Je, unafahamu watu wanapataje Mzio (Allergy) ya vitu, hali ya hewa au vyakula?

Jamii Africa

Watu wanaweza kupata mzio wa vitu au vyakula katika namna mbili; Kwanza, wanawaweza kuwa na mzio wa kitu fulani tangu kuzaliwa (Hii ni kutokana na vinasaba vyao) au wanaweza kupata mzio kadiri umri unavyosogea (wanavyokua).

Nadhani umeshawahi kuona watu wakipata mzio katika umri mkubwa na pia umeshaona wale ambao wana mzio tangu kukua kwao. Pia kuna mazingira hutokea baadhi ya watu wakipoteza mzio waliokuwa nao wa kitu fulani. Hali hizi hutokeaje? Inakuaje mtu anapata mzio au anaacha kuwa na mzio aliokuwa nao mwanzo wa kitu fulani?
Tuanze na mambo ya msingi kwanza…

Mzio ni nini (What is allergy)?
Mzio ni hali inayojitokeza pale kinga ya mwili ya binadamu inapokuwa na mwitikio mkubwa sana (mwitiko hasi) kuliko kawaida juu ya mazingira au chakula fulani, lakini mara nyingi kitu hicho huwa hakina madhara kwa watu wengine.

Mzio hujulikana kama magonjwa ya mzio, maana mzio wa vitu vingi huweza kusababisha magonjwa mengine au matatizo ya kiafya ikiwemo pumu, homa kali na mengineyo.

Japokuwa kuna mzio unaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya ikiwemo pumu lakini sio hali zote za mzio husababisha madhara ya kiafya, hasa yale yanayogundulika mapema na kutibiwa haraka.

Visababishi maarufu vya mzio
Kuna vitu vingi vinavyoweza kusababisha mzio kwa binadamu. Hivi ni baadhi ya visababishi (sio vyote vina madhara makubwa kwa mwili wa binadamu): karanga, papai, nyama, marashi, mayai, samaki, dawa, dhahabu pamoja na aina fulani za nguo.

Pia kuna watu wana mzio wa vumbi au uchafu na wengine vipindi fulani vya majira na nyakati. Idadi kubwa ya visababishi hivyo ni vile ambavyo vinavyopatikana kwenye mazingira. Kuna baadhi ya mizio husababishwa na aina fulani za dawa na hizi huwa sio nzuri.

Dalili za mzio 

Aina tofauti tofauti za mizio huleta dalili ambazo ni tofauti pia. Dalili ambazo huwapata watu wengi ni chafya za mara kwa mara, mafua, homa, ngozi kuwasha, kushindwa kupumua vizuri, kukohoa na mengineyo.

Baadhi ya mizio huweza kudhibitiwa kirahisi sana ikiwemo kuacha kutumia kitu hicho au kukaa kwenye mazingira yanayokudhuru. Hii ndio njia inayokubalika zaidi kukabiliana na mizio isiyosababisha sumu mwilini. Mfano, mtu ambaye hapatani na aina fulani ya majani anachotakiwa kufanya ni kukaa mbali na mazingira yenye majani hayo. Hivyo hivyo kwa wale wasiopatana na wanyama fulani.

Mpaka hapa unaweza kuelewa vitu ambavyo watu hawapatani navyo. Lakini Je, watu wanapataje mzio? Kwanini wanapata? Kwanini mwili wa binadamu hukikataa kitu fulani ghafla?

Tunapataje mzio?
Mzio hutokea pale kinga ya mwili inapokosea kukitambua kitu fulani kipya kilichoingizwa mwilini na kinga hiyo kuanza kushindana nacho. Dalili kama vile mafua, chafya za mara kwa mara au mapafu kushindwa kuchuja hewa huwa ni matokeo ya kinga ya mwili kukishambulia kitu kipya kilichoingizwa mwilini.

Kwa wale ambao hupata mzio ukubwani hupatwa na hali hii pale kinga za mwili yao zinapokutana na kitu kipya na kushindwa kukitambua na kuanza kukishambulia kitu hicho. Na hii husababisha seli zingine za kinga ndani ya mwili nazo kufuata mkumbo wa mashambulizi kwa kile kitu kigeni kilichoingia mwilini na kukitambulisha kama ‘hatari’.

Kadiri mtu anavyozidi kuwa karibu au kutumia kitu kinachomdhuru ndivyo anavyozidi kuwa na hali mbaya kiafya. Kadiri mtu anavyozidisha kuwa kwenye mazingira hatarishi ndivyo mwili unavyozidi kutengeneza seli za kinga ambazo huongeza mashambulizi na dalili za mzio huongezeka au kuzidi kuwa mbaya.

Hivi ndivyo ambavyo watu hupata mzio juu ya kitu au hali fulani. Sasa tuangalie kitu kingine kuhusu hali hii.

Tunawezaje kuzuia mzio (How to stop allergy)

Kuna namna mbili (2) ambazo watu wanaweza kuzitumia ili wasipate mzio wa vitu mbalimbali: Hizi zinaweza kufanya mzio ukapotea kwa muda fulani au kupotea kabisa.

Zamani watu walikuwa wakipona mzio pale walipozidisha matumizi ya kile kilichokuwa kinawadhuru. Kwa maneno mengine, unaweza kusema kuwa kinga zao za mwili zinakuwa sugu na kugundua kwamba zilikuwa zikishambulia kitu kisicho na madhara yoyote.

Pia watu huweza kupona mzio ghafla tu, kama ambavyo huupata ghafla. Hilo hufanywa na kinga ya mwili yenyewe; Kinga huweza kuanza kuua seli za mzio yenyewe hasa pale inapogundua kwamba seli hizo zinadhoofisha kinga ya mwili inaposhambuliana nazo. Hivyo kinga ya mwili huua seli zake yenyewe na mtu hupona mzio aliokuwa nao.

Namna nyingine ya kuzuia mzio ni matibabu. Unaweza kupata matibabu fulani ili kuua seli zote zinazosababisha mzio. Njia hii inaweza kuleta madhara fulani hasa yale ambayo ni hatari kwa uhai wa mtu. Jambo la muhimu ni kwamba ukihisi hali tofauti kwenye mwili wako ni vema kumuona daktari kwa ushauri zaidi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *