Katavi: Vyumba vitano kujengwa, madawati 300 yatengenezwa kuwanusuru wanafunzi 750 wa Shule ya Mkuyuni wanakaa chini

Jamii Africa

HALMASHAURI ya Kavuu katika Wilaya ya Mlele mkoani Katavi imeanza kuchukua hatua ya kutengeneza madawati 300 na kujenga vyumba vitano vya madarasa katika Shule ya Msingi Mkuyuni, Kata ya Majimoto.

Hatua hiyo imechukuliwa mara baada ya FikraPevu kuchapisha makala iliyoelezea kwamba, takriban wanafunzi 750 kati ya 2,500 wa shule hiyo wanaketi sakafuni kwa kukosa madawati.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kavuu, ambaye pia ni Diwani wa Kata hiyo, Nyansongo Serengeti, ameieleza FikraPevu kuwa, katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa madawati na vyumba vya madarasa, halmashauri  yake imeanza ujenzi wa vyumba hivyo vitano vya madarasa na kutengeneza madawati.

Serengeti alisema wamejipanga kuhakikisha ifikapo Aprili 2017 wawe wamekamilisha ujenzi wa madarasa hayo na kwamba wanataka yazinduliwe na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ambao unatarajiwa kuzinduliwa mkoani Katavi Aprili 2.

“Tumeona tutoe kipaumbele kwa shule hii wakati wa uzinduzi wa mbio za Mwenge ili kufanikisha uzinduzi wa madarasa hayo matano na utengenenzaji wa madawati 300,” alisema diwani huyo.

Februari 8, 2017, FikraPevu ilichapisha makala kwamba, licha ya baadhi ya shule kuwa na madawati mengi kufuatia agizo la Rais John Magufuli, lakini shule ya msingi Mkuyuni wilayani Mlele ilikuwa na uhaba mkubwa wa madwati kiasi kwamba wanafunzi 750 walikuwa wakiketi sakafuni.

Agizo la Rais Magufuli la kuondoa tatizo la uhaba wa madawati nchini limetekelezwa kwa kiasi kikubwa ambapo shule nyingi, hasa za msingi, zimekuwa na “mafuriko” ya madawati, kiasi cha kukosekana mahali pa kuyahifadhi, kwani yanazidi mahitaji ya shule. 

Mwongozo wa Wizara ya Elimu unahimiza dawati moja kukaliwa na wanafunzi watatu hadi wanne.

Licha ya changamoto ya ukosefu wa madawati na vyumba vya madarasa, shule hiyo yenye wanafunzi 2,500 pia ina uhaba mkubwa wa walimu ambapo inao watatu tu wa kuajiriwa, hali inayoleta uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 833.

Mwalimu  Mkuu  wa  shule  hiyo,  Mbamba Makoye aliieleza FikraPevu kuwa shule yake inao walimu wanne wengine wa kujitolea, ambao kwa kiasi wameweza kupunguza mzigo huo.

“Tunashukuru pia kwamba pamoja na kuwa na idadi ndogo ya walimu wanaofundisha masomo yote na madarasa yote, pia tunao vijana wanne wa kujitolea, hawa wanatusadia sana,” alieleza.

Mwalimu huyo alisema ongezeko la wanafunzi walioandikishwa darasa la kwana mwaka huu, linesababisha kukosekana kwa madawati.

Serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais Magufuli ilitangaza kuwepo kwa elimu bure kuanzia darasa la awamu hadi elimu ya sekondari, uamuzi ambao umeongeza wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.

Pamoja na mwalimu Makoye kueleza hali hiyo kuwa ameizoea, walimu watatu anaowaongoza wameilalamikia, huku wakisisitiza kuwepo kwa mazingira bora ili wapate mwanya wa kufundisha vyema.

Mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, Dickson Fabian aliiambia FikraPevu kwamba mazingira yao ya kufundisha ni magumu na kamwe hayawezi kuwapa wanafunzi elimu bora.

“Ninalazimika kufundisha madarasa matano na masomo yote, wakati siyo utaratibu wa taaluma yetu katika kuwapa wanafunzi elimu nzuri,” aliongeza mwalimu huyo.

FikraPevu ilibaini kuwepo kwa wanafunzi takriban 250 kwa darasa moja na ambao hufundishwa kwa wakati mmoja, wengine wakiwa wamekaa chini.

Mbali ya changamoto hiyo, lakini pia ilibainika kuwa, shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo, hivyo kufanya mazingira ya kusoma na kusomesha kuwa magumu.

“Inasikitisha kuwa walimu wa shule hii wanatumia vyoo kwa pamoja, walimu hawana choo, hii siyo nzuri kwa utoaji wa elimu bora,” analalamika mwalimu Fabian.

Mmoja wa wazazi wa wanafunzi, Michael Kalubwa, alisema ni jambo la kushangaza kwamba shule hiyo na nyingine za mkoa wake, bado zinakabiliwa na upunguu wa madawati wakati zipo ambazo zina madawati ya ziada.

Lakini agizo la Rais Magufuli lilizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatengeneza madawati ya kutosha ili kuondoa tatizo hilo.

TAGGED:
Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *