Jinsi Intaneti inavyofanya kazi kwenye ndege

Jamii Africa

Intaneti iko kila mahali. Inapatikana ofisini, kwenye maduka makubwa, hata vituo vya mabasi utaipata huduma hiyo. Sio tena anasa lakini kiuhalisia ni fahari na haki ya kuzaliwa hasa kwa wakazi wa mijini.

Intaneti inamuwezesha mtumiaji wa simu au kompyuta kuangalia video, kusikiliza na kusuma taarifa akiwa popote na wakati wowote. Lakini umewahi kujiuliza huduma ya intaneti (Wi-Fi) kwenye ndege inapatakanaje na inafanyaje kazi ?

Kimsingi ndege zinatumia intaneti (wireless internet ) ambayo hutolewa na watoa huduma za intaneti (ISP). Huduma hiyo huunganishwa na ndege iliyopo angani na mnara wa simu uliopo ardhini ambao una mawasiliano ya moja kwa moja ya intaneti.

Mnara wa simu unawasiliana na kifaa cha ndege kupitia mawimbi ya radio. Gridi za minara ambazo ziko maeneo mbalimbali hukakikisha ndege iliyopo angani inaunganishwa wakati wote bila kuathiri upatikanaji wa huduma hiyo wakati ikisafiri kutoka eneo moja hadi nyingine.

        Minara ya simu inatuma mawimbi ya redio kwenye ndege kuwezesha intaneti

Wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano ya anga wanaeleza kuwa huduma ya intaneti inafanya kazi kama simu za mkononi ambazo zinategemea minara iliyosimikwa katika maeneo mbalimbali ili kuwezesha mawasiliano na intaneti kwa haraka na rahisi.

Huduma ya intaneti kwenye ndege hutolewa na kampuni kubwa kama Gogo Inc. ambayo inamiliki minara ya simu katika maeneo mbali mbali duniani.

Changamoto ya huduma hiyo ni kwamba hupatikana zaidi kwa ndege zinazoruka ndani ya nchi moja.  Ikiwa ndege itapita eneo ambalo halina minara hiyo kama juu ya bahari, intaneti itakata.

Kwasababu minara haiwezi kuwekwa kila mahali, ndege inapopita, intaneti nayo hutoweka na huimarika zaidi sehemu yenye minara.  Lakini wakati mwingine hali ya hewa inaweza kuathiri mawasiliano ya ndege na minara.

Ku na Ka-band

Mapungufu ya huduma za intaneti yanayotolewa na minara yanaweza kutatuliwa kwa msaada wa setilaiti ambayo huzungukazunguka kwenye uso wa dunia. Setilaiti hizo huwasiliana na ndege kupitia kipande cha mawimbi yajulikanayo kama Ku-band.

Setilaiti inatenda kazi kwa kioo akisi ambacho kinaakisi ishara kutoka kwenye mnara wa simu hadi kwenye ndege. Kinachofanyika ni kwamba Antena hufungwa juu ya ndege ikiwa imefunikwa na kisahani kidogo ili kudaka mawimbi kutoka kwenye setilaiti na kuyaelekeza kwenye kifaa kinachowezesha intaneti ndani ya ndege.

         Picha na Gogo Inc.

Teknolojia hiyo ya setilaiti inaweza kutoa intaneti yenye kasi ya Mbps  30 hadi 40, lakini kwasababu setilaiti huudumia ndege zaidi ya moja kwa wakati mmoja, kasi inaweza kupungua. Lakini pia maeneo yenye bahari yanaathiri upatikanaji wa intaneti japokuwa kasi inabaki ileile wakati ukiperuzi Facebook na Youtube.

Kama utahitaji laivu video italazimika kuhamia kwenye mawimbi ya Ka-band. Teknolojia ya Ka-band inakupa intaneti yenye nguvu ndani ya ndege. Inatumia setilaiti ya ya ViaSat1 ambayo kasi yake ni kubwa kwa Mbps 70 hadi 80 sawa na kasi ambayo mtu anafurahia akiwa anatumia intaneti ya nyumbani au ofisini.

Hata hivyo huduma hii ni ghali, inapatikana tu kwa wenye uwezo wa kuinunua. Hupatikana zaidi kwenye ndege kubwa kama JetBlue, Virgin America na Emirates.

 

Kwanini siyo kila ndege inatoa huduma ya Wi-Fi?

Sababu mojawapo tayari tumeiongelea hapo juu- kwamba huduma hiyo ni ghali. Ndege nyingi hazina huduma ya Ku-band kwasababu antenna inayowekwa juu ya ndege inatatiza au yumbisha mwelekeo.

Wataalamu wa anga wanaeleza kuwa kisahani kinachoshikilia antenna ni kinene na kizito; kwa maana hiyo injini ya ndege inatumia mafuta mengi kuhimili uzito wa ziada. Wamiliki wa ndege watatumia pesa nyingi kuwafurahisha wateja wao watapandisha bei ya tiketi ili kufidia gharama za intaneti.

Bahati nzuri, Wahandisi wanaendelea na mchakato wa kutengeneza antenna nyembamba, nyepesi na yenye gharama ndogo inayoweza kutumia mafuta kidogo.

Ikiwa watafanikiwa, watasaidia kuokoa mafuta na fedha nyingi zinazotumika kutoa huduma hiyo.

Naamini hata kasi ya intaneti itaboreshwa ili wasafiri wa ndege wafurahie ukuaji wa teknolojia kwa kutazama na kuperuzi kwa uhuru mambo wayatakayo wakati wakiwa angani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *