Haki ya kujieleza ilivyopindishwa katika mchakato wa Katiba Mpya

Jamii Africa

Uhuru wa mtu kutoa maoni kwa jambo analoliamini ni haki ya kila mtu isipokuwa tu pale haki hiyo inapoonekana kuvunja haki nyingine za msingi za watu. Uhuru wa kutoa maoni au kujieleza ni haki inayotambulika kimataifa na inampa mtu uwanja mpana kuwasiliana na kusikika ili kuwa na jamii iliyostaarabika.

Kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kutoa maoni na kujieleza, jamii nyingi zimezuia mawazo mbadala ambayo yangeweza kutumiwa katika kuleta maendeleo. Wakati mwingine watu wanaweza kuwa na kiu ya kujieleza lakini mfumo wa kiutawala unaweza kuwa kikwazo kwa watu kutoa maoni yao.

Jitihada mbalimbali zimekuwa zikiratibiwa ili kupigania haki ya kutoa maoni na kuiwezesha dunia kuwa sehemu huru ambayo kila mtu mwenye jambo la kuwashirikisha wengine aweze kuongea. Mfano kampeni hizo ni ‘Vunja ukimya zungumza na mwenzio’, ‘sikai kimya’, ‘sema usikike’, ni miongoni mwa hatua muhimu zilizochukuliwa kuwajengea watanzania uwezo wa kuongea kile wanachokiamini.

Hapa nchini Tanzania uhuru wa kujieleza unalindwa na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara ya 18. Pia mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imesaini inalinda uhuru wa kujieleza, mikataba hiyo inajumuisha:

Tamko La Ulimwengu La Haki Za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights 1948) pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Haki za Watu. Ibara ya 19 inatoa haki na uhuru wa kila mtu kuwa na maoni yake na kujieleza na bila mawasiliano yake kuingiliwa. Tamko la Haki za Binadamu na za Jamii Afrika (The African Charter on Human and People’s Rights (1981)) na Mkataba wa Kanuni za Uhuru wa Kujieleza Afrika (Declaration of Principles on Freedom of Expression in Africa).

Kushindwa au kuzuia kujieleza imekuwa changamoto ya muda mrefu kwa wananchi walio wengi, kazi ya kutoa maoni wameachiwa watu wachache ambao ndio hufanya maamuzi kwa niaba ya watu wengine. Hali hii huzuia matakwa ya walio wengi kutekelezwa.

Mfano mzuri ni suala la upatikanaji wa katiba mpya ambao ulikwama kwasababu watu wachache walizuia sauti za walio wengi (wananchi wa kawaida/maskini) kusikika kwenye katiba mpya ambayo ilionekana kuwa mkombozi.

Hata mchakato wa kutoa ulipokuwa ukiendeshwa na Tume ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba waliojitokeza kutoa maoni yao walikuwa wachache na idadi hiyo haikuvuka nusu ya watu waliopaswa kuongea.

Uchunguzi wa shirika la Twaweza (2017) juu ya Sauti za Wananchi na upatikanaji wa Katiba mpya unathibitisha kuwa mwananchi mmoja kati ya 8 ambayo ni sawa na asilimia 18 alishiriki kwa namna fulani katika mchakato wa kukusanya maoni wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Yafaa ifahamike kuwa Novemba mwaka 2013, 36% wananchi walieleza kuwa waliwasilisha maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia mikutano, barua, mitandao au ujumbe wa simu” inaeleza ripoti hiyo.

Tafsiri yake ni kuwa wananchi 6 kati ya 10 (64%) hawakutoa maoni yao juu ya upatikanaji wa katiba mpya. Huenda mapendekezo yaliyotolewa yangekuwa bora zaidi kama idadi hiyo ingevuka nusu ya wananchi.

Haki ya kujieleza inaenda sambamba na haki ya kukusanyika (kukutana), lakini katika kipindi cha kukusanya maoni ya katiba mpya bado idadi ya watu waliojitokeza kwenye mikutano ilikuwa ni ndogo.

Ripoti ya uchunguzi ya Twaweza inabainisha kuwa, Mwananchi mmoja kati ya nne (12%) anasema alihudhuria mkutano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini waliohudhuria sio wote walijieleza au kutoa maoni, na idadi ndogo wanasema walihojiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba (6%) au waliwasilisha maoni yao kwa njia ya maandishi (4%), kupitia ujumbe wa simu (3%) au kwa barua pepe ama mitandao ya kijamii (1%).

Uhuru wa kutoa maoni unatofautiana baina ya wanaume na wanawake. Wanaume wanaonekana zaidi kuwa na ujasiri wa kujieleza ikilinganishwa na wanawake katika majukwaa ya kutoa maoni hawajitokezi kwa wingi. Sababu kuu ni mfumo wa uongozi wa jamii tunazoishi na mila na desturi ambazo hazimpi nafasi mwanamke kupaza sauti yake akasikika ikidhaniwa wa kuwa anahatarisha maslahi ya wanaume.

Uchunguzi huo unaeleza kuwa “Wanaume wameonyesha viwango vikubwa vya ushiriki kwenye mchakato wa kutoa maoni wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (25%) kuliko wanawake (10%)”.

Lakini ukitazama asilimia ya wanawake na wanaume katika kutoa maoni iko chini na hazitoi tafsiri pana kuwa uhuru wa kutoa maoni umepata mpenyo katika jamii zetu kama inavyotakiwa. Kutokana na maendeleo ya teknolojia na ukuaji wa sekta ya mawasiliano inetegemewa vijana wawe vinara wa kujieleza lakini hali ni tofaut.

Vijana bado hawatumii fursa hiyo kujieleza na kuongea kile wanachokiamini kwa ajili ya mstakabali wa maisha yao. Bado watu wazima wana sauti katika jamii na maslahi yao ndio yanazingatiwa na vijana wanabaki kunung’unika bila kuchukua hatua stahiki za kuongelea masuala yao yakapatiwa ufumbuzi.

“Wenye umri zaidi ya miaka 50 (24%) walikuwa na uwezekano zaidi wa kushiriki kuliko wenye umri chini ya miaka 30 (13%). Tofauti katika viwango vya ushiriki kati ya makundi yenye uwezo mbalimbali ni mdogo, sawa na wananchi weney viwango tofauti vya elimu na wale wanaoishi maeneo ya mijini na vijijini.

Ili taifa liendelee linahitaji watu wenye uwezo wa kuzungumza na kuwa huru kuelezea mustakabali wa maisha yao. Ni muhimu kwa viongozi wa jamii kufungua milango na kuweka mazingira rafiki kwa watu kukutana katika mijadala mbalimbali na kutoa maoni yao.

Kila mtu anawajibu wa kudai haki ya kujieleza ambayo imetajwa katika katiba na matamko ya kimataifa. Tukijenga utamaduni wa kusema yale tunayoamini tutaifanya jamii yetu kuwa jukwaa muhimu la kufikia maendeleo endelevu.

 

 

 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *