Ni jambo la kushangaza tena la kustaajabisha! Ni kule mashariki ya mbali, rasi ya Korea. Nchi zenye uhasama mkubwa kisiasa ziliamua kuweka tofauti zao pembeni na kuingia kwenye meza mazungumzo.

Ni historia ya kipekee duniani, Kwa viongozi wa nchi za Korea Kaskazini na Korea Kusini kushikana mikono na kufurahi pamoja. Nchi hizi mbili zina umuhimu mkubwa katika kulinda amani ya dunia.

Ziliyagawa mataifa makubwa ikiwemo China, Marekani, Urusi, Ufaransa katika makundi ya kisiasa na kiuchumi na kujenga uhasama mkubwa juu ya matumizi ya silaha za nyuklia.

Tukio hilo la Kihistoria lilitokea jana baada ya  Viongozi wa Korea Kaskazini na Korea Kusini kufanya mkutano wa kilele katika eneo la mpakani lisilo na shughuli za kijeshi, huku wakiahidi kutafuta amani baada ya miongo mingi ya uhasama.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in walipeana mikono na kuonyesha tabasamu katika eneo la mstari wa kijeshi ambao unazitenganisha nchi zao na kupeleka ujumbe mkubwa duniani.

 

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un (kushoto) akiwa ameshikana mkono na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in baada ya kukutana katika mpaka wa nchi hizo mbili.

Kim alimwambia Moon huku akitabasamu kuwa ana furaha kukutana naye, kabla ya mgeni huyo kuvuka upande wa Korea Kusini, na hivyo kuwa kiongozi wa kwanza wa Korea Kaskazini kukanyaga ardhi ya Kusini tangu kumazilika vita vya Korea miaka 65 iliyopita.

Viongozi hao wawili walivuka na kuingia upande wa Kaskazini huku wakiwa wameshikana mikono kabla ya kuingia katika Jumba la Amani  upande wa Kusini wa kijiji cha Panmunjom kwa ajili ya mkutano wao wa kilele. Mkutano huo wa tatu wa aina yake tangu uhasama ulipositishwa mwaka wa 1953.

Kim ambaye utawala wake unatuhumiwa kwa ukiukaji wa haki za binaadamu, alimwambia Moon kuwa mkutano huo ni mwanzo wa historia mpya. “Ninataka kusema kuwa tunapaswa kujitahidi ili tukiangalia nyuma katika miaka 10 iliyopita na kusema kuwa haikupotea tu. Natumai kuwa tunaweza kukutana mara kwa mara ili kutatua matatizo baina ya nchi zetu”.

Naye rais wa Korea Kusini, Moon aliitaja hatua ya Kim kuvuka mstari wa kijeshi kuwa ya ujasiri na ishara ya Amani. Alimuahidi kushirikiana pamoja ili kudumisha mahusiano ya kidiplomasia.

“Natumai kuwa tunaweza kuwa na mazungumzo yenye matokeo makubwa na kufikia makubaliano, ili tuwape zawadi kubwa raia wetu na kila mmoja kote duniani, wanaotaraji kupata Amani,” alisema Moon.

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la DW, linaeleza kuwa, Kim aliandamana na dada yake na mshuauri wa karibu Kim Yo Jong na kiongozi wa Kaskazini wa mahusiano ya Korea mbili, wakati Moon akiandamana na mkuu wa ujasusi na mkuu wa jeshi.

Mkutano huo wa kihistoria ulifanyika wiki chache tu kabla ya Kim kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump ili kujadili suala la kuondoa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea.

Duru za siasa zinasema Kim na Moon walijadili kuhusu mpango wa kuondoa silaha za nyuklia na kupatikana amani ya kudumu katika rasi ya Korea na kusaini tamko la pamoja.

Siku chache kabla ya mkutano huo, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis alitoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya uwazi baina ya mataifa mawili ya Korea ili kuionyesha dunia kuwa inawezekana kudumisha amani duniani.

Hata hivyo, Marekani mshirika mkubwa wa Korea Kusini inaamini kuwa mkutano wa viongozi hao ni mwanzo mzuri  katika kupatikana Amani na ustawi duniani. Ikulu ya White House imesema inaendelea kufanya  mazungumzo na Korea Kusini katika matayarisho ya mkutano unaopangwa wa Rais Donald Trump na Kim katika wiki chache zijazo.

 

Vita ya Korea

Vita ya Korea ya  ilitokea kati ya 1950 hadi 1953. Ilianzishwa na Korea Kaskazini iliyovamia Korea ya Kusini. Korea ya Kaskazini ilisaidiwa na Jamhuri ya Watu wa China na Umoja wa Kisovyeti (Urusi).  Korea ya Kusini ilisaidiwa na Marekani. Lakini Marekani ilishiriki katika vita hii kwa jina la Umoja wa Mataifa pamoja na wanajeshi wa nchi 16.

Katika miaka mitatu ya vita mapigano ya maadui yalifika karibu kila sehemu ya rasi ya Korea na mateso ya wanachi raia pia ya wanajeshi kwenye pande zote yalikuwa mabaya. Inakadiriwa karibu watu milioni 4 na wanajeshi milioni 1 waliuawa.

                        Ramani ya Korea Kaskazini (juu) na Korea Kusini (chini)

Julai 1950, Baraza la Umoja wa Mataifa iliamua kuingilia kijeshi dhidi ya uvamizi kutoka Korea Kaskazini. Azimio hili lilipita kwa sababu Umoja wa Kisovyeti hukuhudhuria kikao hivyo ulishindwa kupiga kura ya veto. Jeshi lililoingia kwa niaba ya Umoja wa Mataifa liliunganisha vikosi kutoka nchi 22, jumla askari 500,000 na wengi wao kutoka Marekani.

Katika awamu ya pili jeshi la Umoja wa Mataifa lilifika Pusan kuanzia Agosti 1950. Ndege za Marekani zilishambulia barabara, madaraja na jeshi la kaskazini kote kwenye rasi. Korea ya Kaskazini ilikosa ndege za kijeshi.

Jeshi la Marekani na Korea Kusini lilelekea kaskazini kwa mbio na kuteka Seoul tena na kuwarudisha Wakorea wa Kaskazini pia kuteka mji mkuu wa kaskazini Pyonyang  hadi kukaribia mpaka wa Korea na China kuanzia mwisho wa mwezi wa kumi 1950.

Katika awamu ya tatu kuanzia Novemba 1950 jeshi la China likaingia kati na kuwasukuma Wamarekani kusini tena na kuteka Seoul mara ya pili Januari 1951. Ndege za kijeshi za Umoja wa Kisovyeti  zilisaidia zikilinda anga nyuma ya mstari wa mapigano lakini bila kuwashambulia Wamarekani juu ya eneo lao.

Wakati wa Januari Wachina waliweza kusogea mbele ndani ya Korea ya Kusini lakini walikwama kwa sababu walishindwa kupata mahitaji yao kutokana na nguvu ya Marekani angani.

Katika awamu ya mwisho hadi Julai 1951 mashambulio ya Kaskazini na Kusini yalibadilishana na Wachina walirudishwa nyuma hadi uliowahi kuwa mpaka kabla ya vita. Marekani iliamua kutosogea mbele zaidi ikitafuta majadiliano ya kusimamisha vita.

Majadiliano haya yalianza 10 Julai 1951 yakaendelea hadi 1953. Muda wote huo vita iliendelea kwa njia ya mashambulizi kila upande lakini kwa shabaha ya kushika maeneo yaliyokuwa yakimilikiwa na kila upande kabla ya vita.

Julai 27, 1953 mapatano ya kusimamisha vita yalifikiwa. Eneo lenye upana wa kilomita nne pande zote mbili lilitangazwa kuwa “Ukanda usio na jeshi”.

Hadi leo ni mpaka kati ya nchi zote mbili za Korea na kulindwa na wanajeshi wengi sana.

By Jamii Africa

JamiiForums' Editorial Website | Tanzania's Online News Portal | Dedicated for Public Interest Journalism

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *