Hizi ndizo changamoto za Sekta ya Afya nchini Tanzania tangu Uhuru!

Dr. Joachim Mabula

AFYA bora ni rasilimali muhimu na kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii. Serikali huwa na lengo la kuinua hali ya afya kwa wananchi wote mahali popote walipo ikiwa ni mijini au vijijlni kwa kupunguza maradhi na vifo kwa wananchi na kuongeza umri wa maisha yao kwa kuwa na afya thabiti kimwili, kiakili na kijamii.

Ili kufanikisha lengo hilo serikali kupitia Wizara ya Afya hutengeneza sera nzuri za kufikia lengo hilo.


Kabla ya Tanzania (wakati huo Tanganyika) kupata uhuru mwaka 1961, huduma za afya zilikuwa mijini na zilijikita katika huduma za tiba na huduma za upasuaji zilikuwa adimu sana. Serikali ya kikoloni haikutilia mkazo kupeleka huduma za afya vijijini.

Baada ya kupata uhuru ilionekana kuwa mipango ya huduma za afya lazima ifanyike kwa kuoanisha na mipango mingine ya maendeleo na katika kufanikisha azma yake serikali ilipitisha Mpango wa Kwanza wa Miaka Mitano wa Maendeleo (1964-1969) uliokuwa na malengo makuu matatu; kuongeza pato la kila mwananchi, kujitosheleza kwa mahitaji ya watumishi wa afya na kuongeza maisha kutoka miaka 55/40 mpaka 50.


Ndani ya mpango huo lengo lilikuwa kila mkoa kuwa na hospitali ya mkoa yenye kutoa huduma za tiba na upasuaji.

Kabla ya lengo hili, serikali ilikuwa imependekeza kuwepo na hospitali za wilaya kwa kila wilaya zenye uwezo wa vitanda 200, ila haikuwezekana na ndipo likaja lengo la hospitali ya mkoa kwa kila mkoa.

Katika kuboresha huduma za afya maeneo ya vijijini, serikali ilitarajia kujenga vituo vya afya 500 kwa mgawanyo sawa, kituo cha afya kimoja kwa kila watu 50,000 kikiwa na jukumu la kusimamia zahanati 5 zinazo kizunguka kituo hicho.

Kila kituo cha afya kilipaswa kuwa na vitanda nane kwa matatizo ya mama wajawazito na vitanda sita kwa ajili ya magonjwa ya kawaida ambayo yatahitaji matibabu ya muda mfupi au rufaa kwenda kwenye hospitali ya wilaya.

Ili kupata rasilimali watu watakaofanya kazi kwenye vituo hivyo vya kutolea huduma za afya, serikali iliongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa katika mafunzo ya afya na kuongeza idadi ya vyuo vya mafunzo hayo katika ngazi zote.

Mkazo uliwekwa katika kuimarisha usafi wa mazingira na lishe hasa kwa watoto ili kuzuia magonjwa ya mlipuko na yanayotokana na uchafu kiujumla.

Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo (1969-1974) ulipitishwa baada ya Azimio la Arusha mwaka 1967 ambalo lilitilia mkazo siasa ya kujitegemea na usambazaji wa usawa na haki wa huduma mbali mbali za jamii na rasilimali zilizopo nchini. Nguvu kubwa zilielekezwa kwenye huduma za afya za kinga ili kuzuia maradhi yanayoambukiza. Kimsingi mpango huu wa pili ulikuwa na lengo la kuendeleza juhudi za mpango wa kwanza. Katika mpango huu serikali ilitarajia kujenga vituo vya afya vipya 80.

Lengo la kuwa na kituo cha afya kimoja kwa watu 50,000 na zahanati moja kwa watu 10,000 lingefikiwa kabla ya mwaka 1985 endapo serikali ingejenga walau zahanati 100 katika kila mpango wa miaka mitano. Mafunzo ya kuwapata watumishi wa kutosha yalienda sambamba na upanuzi wa huduma za afya.

Mpango huu wa pili ulikuwa na mafanikio mazuri zaidi kwa sababu serikali ilikuwa imejifunza kutokana na uzoefu wa mpango wa kwanza.
Malengo ya Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano wa Maendeleo (1976-1981) yalikuwa kutoa huduma ya maji, afya mijini na vijijini na pia kukamilisha mpango wa elimu ya UPE.

Azimio la Alma Ata la mwaka 1978 lilizitaka nchi zote duniani kuwa na huduma za afya za msingi kwa wanachi wake hadi kufikia mwaka 2000, liliongeza kasi ya utekelezaji wa utoaji wa huduma za msingi.

Katika mpango huo wa tatu serikali ilitoa kipaumbele pia katika usafi wa mazingira na lishe kwa magonjwa mengi yaliua idadi kubwa ya watu yalitokana na usafi wa mazingira na chakula.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliandaa kampeni kama vile "Chakula ni Uhai” na "Mtu ni Afya"; ujenzi wa vituo vya afya na zahanati vijijini; kupanua na kuimarisha huduma za kinga; utoaji wa elimu ya watu wazima na usambazaji wa vitabu vya kutosha kuhusu masuala ya afya na utoaji wa elimu ya msingi kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule. Huu ulikuwa ndio mwanzo wa ushirikiano wa sekta nyingine zinazohusika na utekelezaji wa afya ya msingi.

Kujitegemea kiuchumi ilikuwa ni moja ya malengo ya Mpango wa Tatu, baadae ilionekana kuwa lengo hili lisingefanikiwa bila kuwa na mafanikio katika sekta za jamii. Hata sasa, katika hatua za kurekebisha hali ya uchumi mchango wa sekta ya jamii ni muhimu na mkazo mkubwa umetiliwa katika uimarishaji wa huduma za afya.

Katika kutekeleza Mpango wa Tatu serikali ilitumia asilimia 9.4 ya bajeti yake kuendeleza huduma za sekta ya afya.

Hadi kufikia mwisho wa kipindi cha Mpango wa Tatu tulikuwa na vituo vya afya 250, zahanati 2,644 na hospitali 149. Kwa maana nyingine asilimia 95% ya watu vijijini na mijini walikuwa umbali usiozidi kilomita 10 kutoka kituo cha huduma za afya na asilimia 72% walikuwa umbali usiozidi kilomita 5 kutoka kituo cha huduma za afya.

Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto za mwaka 2016, Tanzania ina jumla ya vituo 7,471 vinavyotoa huduma za afya. Asilimia 73.7 vikimilikiwa na serikali na asilimia 26.3 vikimilikiwa na taasisi au watu binafsi. Jumla ya Zahanati zote nchini ni 7,193 zinazofanya asilimia 88.6 ya vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.

Jumla ya Vituo vya Afya vyote nchini ni 70 ambavyo ni asilimia 10.8 ya vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini. Jumla ya Hospitali zote nchini kutia ndani Hospitali ya Taifa Muhimbili ni chini ya asilimia 1 ya vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini. Jumla ya Hospitali Teule za Wilaya ambazo zilijengwa na Taasisi za Hiari ni 36, Jumla ya Hospitali za Wilaya ni 70, Jumla ya Hospitali za Rufaa ni 9. Jumla ya hospitali za Rufaa za Mikoa ni 23.

Jumla ya Hospitali za Rufaa za Kanda ni 5, Kanda ya Mashariki kuna Hospitali za Rufaa za Kanda mbili ambazo ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Lugalo inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi Tanzania (JWTZ) na Hospitali ya CCBRT inayomilikiwa na Taasisi Isiyo ya Kiserikali (NGO),  Kanda ya Ziwa kuna Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando ambayo inamilikiwa na Taasisi ya Dini ya Kikristo, Kanda ya Kaskazini kuna Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC inayomilikiwa na Taasisi ya Dini ya Kikristo, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuna Hospitali ya Rufaa ya Mbeya inayomilikiwa na Serikali.

Jumla ya Kanda tatu ndizo bado hazijapata Hospitali za Rufaa za Kanda ambazo ni Kanda ya Kati yenye Mikoa ya Singida na Dodoma ambako ni Makao Mkuu ya Serikali. Kanda ya Magharibi ikijumuisha Mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi na Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Mtwara na Lindi.

Jumla ya Hospitali za Taifa za Magonjwa Maalumu ni 4 ambazo ni Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili Mirembe, Hospitali ya Taifa ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu Kibong’oto, Taasisi ya Mifupa (MOI) na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI). Jumla ya Vituo vya Wazazi (Maternity Homes) ni 55. Jumla ya Nyumba za Kutunzia Wazee zenye huduma za afya ni 3 na jumla ya aina zingine za hospitali ni 59.

Alipokuwa akifungua mkutano wa 48 wa chama cha madaktari uliofanyika Novemba 2016, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema sekta ya afya inakabiliwa na upungufu mkubwa wa takribani asilimia 52 wa wataalamu wa afya katika kila ngazi ya vituo vya kutolea huduma za afya huku akiutaja upungufu huo kuwa umezidi kuwa juu vijijini ukikadiriwa kufikia asilimia 74.

Sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na msongamano mkubwa wa wagonjwa katika hospitali za wilaya, hospitali za mkoa, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za rufaa za kanda na hospitali ya taifa.

Huduma za afya zikiboreshwa katika ngazi ya msingi ya zahanati na vituo vya afya hospitali zinaweza zisipate msongamano wa wagonjwa kama ilivyo sasa. Uboreshaji wa huduma hizo unatia ndani uwepo wa rasilimali watu wenye ujuzi stahiki, madawa, vifaa tiba na mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

Serikali inapaswa pia kuimarisha mfumo wa rufaa ili wagonjwa ambao wanaweza kuhudumiwa katika ngazi za chini wasiruke ngazi za huduma na kwenda kutibiwa hospitali kubwa bila rufaa.

Azimio la Abuja lililofanyika miaka 15 iliyopita linazitaka nchi kutenga asilimia 15 ya fedha zote za bajeti ya nchi katika sekta ya afya, ambapo nchini mwetu lengo halijafikiwa kwa kuwa bajeti ya sekta ya afya ni chini ya asilimia 10.

Kulingana na takwimu za 2013, magonjwa 10 yanayosababisha vifo vingi zaidi nchini ni paoja na UKIMWI, Magonjwa ya Njia ya Chini ya Hewa, Malaria, Magonjwa ya Kuhara mfano Kipindupindu, Kifua Kikuu, Saratani mbalimbali, Magonjwa ya Moyo, Kiharusi (Stroke), Magonjwa Yanayoenezwa kwa Ngono na Maambukizi kwenye Damu (Sepsis).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *