Japan yatoa bilioni 77.3 ujenzi wa barabara ya New Bagamoyo itakayotumiwa na mabasi ya mwendo kasi

Jamii Africa

Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA), imeipatia Tanzania msaada wa shilingi bilioni 77.3 kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya New Bagamoyo, kuanzia Morocco hadi Mwenge, Jijini Dar es Salaam ili kupunguza masongamano wa magari.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 4.3 Itahusisha ujenzi wa barabara yenye njia nne pamoja na kuanza kwa awamu ya nne ya ujenzi wa barabara itakayotumiwa na mabasi ya mwendo wa haraka (BRT phase IV).

Utafiti uliofanyika hivi karibuni unaonesha kuwa Barabara ya Bagamoyo ndiyo yenye msongamano mkubwa wa magari  ambapo kwa siku moja magari 52,000 hupita kwenye barabara hiyo.

Akizungumza katika hafla ya kuweka saini kwa makubaliano ya kupokea msaada huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amesema kuwa barabara hiyo ikikamilika itasaidia  kutatua changamoto ya msongamano wa magari yanayotoka na kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

"Upanuzi wa Barabara ya New Bagamoyo si tu kwamba utaondoa msongamano wa magari, bali pia ni kiungo muhimu cha Bandari ya Bagamoyo ambayo itarahisisha usafirishaji wa abiria, mizigo na huduma kutoka Jiji la Dar es Salaam, mkoa wa Pwani na mikoa mingine nchini" Alisema.

Awali Japan ilitoa msaada mwingine Septemba, 2017 wabilioni 1.4 ambazo zilitumika kufanya upembuzi yakinifu wa barabara hiyo itakayoanza kujengwa hivi karibuni.

Katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo, Japan ilitoa bilioni 99.5. kujenga barabara ya njia nne katika kipande cha kilometa 12.9 kutoka makutano ya barabara ya Tegeta na makutano ya barabara ya Mwenge pamoja na kukamilisha ujenzi wa madaraja ya Mlalakuwa, Lugalo na Tegeta.

“Si mara ya kwanza kwa Japan kuisaidia Tanzania, wanajenga barabara za juu katika makutano ya Tazara, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Dodoma hadi Babati mkoani Manyara (km 188.15), Tunduru-Mangaka – Mtambaswala (km 202) na barabara ya Iringa hadi Dodoma (259.9)” alisisitiza James.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia), akizungumza na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Masaharu Yoshida (katikati)na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini-TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale. baada ya tukio la kusaini mkataba wa msaada wa Shilingi bilioni 77.3 .

Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaharu Yoshida amesema kutolewa kwa msada huo ili kuwezesha awamu ya pili ya ujenzi wa barabara kutasaidia   kupunguza msongamano wa magari kwa kiasi kikubwa na kuokoa fedha nyingi zinazotokana na changamoto za msongamano huo.

"Ili kukamilisha usanifu wa kina wa mradi huu, nilisaini mkataba wa usanifu  wa mradi wa upanuzi wa barabara ya new Bagamoyo  (Awamu ya Pili) miezi mitano iliyopita, hatimaye sasa ninasaini mkataba wa sehemu kuu ambayo ni ujenzi wenyewe" Amesema Balozi Yoshida.

Balozi huyo,, amesema mradi huo utasaidia kuboresha ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini nchini na kwamba msaada huo ni mwendelezo wa kudumisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Japan na Tanzania.

Makubaliano ya msaada huo yametiwa saini Februari 28, 2018, Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, kwa niaba ya Serikali, na Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaharu Yoshida na kushuhudiwa na Mwakilishi Mkazi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Japani (JICA), Toshio Nagase na Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Barabara nchini-Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *