Ongezeko la gharama za uendeshaji wa benki na masharti mapya ya kodi yaliyowekwa na serikali kwa taasisi za fedha yametajwa kuathiri mwenendo wa utoaji mikopo kwa wafanyabiashara nchini.
Ongezeko la gharama za kuendesha benki linachangiwa na kupungua mzungo wa fedha ambao ni matokeo ya kupungua kwa amana za serikali zilikuwa zinawekwa katika benki hizo. Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani iliamuru taasisi zake kuhamishia akaunti zao Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa madai ya kuthibiti matumizi ya fedha za umma.
Mabadiliko hayo katika sekta ya fedha yaliathiri mwenendo wa ukopeshaji katika benki mbalimbali ambapo benki zimeongeza riba ili kufidia gharama za kuendesha shughuli zao.
Ripoti ya mapitio ya uchumi ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ya mwezi Oktoba mwaka huu, inaeleza kuwa katika nusu ya pili ya mwaka 2017 riba inayotozwa kwenye mikopo ya benki imeongezeka ikilinganishwa na mwaka uliopita wa 2016.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa riba iliyotozwa kwenye mikopo kwa mwezi Septemba 2017 imeongezeka hadi kufikia asilimia 18.46 kutoka asilimia 17.46 mwezi Agosti ikilinganishwa 15.83% ya mwezi kama huo mwaka 2016.
Ongezeko la riba limetajwa kupunguza idadi ya wateja wanaokopa na kuathiri sekta za kilimo, ujenzi, mawasiliano na usafiri ambazo zinategemea mikopo kutoka benki kuendesha shughuli zao. Ili kukabiliana na hali hiyo benki zimepunguza riba kwenye amana zinazowekwa katika benki zao ili kuvutia wateja wengi zaidi kuwekeza fedha katika taasisi hizo.
Ripoti hiyo ya BOT inaonyesha kuwa mwezi Septemba 2017, riba iliyokuwa inatozwa kwa amana za benki ilipungua zaidi kuliko mwezi uliotanguliwa wa Agosti, na riba hiyo ni kubwa ikilinganishwa na mwezi kama huo 2016. Kutokana na hali ya kiuchumi uwezekano wa riba hiyo kupungua ni mkubwa kwa siku zijazo.
Hata hivyo, Benki Kuu ambayo ndio mlezi wa benki zote nchini imeendelea kusimamia sera ya fedha na kuhakikisha mikopo haithiri mwenendo wa uchumi ikiwemo ukuaji wa Pato la Taifa (GDP). Pia imeendelea kuzishauri benki kupunguza zaidi riba na kujikita katika sekta ya uwekezaji ili kuokoa fedha zinazoelekezwa kwenye mikopo.
Majengo pacha ya Benki Kuu ya Tanzania
Mapema mwaka huu, Gavana wa BOT aliyemaliza muda wake, Benno Ndulu wakati akiongea na Wakurugenzi wa benki za biashara alizishauri taasisi za fedha kuwa makini na kutoa mikopo kwa wateja wenye rekodi nzuri za mapato ili kujiepusha na madeni yasiyolipika.
Benki ya Dunia (WB) kupitia uwakilishi wake Tanzania, mwezi Novemba mwaka huu katika mkutano wa kujadili Ukuaji wa Uchumi wa Afrika imeishauri serikali ya Tanzania kuimarisha sekta ya fedha hasa taasisi ndogo zinazotoa mikopo ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kupata mikopo yenye masharti nafuu kuendesha biashara zao.
Licha ya Tanzania kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia biashara na uwekezaji lakini shughuli hizo zinatatizwa na ongezeko la kodi ya serikali na kupungua kwa kiwango cha ukopeshaji kinachotelewa kwa sekta binafsi. Hatua hiyo inatajwa kushusha uzalishaji na mwenendo wa soko la bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani.
Ili kuhakikisha uchumi unakuwa kwa kiwango kizuri, serikali imeshauriwa kulegeza baadhi ya masharti ya kodi na kuruhusu mzunguko wa fedha kupitia benki za biashara ili kuziwesha benki kumudu gharama za uendeshaji na riba zinazotozwa kwenye mikopo.
Viwango vya Riba Afrika
Kulingana na Shirika la CGAP linalojihusisha na kuboresha maisha ya watu maskini kupitia uwezeshaji wa kifedha linaeleza kuwa gharama za uendeshaji wa benki katika nchi za Afrika zimepungua kutoka asilimia 28 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 19 mwaka 2011.
Licha ya kupungua kwa gharama hizo, Afrika ni bara lenye viwango vikubwa vya uendeshaji wa taasisi za fedha ikilinganishwa na maeneo mengine duniani. Kuna haja ya kutathmini vichocheo vya gharama za uendeshaji benki Afrika na kutafuta suluhu ya kudumu ya kuimarisha utendaji na ustawi wa taasisi za fedha.