IFFEd yabeba jukumu la kuinua elimu Kusini mwa Jangwa la Sahara

Jamii Africa

Rais mstaafu Jakaya Kikwete ameungana na makamishna wengine wa Tume ya Elimu ya Umoja wa Mataifa (UN) kuanzisha Mfuko wa kimataifa  elimu (IFFEd) ambao unalenga kutatua changamoto sugu za elimu duniani.

Uzinduzi wa mfuko wa IFFEd ulifanyika hivi karibuni New York, Marekani zilipo ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Mfuko huo unakusudia kukusanya Dola  za Marekani 10 bilioni (Tsh. 22.8 trilioni) ili kusaidia utekelezaji wa lengo la 4 la Malengo ya Maendeleo Endelevu  (SDG’s) ya 2030 ambalo linahimiza kila mtoto kupata haki ya elimu bora ya awali, msingi na sekondari.

Makamishna wa Tume ya Elimu Duniani akiwemo rais Jakaya Kikwete watafanya kazi na nchi ambazo zina dhamira ya dhati kuinua elimu ambapo katika awamu ya kwanza fedha hizo zitatolewa katika maeneo milioni 200 ya shule kwaajili ya watoto na vijana wadogo.

Pia IFFEd itasaidia kukomesha mimba ya utotoni, kazi ngumu na usafirishaji  watoto, ubaguzi kwa wasichana unaowazuia kwenda shule. Kuondoa tatizo la kutokujua kusoma na kuandika ambalo limeathiri watu wazima milioni 750 ambao theluthi mbili ni wanawake.

Mfuko huo utafungua milango wa utekelezaji wa malengo mengine ya SDG’s ya afya, jinsia, usawa, ajira na ustawi wa maisha ambayo yanahusiana moja kwa moja na maendeleo ya elimu duniani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mfuko wa IFFEd, Balozi wa Elimu katika Umoja wa Mataifa, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown alisema mfuko huo ni matokeo ya pendekezo la vijana milioni 1.5 ambao waliitaka UN kuunda chombo kitakachosaidia kutatua kero za elimu duniani.

“Ni muda muafaka kuyafanya yasiyowezekana yawezekane,” alisema Brown na kuongeza kuwa mfuko huo utaongezewa nguvu na UN, Benki ya Dunia an Benki za Maendeleo za Kanda.

“Sasa vijana milioni 11.5 wanataka mabadiliko. Leo watoto milioni 260 hawapo shuleni, hata katika mwelekeo wa sasa wa 2030, watoto milioni 400 hawajapata elimu hata baada ya kuvuka miaka 11; na na nusu ya watoto milioni 800 wenye umri wa kwenda shule watakuwa hawa sifa, watashindwa kufurahia ubora wa elimu,” alisema Gordon.

Inaelezwa kuwa ikiwa hali hiyo itaachwa iendelee idadi kubwa ya watoto watakosa elimu na matokeo yake ni kuwa na kizazi cha watu wasioelimika. Idadi hiyo itahusisha watoto milioni 75 ambapo milioni 10 ni wakimbizi katika nchi zenye mapigano ya kisiasa.

“ Haki ya kusoma ya watoto haiwezi  kupatikana kwa mbinu za kawaida tukizingatia kuwa tuko nyuma sana katika utekelezaji wa Maendeleo Endelevu. Lengo la watu kuwa shuleni linahitaji mbinu zisizo za kawaida, ikiwezekana juhudi za binadamu,” alisema Brown.

Mfuko huo utatumia njia ya ufadhili wa kisasa kwa matatizo makubwa ya elimu duniani ikiwemo kutokujua kusoma na kuandika ili kufikia lengo la dharura la haki ya elimu kwa kila mtoto.

 

Kwanini haki ya elimu kwa mtoto?

Haki ya elimu ni haki ambayo iko kwenye Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu la 1948, Mkataba wa Haki za Watoto wa 1989, Mkataba wa Dunia wa Elimu kwa Wote wa 1990 na ilitamkwa kwenye Jukwaa la Elimu lilifanyika Dakar, Senegal mwaka 2ooo. Lakini ni ahadi hiyo haijatekelezwa kikamilifu.

Hivi sasa, asilimia 1 tu ya fedha zinazotolewa na benki za Maendeleo kwenye nchi zenye uchumi wa kati huelekezwa kwenye elimu katika nchi za Afrika na Asia. Katika nchi hizo, wanafunzi wanakabiliwa na changamoto nyingi za kielimu. kuongeza bajeti za elimu zinazolenga kuboresha mazingira ya kusomea kutasaidia kuongeza idadi ya watoto walioelimika duniani.

Mfuko huo unaenda sambamba na juhudi za nchi wahisani zinazoshirikiana na mashirika ya kimataifa ikiwemo, UNESCO, UNICEF, UNHCR ambayo yote yanalenga kuondoa ujinga na kuboresha maisha ya mtoto.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *