
Gazeti hili tando lina uhakika kuwa mradi huo wa kuingiza gesi asilia majumbani kwa mikoa hiyo huenda ukaanza baada ya mwaka mmoja, ikiwa jitihada zitaongezwa.
Kuhusu magari yanayotumia gesi, FikraPevu inazo taarifa kuwa ni gari moja tu walilonalo TPDC lenye mfumo wa kutumia gesi, lakini nalo liko “juu ya mawe.”
Magari yanayoelezwa na TPDC kuwa yako 60 yakifanya kazi, FikraPevu inaweza kueleza pasipo shaka, kuwa magari yanayofanya kazi hayazidi matatu, na yoteyako Dar es Salaam.
Pendekezo: Ikiwa bado TPDC ina nia ya kuendelea kuona yapo magari yanayotumia gesi, inabidi ishiriki kuagiza magari yanayotumia mfumo huo, badala inavyofanyika sasa; kubadili magari yenye mfumo wa mafuta.
Gharama ya kubadili magari hayo ni kubwa mno, kwani wamiliki hutumia zaidi ya sh. milioni 3. Unapoagiza gari lenye mfumo wa gesi, hakuhitajiki tena ufundi wowote zaidi ya kuweka gesi na gari kuanza mwendo.