Jinsi ya kukabiliana na ‘Shambulio la Usingizi’ linaloambatana na kupooza

Jamii Africa

Umewahi kusikia  hali ya kuishiwa nguvu au kushindwa kusogeza viungo vya mwili muda mfupi baada ya kulala au kumka? Au unakosa usingizi wa uhakika? Naamini watu wengi imewatokea hali hii ambayo huleta hofu na kukosa kujiamini.

Kitaalamu inajulikana kama ‘Sleep Paralysis’ na tafsiri yake ni kupooza kwa muda mfupi au kushindwa kufanya kazi kwa misuli ya mwili ukiwa umelala. Mara nyingi hutokea kwa mtu muda mfupi baada ya kulala au akiwa ametoka usingizini. Mhusika hushindwa kusogeza viungo na kutoa sauti hapati usingizi wa uhakika.

Kulingana na chuo cha American Academy of Sleep Medicine,  wale wanaopooza wanapata hali hiyo kwa mara ya kwanza kati ya umri wa miaka 14 na 17. Ni tatizo la kawaida la usingizi ambapo watafiti wanakadiria kuwa inawatokea watu kwa asilimia  5 mpaka 40.

Matukio ya kupooza wakati umelala yanaweza kuambatana na matatizo mengine ya usingizi yanayojulikana kama ‘narcolepsy’. Narcolepsy ni matizo ya usingizi ambayo husababishwa na kupata usingizi kwa ghafla au ‘shambulio la usingizi’ na mtu kulala muda mrefu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Kliniki ya Mayo (Mayo Clinic), watu ambao hawana matatizo ya kupata shambulio la usingizi bado wanaweza kuonyesha dalili za sleep paralysis. Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa maradhi hayo sio hatarishi licha ya kuwatokea watu wengi.

Kwa karne nyingi, maradhi ya kupooza wakati umelala yamekuwa yakielezewa kwa namna mbalimbali na mara nyingi yamekuwahusishwa na jinamizi; sauti na picha za kutisha ambazo humjia mtu akiwa amelala.

 

Dalili za Sleep Paralysis

Kupooza ukiwa umelala sio maradhi ya dharula. Ukizifahamu dalili zake inaweza kukupa amani ya moyo.

Dalili kubwa ambayo inajitokeza zaidi ya ‘sleep paralysis’ ni kushindwa kuongea na kusogeza viungo vya mwili ikiwemo mikono na miguu. Matukio hayo yanaweza kudumu kwa dakika mbili au zaidi.

Matukio hayo huisha yenyewe au ikiwa mtu mwingine amekugusa na kukubeba. Kwa kawaida unakuwa unaelewa kinachoendelea lakini huwezi kutembea au kuongea wakati kupooza huko kunatokea. Pia unaweza kukumbuka jinsi kupooza kulivyotokea muda mfupi baada ya hali hiyo kuondoka.

 Mara chache sana, baadhi ya watu wanye ‘sleep paralysis’ hupata usingizi wa mang’amu ng’amu unaombatana na picha na sauti za vitisho lakini hazina madhara na wengi hupenda kuziita ndoto za mchana.

 

Nani yuko katika hatari ya kupata ‘Sleep Paralysis’

Takwimu zinaonesha kuwa watu 4 kati ya 10 wanaweza kuwa na tatizo la kupooza wakati wa kulala. Maradhi haya hugundulika zaidi kwa watoto lakini wanawake na wanaume wa umri wote wanaweza kupata. Pia linaweza kuwa tatizo la kifamilia. Sababu nyingi ambazo zinahusishwa na aina hiyo ya kupooza ni:

  • Kukosa usingizi

  • Ratiba za kulala zinazo badilika badilika
  • Matatizo ya afya ya akili ikiwemo msongo wa mawazo au kupoteza fahamu
  • Kulalia mgongo
  • Matatizo mengine ya usingi kama shambulio la usingizi au miguu kukaza
  • Matumizi ya baadhi ya dawa za hospitalini
  • Matumizi ya dawa za kulevya
  • Kupata kiwewe (TRAUMA)

 

Matibabu ya Sleep Paralysis

Dalili za kupooza wakati umelala zinatatulika zenyewe kwa dakika chache baada ya tukio hilo kutokea na haziwezi kusababisha matatizo makubwa ya kiafya. Ingawa, inaweza kusababisha hofu na mashaka.

 Kupooza ambako kunatokea kwenyewe hakuhitaji matibabu, labda kwa mtu ambaye ameonyesha dalili za shambulio la usingizi ‘narcolepsy’ anaweza kumuona daktari kwa ushauri, kama maradhi hayo yanaingilia kazi na maisha ya kawaida ya nyumbani.

 Daktari anaweza kufanya uchunguzi wa usingizi wako kwa kutumia kipimo cha  ‘polysomnography’ ambapo uchunguzi huusisha kulala hospitalini au kwenye kituo cha uchunguzi wa mwenendo wa usingizi.  Daktari atakuandikia dawa za kutumia ili kukabiliana na ‘sleep paralysis’ ikiwa imeshababishwa na ‘narcolepsy’.

 

 Dondoo muhimu za kukuepusha na Sleep paralysis…

Unaweza kupunguza dalili au matukio ya kupooza kwa kubadilisha baadhi ya mambo:

  • Punguza msongo wa mawazo au mkazo katika maisha yako
  • Fanya mazoezi kila siku lakini isiwe muda mfupi kabla ya kulala
  • Pata muda wa kutosha wa kupumzika
  • Tengeneza ratiba nzuri ya kulala
  • Fuatilia dawa unazotumia kwa tatizo lolote
  • Fahamu athari za upande pili na muingiliano wa dawa tofauti unazotumia ili ujiepushe na athari hizo ikiwemo kupooza wakati umelala.

Hata hivyo, ni muhimu kumuona daktari ikiwa unahisi kuna tofauti inayotokea wakati wa kulala ili akufanyie uchunguzi wa kitabibu atakaotoa suluhisho la afya yako.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *