Polisi kuwalinda wanaoshambuliwa na wananchi ili kupunguza vifo vinavyotokana na uhalifu

Jamii Africa
Msemaji wa Jeshi la Polisi, ACP Barnabas Mwakalukwa amesema kuna masuala ya uchunguzi ambayo hayatolewi kwa umma kwa sababu yataharibu upelelezi na mengine hufichwa ili kulinda usiri wa mlalamikaji - Ametolea mfano uchunguzi juu ya tuhuma za kamera za CCTV kung'olewa kwenye eneo ambalo Tundu Lissu alipigwa risasi kuwa hawawezi kusema kwa kuwa litaathiri uchunguzi. - ACP Mwakalukwa ameyasema hayo jioni hii akiwa kwenye kipindi cha #NjooTuongee kinachorushwa kila siku ya Ijumaa, saa 12 na nusu jioni.

 Ili kupungu za vifo vinavyotokana na uhalifu nchini, Jeshi la Polisi limesema litawalinda wahalifu wanaokamatwa na kuuwawa na wananchi ambao wanajichukulia sheria mkononi.

 Hatua hiyo ya Jeshi la Polisi ni mkakati wa kudhibiti chuki iliyojengeka katika jamii dhidi ya wahalifu ambao wakikamatwa  hupigwa mpaka kufa. Wananchi wanapaswa kuwakamata wahalifu na kuwakabidhi polisi ili hatua za sheria zichukuliwe lakini baadhi ya wananchi hukosa uvumilivu na kuwashambulia wahalifu.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, ACP Barnabas Mwakalukwa, akihojiwa katika kipindi cha ‘Njoo Tuongee’ kinachorushwa na runinga kwa udhamini wa Twaweza na JamiiForums amesema Jeshi hilo limepewa dhamana ya kuwalinda wananchi na mali zao na kwamba watahakikisha wahalifu wanaokamatwa hawauwawi lakini wanafikishwa katika vyombo vya sheria na kupatiwa haki zao.

“Pale ambapo wale wachache ambao wanakwenda kinyume na sheria, wananchi wanapokosa nafasi ya kuripoti na Polisi kuwahi kuwakamata wale wahalifu na ile kero ikizidi kutoka kwenye  jamii hiyo hiyo ya watu wachache wananchi wanajichukulia sheria mkononi” anaeleza ACP Mwakalukwa na kuongeza kuwa,

“Jeshi la Polisi ambalo ndio limepewa dhamana ya kulinda maisha ya watu, wanapaswa kuhakikisha hata wale wanaokiuka tuwalinde ili tupunguze idadi ya vifo vinavyotokana na kujichukulia sheria mkononi”.

ACP mwakalukwa amesema suala la kuwanusuru wahalifu na kifo linawezekana ikiwa wananchi wa kada mbalimbali watashirikiana na Jeshi la Polisi kuwatambua waharifu katika maeneo yao na kuhakikisha wanarejeshwa kuwa wananchi wazalendo.

Amesema hatua ya kwanza inaanzia katika ngazi ya familia kwa wazazi kuwalea watoto wao katika maadili na kuwafunza kuwa raia wema wanaopenda amani, “Wadau kama hao tunaanzia na familia, wazazi  wakatoa elimu bora ya malezi wakasaidiwa na viongozi wa taasisi za kidini wakawabadilisha kutoka kwenye tabia zile mbaya itasaidia sana”, amesema ACP Mwakalukwa ambapo kupitia programu ya  polisi jamii wanaendelea kupambana na uhalifu.

Kulingana na Uchunguzi wa Twaweza (2017) ambao uliangazia haki za raia hata za wale wanaofanya uhalifu, imedhihirika kuwa wananchi wengi bado wanashauri watu wanaokamatwa kwa makosa ya uhalifu wauwawe. Asilimia 54 ya wananchi walisema wanasheria hawatakiwi kuwatetea waharifu kwa sababu wanavunja sheria, lakini asilimia 95 walisema Afisa Askari akimkamata mhalifu anatakiwa kuwa na mamlaka ya kumuua kwa sababu ni muovu.

Maoni ya wananchi yanaashiria kuwa bado  haki ya kuishi bado haizingatiwi ipasavyo katika jamii kwa sababu zaidi ya nusu ya wananchi wanataka mhalifu auwawe hata kabla sheria haijamkuta na kosa. Inaelezwa kuwa kasumba ya wananchi kujichukulia sheria mkononi inatokana na kutokuwa na imani na Polisi ambao katika tafiti mbalimbali zinathibitisha kuwa taasisi hiyo imekithiri kwa rushwa.   

  Uchunguzi wa Twaweza unaonyesha kuwa tishio kubwa la usalama wa wananchi ni wizi wa mali ambao ni asilimia 61 ya matukio yote ya uhalifu unaotokea katika jamii ambapo huleta hasara na wakati mwingine kusababisha majeraha na vifo. 

 

Hata hivyo, ACP Mwakalukwa amewataka wananchi kupitia mamlaka za serikali za mitaa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kukomesha vitendo vya uhalifu, ikizingatiwa kuwa wananchi wanawaamini sana viongozi wa mitaa kuliko Polisi. Ikiwa watatoa taarifa na ushahidi itasaidia kupunguza uhalifu katika jamii.

“ Hata utafiti umeonesha taarifa zingine za uhalifu wanapendelea zaidi wapeleke kwa Mwenyekiti wa serikali ya mtaa itakuwa ni rahisi kuondoa hiyo kero. Ushiriki unaanza na mambo matatu; jambo la kwanza ni kutambua ni aina gani ya uhalifu unatokea, ni vijana gani wanaoshiriki kufanya uhalifu na waathirika wa aina gani wanaolengwa kusudi waweze kulindwa, hatua zichukuliwe na kutanzuliwa na mahakama”

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *