Jamii imetakiwa kujenga utamaduni wa kuzungumza na kujadili mambo ya msingi yanayohusu maendeleo ili kuondokana na mifumo kandamizi ya haki za binadamu na kujenga jamii inayoheshimu usawa, upendo na amani.
Inaeleezwa kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji vinaendelea katika ngazi ya familia na jamii kwasababu baadhi ya watu wanaoshuhudia matendo maovu hawatoi taarifa kwa mamlaka husika ili zishughulikiwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Edda Sanga wakati akizungumza katika Uzinduzi wa Maonesho ya Miaka 30 ya TAMWA amesema jamii bado inakabiliwa na changamoto nyingi za ukatili wa kijinsia ambazo zinatokea katika familia lakini waathirika au watu wanaoshuhudia hawazungumzi hadharani ili kukomesha vitendo hivyo.
“Huko nyuma tumekuwa kimya sana haya mambo hatuyazungumzi kwa kuogopa kwamba nikiyatoa nje mambo ambayo yanahusu undani wa familia yangu nitaonekana kama vile ninakiuka misingi na haki za ustawi wa kabila langu”, amesema Edda Sanga.
Licha ya serikali kushirikiana na Asasi za Kiraia kuendelea kutoa elimu na kupambana na vitendo vya kikatili katika jamii, wananchi pia wanawajibika kupaza sauti na kukemea viashiria vyote vinavyokiuka usawa wa kijinsia na haki za wanawake na watoto ambao ndio waathirika wakubwa wa ukatili.
“Yaliyo mengi yanatokana na tulivyozaliwa na kulelewa katika mifumo hii ambayo haichangamkii haki za wanawake na watoto mfano mimba za utotoni. Ni vizuri jamii tukakaa tukazungumza. Ni wakati wa kuyatoa nje tuyazungumze ili suluhu apatikane palepale ambapo tukio limetokea”, amesema Edda Sanga.
Ripoti ya Uchunguzi ya Watu na Afya ya 2010 inaonyesha kuwa asilimia 10 ya wanawake walio na umri wa miaka kati ya 15 mpaka 49 waliripoti kulazimishwa kufanya mapenzi kwa mara kwa kwanza na 48% ya wanawake walioolewa wanapata udhalilishaji wa kingono.
Pia amewataka wanawake ambao wanashiriki kuwafanyia ukatili wanaume waache kwasababu wanadhalilisha utu wao na kukwamisha harakati za kuleta usawa na haki katika jamii ikizingatiwa kuwa kila mtu pasipo kujali hali yake ana haki ya kuishi kwa amani na kuwa na ustawi mzuri wa maisha yake.
“Tunapozungumza masuala hayo na mwanaume tumuhusishe ili na yeye ahamasike sasa kuingia hata kama ni kwa mawazo tu kwasababu haya masuala yanataka tubadilishe namna tunavyofikiri. Hatuwezi kubadilika kama tunaongea wanawake kwa wanawake ni lazima tuwe na wanaume huo ndio mfumo tunauchukua”, ameeleza Edda Sanga.
Katika miaka ya hivi karibuni wamejitokeza wanaume ambao wanafanyiwa ukatili na wake zao ikiwemo kupigwa, kutukanwa na hata kunyimwa tendo la ndoa. Lakini muitikio wake sio mkubwa ikilinganishwa na matukio yanayowapata wanawake na watoto.
Baadhi ya tafiti zinaeleza kuwa asilimia 35 ya wanaume wanapigwa na wake zao ingawa hawasemi kutokana na kuona aibu kwasababu bado mtazamo wa jamii umeegemea kwenye mfumo dume ambao unampa mwanaume nguvu ya kumtawala mwanamke.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IPP Media inayomiliki radio na televisheni, Joyce Mhavile (wa pili kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Edda Sanga (Wa pili kulia) katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa TAMWA baada ya uzinduzi wa Maonyesho ya Miaka 30 ya TAMWA
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IPP Media inayomiliki radio na televisheni, Joyce Mhavile amesema jamii inapaswa kutambua mchango wa Asasi za Kiraia katika kuchochea maendeleo na kuondoa aina zote ukatili wa kijinsia.
“TAMWA imeiwezesha jamii hapa nchini kuongea kwa uwazi kuhusu ukatili wa kijinsia na vitendo hivyo kuvichukulia hatua za kisheria pale inapotakikana”, ameeleza na kuongeza kuwa utendaji wa vyombo vya habari nchini katika kuibua na kuvisemea vitendo vya ukatili ni wa kupigiwa mfano ikizingatiwa kuwa unaendana na vipaumbele vya serikali katika kujenga jamii huru yenye kuthamini mchango wa wanawake katika kufikia malengo yake.
Pia amewataka wanawake kutambua kuwa wana fursa nyingi ambazo wakizifanyia kazi wataimarisha uchumi wa familia na taifa. Anasema wajikite katika kutengeneza bidhaa zenye ubora ambazo zinaweza kuhimili ushindani wa soko.
Naye aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Mwanaharakati wa Masuala ya wanawake, Fatma Mwasa amesema ili wanawake wafikie ndoto zao za kielimu na biashara wanapaswa kusimama imara na kutumia fursa zilizopo kujikomboa.
“Nitoe wito kwa watoto wa kike kwamba tupambane kwa fursa walizonazo hasa walio mashuleni na vyuoni walenge kupata elimu bora. Ukishakuwa na elimu nzuri na sifa zinazotakiwa kwenye kazi na kujadili nafasi unayopewa lakini kama umepungua kwenye sifa unataka uhurumiwe kwasababu ni mwanamke inakuwa ni changamoto kubwa sana”, ameshauri Fatma Mwasa.
Maadhimisho ya Miaka 30 ya TAMWA yamezinduliwa leo na yanatarijiwa kufikia kilele Novemba 17 mwaka huu huku chama hicho kikijivunia kutimiza dira yake ambayo ni Tanzania yenye amani inayoheshimu haki za binadamu kwa mtazamo wa kijinsia.
Malengo Ya Maendeleo Endelevu
Katika Lengo la 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s 2030) linasisitiza Usawa wa Kijinsia katika jamii na linakusudia kuondoa aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika sekta binafsi na Umma ikiwemo usafirisha wa watoto, udhalilishaji kingono na aina zote unyanyasaji.
Ili lengo hilo litimie linazitaka nchi wahisani kutunga na kuimarisha sera madhubuti na sheria zinazolenga kukuza usawa wa kijinsia na kumuwezesha mwanamke na msichana katika Nyanja zote.