Kamati ya Ulinzi na Usalama Mwanza yawahoji vigogo wa Misungwi tuhuma za ufisadi

Jamii Africa

SIKU chache baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Mkoani Mwanza, kuanza kuwahoji baadhi ya vigogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mkoani hapa, kwa tuhuma za ufisadi wa mamilioni ya fedha za miradi ya maendeleo wilayani humo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo nayo imeanza kuwahoji baadhi ya vigogo wa halmashauri ya wilaya hiyo; FikraPevu imeelezwa.

Imeelezwa kwamba, kazi hiyo ya kuwahoji vigogo wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Misungwi, imeanza Jumatatu wiki hii, ambapo inadaiwa kamati hiyo ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa iliyopo chini ya uenyekiti wake Mkuu wa mkoa huo wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilo, iliwahoji vigogo watano juu ya tuhuma nzito za ubadhilifu wa fedha zinazoikabili halmashauri hiyo, inayoongozwa na Mkurugenzi wake, Xavier Tilweselekwa na mwenyekiti wake, Bernard Polcarp.

Vyanzo vya habari vimeiambia FikraPevu leo kwamba, vigogo hao ambao majina yao tunayahifadhi, waliwekwa kiti moto na wajumbe wa kamati hiyo inayojumuisha vigogo wa jeshi la polisi, wanajeshi, usalama wa taifa pamoja na watumishi mbali mbali wa Serikali.

“Jumatatu Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa iliwaweka kitimoto vigogo watano wa halmashauri ya Misungwi kuhusu tuhuma za ufisadi wa fedha za maendeleo.

“Hawa watu walikuwa wakihojiwa mmoja mmoja na kamati hiyo. Na mimi nilifika hapo nikakuta wameanza kuhojiwa, na mmoja wao alikuwa ndani akihojiwa na kamati hiyo ya ulinzi na usalama ya mkoa juu ya tuhuma hizo nzito za ufisadi wa fedha za miradi ya maendeleo”, kilisema chanzo chetu cha habari na kuongeza:

“Wakati nikiwa mkoani hapo, nilikuwa nikiwaona vigogo hao hawana raha kabisa, na kila aliyekuwa akitoka kuhojiwa ndani ya ofisi alionekana hana raha. Na hii inaonekana pengine walikuwa wakibanwa maswali magumu sana!. Lakini acha wabanwe maana wanatuhumiwa kwa ufisadi”.

Wiki iliyopita, baadhi ya vigogo wa halmashauri hiyo, walianza kuhojiwa na Takukuru kuhusiana na tuhuma za ubadhilifu huo wa fedha zinazoikabili halmashauri ya wilaya hiyo ya Misungwi, na kwamba hiyo ni moja ya hatua za kisheria zilizoanza kuchukuliwa na vyombo vya dola, ambapo inadaiwa huenda vigogo hao wakafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Inadaiwa kwamba, kuanza kuhojiwa kwa vigogo hao wa halmashauri ya wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, inatokana na ripoti mbali mbali za wakaguzi, ikiwemo ya TAMISEMI na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambazo zinadai kuwepo kwa ubadhilifu mkubwa wa mali za umma katika halmashauri ya wilaya hiyo ya Misungwi, na wahusika wametajwa moja kwa moja kwa majina yao.

Hivi karibuni, baadhi ya vyombo vya habari liliwemo gazeti hili viliripoti kuwepo kwa tuhuma hizo nzito za ubadhirifu wa fedha za miradi mbali mbali ya maendeleo wilayani humo, ambapo baadaye uongozi wa halmashauri hiyo uliwaita baadhi ya waandishi wa habari (si wa FikraPevu), kwa ajili ya kwenda kutembelea miradi na ‘kukanusha’ habari za awali.

Hata hivyo, tuhuma hizo za ufisadi katika halmashauri hiyo, ziliibuliwa upya Januari 25 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilo, baada ya kiongozi huyo kufanya ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo, ambapo pamoja na mambo mengine alikutana na watumishi wa halmashauri hiyo kisha kuzungumzia tuhuma hizo nzito.

Katika kikao hicho, RC Ndikilo ambaye alikuwa akitumia ripoti mbali mbali za wakaguzi kwa kutaja baadhi ya majina ya watumishi waliotajwa kwenye ripoti hizo kwa ufisadi, alitumia muda wa dakika 57 kukemea hali hiyo, na alisema atamshauri Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aivunje halmashauri hiyo, ili ianze upya.

Alipitafutwa jana ili azungumzie taarifa hizo za kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mwanza kudaiwa kuwahoji vigogo hao wa halmashauri ya wilaya ya Misungwi, mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa mkoa huo wa Mwanza, Evarist Ndikilo hakupatikana mara moja baada ya kuelezwa kwamba yupo na vikao vya Kiserikali.

Habari hii imeandaliwa na Sitta Tumma – FkraPevu Mwanza

1 Comment
  • Nikubaliane kimsingi kuwa hatua inayodaiwa kushughulikiwa na Mkuu wa mkoa wa Mwnza ambaye ni m/kiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa inastahili kupongezwa na kuigwa na taasisi zingine, Mimi nitoe wito kwa ngazi za kata na vijiji waliko wananchi wengi. Wazihuishe na kuzitumia kamati za ulinzi na usalama za kata/shehia na vijiji kudhibiti aina mbalimbali za uhalifu kama alivyo onyesha mkuu huyo wa Mkoa.

    Tuna majambazi kwenye mitaa yetu, Mafisadi yanatesa ktk mitaa , wauza unga ( madawa ya kulevya) nikitaja mifano michache. KUU Ya Kata/Shehia,Mtaa na Kijiji ni fursa muhimu sana ktk kudhibiti kama Mkuu huyo alivyofanya, Ninatamani hamasa ya mkuu huyo ishuke ngazi za Chini ili kuboresha ulinzi na usalama. Hapa napenda nimshauri, awaite wajumbe wa KAMATI ZA ULINZI NA USALAMA ZA KATA walau kwa awamu hata wakae chini ya mti awafunde akishiriana na Jeshi la Polisi na wadau wengine kudhibiti, kuzuia na kukabiliana na kila aina ya uhalifu katika HIMAYA ZAO ili kuwaponya waliowengi kule chini, wazungu wanasema To serve the people at the glassroot level /Community level…. ni mimi mpenda amani ya kweli

    UPANGA KATAYA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *