Je ni sawa kufanya mazoezi kabla ya kula?

Jamii Africa

Mazoezi ni sehemu muhimu ya kuufanya mwili kuwa imara na wenye afya, lakini kumekuwa na mijadala mbalimbali juu ya kufanya mazoezi ukiwa na njaa au tayari umekula chakula.

Baadhi ya wataalamu wa afya ya binadamu wanasema kufanya mazoezi kabla ya kula kunamuweka mtu katika hatari ya kupoteza fahamu kwasababu sukari inakuwa imepungua katika mzunguko wa damu.

Jarida la TIME la afya lilimuhoji Prof. Douglas Paddon-Jones ambaye ni Mtafiti wa Sayansi ya Misuli ya Mwili ambapo alisema;

“Ukiwa umechoka au una hofu huwezi kufanya kazi vizuri tofauti na kama utakuwa umekula chochote. Ukila chakula cha kutosha kitakusaidia kufanya kazi zako kwa ufanisi huku ukiwa na nguvu zaidi”

Inashauriwa kwa watu wazima walio na umri zaidi ya miaka 55 kula kabla ya kufanya mazoezi hasa wakati wa asubuhi ambapo mtu anakuwa ametoka usingizini.

“Usiku mzima miili yetu hujiweka sawa ili kutuwezesha kuishi na kitendo hicho husababisha kiwango cha sukari kilichopo kwenye damu kupungua” anasema Prof. Nancy Rodriguez wa Sayansi ya Lishe katika Chuo Cha Connecticut.

Anafafanua kuwa kufanya mazoezi asubuhi kabla ya kula husababisha mwili kufanya kazi katika hali ya kuchoka na inaweza kusababisha kupungua kwa misuli.

Wataalamu hao wanasema ikiwa lengo la mazoezi ni kupunguza uzito, kufanya mazoezi kabla ya kula inaweza kuwa njia sahihi lakini tafiti zinahitajika zaidi katika eneo hili.

Mazoezi kabla ya kula

“Kuna baadhi ya tafiti zinakubaliana na hoja ya kufanya mazoezi ukiwa na njaa kwasababu husaidia kuchoma mafuta kuliko ukiwa umeshiba” Prof. Paddon-Jones anaeleza katika jarida la TIME.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Obesity Society mwaka 2013 unaonyesha kuwa watu 64 ambao walikuwa na uzito uliopitiliza walianzishiwa program maalum ya kufunga kwa siku kadhaa na kula asilimia 25 tu ya chakula wanachokula kila siku. Waliposhiriki zoezi hilo matokeo yalionyesha kupungua kwa uzito bila ya kufanya mazoezi na kuzingatia mlo kamili.

Hata hivyo, hakuna jibu la moja kwa moja. Baadhi ya tafiti zimeshindwa kuthibitisha faida za kupunguza uzito kwa kufunga ikilinganishwa na kula chakula cha asili. Watafiti wengine wanapendekeza kuwa kutokunywa chai asubuhi ni hatari kwa afya.

Waatalamu wanashauri kuwa ikiwa mtu anataka kufanya mazoezi akiwa amefunga ni muhimu kumuona Daktari ili achunguze afya yake na kutoa mapendekezo yake. Na hili litategemea mlo anaopata mtu kila siku.

Watu wazima walio na umri zaidi ya miaka 50 wanapaswa kuwa makini katika kufanya mazoezi wakiwa wamefunga. “ Kadiri mtu anapokuwa na  umri mkubwa protini katika mwili huongezeka, na anahitaji mazoezi ya kila siku ili iweze kutumika vizuri” anasema Shivani Sahni, Mkurugenzi wa Programu ya Lishe katika Chuo Cha Harvard Marekani.

“Nafikiri kuna haja ya kulitaza kwa kina suala hili kabla ya kukubali kuwa kufanya mazoezi ukiwa umefunga ni sawa kwa aina fulani ya watu”.

Watu ambao sio wakiambiaji wa mbio ndefu, wanashauriwa kula chakula kabla ya mazoezi ili kuusaidia mwili kuchoma mafuta. Prof. Rodriguez anapendekeza kula chakula chenye protini na wanga muda mfupi kabla ya kula, “ Kula kipande cha ndizi mbivu, karanga na yai lililochemshwa”. Anasema mtu asile chakula kingi bali kidogo ili kuamsha nguvu za mwili kwa ajili ya mazoezi.

Baada ya mazoezi kunywa maji kiasi na subiri dakika 60 mpaka 90 kabla ya kula chakula ili kuandaa mfumo wa mmeng’enyo kupokea chakula.

Kumbuka wakati wote kumuoana daktari ili akushauri njia sahihi unayoweza kutumia kufanya mazoezi ili kuepuka matatizo ya kiafya yanayoweza kujitokeza.

 

 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *