Kakao ilivyoboresha maisha ya wakulima Kilombero, Kyela; wajasiriamali wahimizwa kuchangamkia fursa ya soko

Jamii Africa

Kila mtu anapenda chokoleti (chocolate). Labda sio kila mtu lakini watu wengi wanapenda. Zao la kakao ambalo hutokana na mti wa Theobroma ndio hutumika kutengenezea chokoleti ambapo hutafsiriwa kama ‘chakula cha miungu’.

Chokoleti ni bidhaa ya anasa yenye mahitaji makubwa duniani kwasababu ya faida nyingi zinazopatikana kwenye zao hilo ikiwemo kutibu magonjwa mbalimbali. Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Kakao (1CCO) mauzo ya bidhaa hiyo duniani ni Dola za Marekani bilioni 100 kila mwaka.

Asilimia 90 ya chokoleti yote inayotengenezwa duniani hutumiwa na nchi zilizoendelea zikiwemo za Ulaya, Asia na Amerika ya Kusini, huku asilimia 70 ya chokoleti hiyo hutokana na kakao inayozalishwa  barani Afrika.

Nchi za Ivory Coast, Ghana, Nigeria na Cameroon ndio wazalishaji wakubwa wa kakao barani Afrika licha ya kuwepo maeneo mengine ya Magharibi na Afrika ya Kati ambayo hayajatumia fursa ya kulima zao hilo.

Nchini Tanzania, zao hilo hulimwa katika Wilaya ya Kyela na Rungwe mkoa wa Mbeya ambapo huzalisha zaidi ya asilimia 95 ya kakao yote nchini. Maeneo mengine ni Ifakara-Morogoro na Maramba-Tanga na uwezekano wa zao hilo kulimwa maeneo mengine ya mkoa wa Kigoma ni mkubwa.

Kila mwaka inakadiriwa kuwa Tanzania huzalisha tani 7,000 ambazo ni sehemu ndogo ya uzalishaji wote unaofanyika katika nchi za Afrika Magharibi ambazo unazidi tani milioni 2.5 kila mwaka.

Kutokana na ongezeko la mahitaji chokoleti duniani, wajasiriamali wa Tanzania wanaweza kutumia fursa ya kuzalisha kakao kwa wingi ili kutengeneza kipato cha familia. Fursa hiyo ni kuhimiza matumizi ya chokoleti nchini ikizingatiwa kuwa Afrika inazalisha kwa wingi kakao lakini sio mtumiaji wa bidhaa hiyo ambayo mahitaji yake yameongezeka maradufu duniani.

Mathalani, nchi ya  Ivory Coast ambayo ni mzalishaji mkubwa wa kakao, wakulima wengi hawajawahi kuonja ladha ya chokoleti. Hii ni kwa mujibu wa runinga ya CNN ambayo ilifanya utafiti kubaini matumizi ya bidhaa hiyo miongoni mwa wakulima.

                                                                Chokoleti tayari kwa matumizi ya binadamu

 

Kwa kiasi gani unafahamu kuhusu kakao?

Mti wa kakao ni mdogo kwa kiasi cha futi 13 hadi 26, matawi yake ni ya kijani ambapo hulimwa maeneo yenye hali ya hewa ya kitropiki.

Nchi za Afrika ya Magharibi na Kati hasa Ivory Coast, Ghana, Nigeria na Cameroon zina zaidi ya wakulima milioni 2 ambao wanawajibika kuzalisha asilimia 70 ya kakao yote ya dunia.

Mti wa kakao hukomaa na kuanza kuzaa mbegu ambazo huwa ndani ya kokwa (pods) ikifikia miaka 4 au 5 tangu kupandwa. Kwa wastani mti mmoja wa kakao unazalisha matunda 20 hadi 30 wakati wa uvunaji. Kila kokwa hubeba mbegu 20 hadi 50 ambazo hujulikana kama mbegu za kakao.

Baada ya kokwa  kukomaa huvunwa na kupasuliwa ili kupata mbegu  ambazo huwekwa kwenye chombo maalum kwa siku 3 hadi 5 ili zichachuke. Mbegu hizo hukaushwa, huoshwa, hubanikwa na kupitia mchakato wa kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo chokoleti, vinywaji dawa za binadamu na vipodozi.

                                                                 Mkulima akivuna kakao baada ya kukomaa

 

Kwa nini ni muhimu kwa Wajasiriamali wa Tanzania kugeukia kilimo cha kakao ?

Kuna sababu mbalimbali kwanini biashara ya kakao ni fursa muhimu kwa wajasiriamali wa Tanzania:

Mti kakao asili yake sio Tanzania, uliingizwa barani Afrika zaidi ya miaka 100 iliyopita ukitokea Amerika ya Kusini, lakini sasa Afrika ndio mzalishaji mkubwa duniani.  Tanzania inaweza kufaidika na zao hilo kwasababu ni nchi pekee ya Afrika Mashariki ambayo hali ya hewa inaruhusu kulima zao hilo katika baadhi ya maeneo nchini.

Wakulima wakitumia vizuri fursa hii uwezekano wa kupata soko la uhakika la kakao ni mkubwa ikizingatiwa kuwa mahitaji yake yanaongezeka kila mwaka hasa katika nchi zilizoendelea ikiwemo Ulaya na Marekani.

Soko la ndani bado halijaguswa wala kufikiwa. Ikiwa wajasiriamali  watalima kwa wingi kakao na kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo chokoleti na kuweza kuishawishi jamii juu ya faida  za bidhaa hiyo; mafanikio ya kiuchumi yatakuwa makubwa kwa taifa.

Wawekezaji wa zao hilo tayari wameingia katika maeneo mbalimbali ya Afrika ili kuwekeza katika ujenzi wa viwanda na mashamba makubwa ya kakao. Taasisi ya TechnoServe  inayoendesha program ya Kokoa Kamili, imeanza kuwajengea uwezo wakulima wa kakao mkoani Morogoro kuchangamkia fursa hiyo adhimu Afrika Mashariki.

Simran Bindra na Brian LoBue waanzilishi wa program hiyo wanasema ikiwa Tanzania itajidhatiti na kuwekeza kwenye kakao uwezekano wa kubalisha maisha ya wakulima kiuchumi ni mkubwa.

“Ni sehemu mikakati ya biashara yetu”, amesema Simran. “Mafunzo ya kulima yameongeza ubora ikizingatiwa kuwa kakao ni zao linalokomaa kwa miaka minne. Pia tumeimarisha mahusiano na wakulima kuonyesha kwamba tunajali maisha yao”.

Kokoa Kamili ambayo inayoendesha shughuli zake katika bonde la Kilombero, Kusini Mashariki mwa Tanzania inanunua kakao mbichi na ghafi kutoka kwa wakulima 2,500 ambapo huichachusha na kuikausha kabla ya kuiuza kwa watengenezaji wa chokoleti waliopo Amerika ya Kusini, Ulaya na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mwaka 2015, taasisi hiyo ilinunua tani 82 za kakao na kuongeza uzalishaji kwa asilimia 70.

Fursa ya uzalishaji na usindikaji wa kakao ikitumiwa vizuri na wajasiriamali itaiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia. Lakini pia itachochea utekelezaji wa sera ya viwanda inayokusudia kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *