KITAMBI: Chanzo chake na jinsi ya kukiondoa

Dr. Joachim Mabula

Kitambi (kilibatumbo) ni tumbo kubwa ambalo linachomoza kwa mbele na wakati mwingi kuning'inia isivyo kawaida. Ni ugonjwa kama magonjwa mengineyo na huweza kuwakumba watoto, vijana, watu wazima na hata wazee wa jinsia zote!

Kwa baadhi ya watu, hukichukulia kitambi kama ishara ya ufanisi au mafanikio kwa mhusika katika nyanda nyingi za kijamii. Ni imani ambayo kwa namna moja ama nyingine inachekesha kwakuwa kilibetumbo ni ugonjwa kama magonjwa mengine.

Mwili wa binadamu una seli bilioni 50-200 za mafuta zilizogawanyika kwenye mwili wa binadamu. Kwa wanawake zipo sana maeneo ya matiti, nyonga, kiunoni na kwenye makalio. Kwa wanaume seli zipo sana kwenye kifua, tumboni na kwenye makalio.

Mafuta ya tumbo yanayofanya kitambi hukusanywa kwa njia kuu mbili, ya kwanza ni mafuta kutoka kwenye tishu zilizo chini ya ngozi na ya pili ni kutoka kwenye ogani za ndani kama moyo, kongosho n.k

SABABU ZA KUPATA KITAMBI:

Sababu kubwa ya kitambi ni kukosekana ulingano wa nguvu(kalori), mtu kula vyakula vinavyotia nguvu sana kuliko jinsi anavyoweza kutumia na kutoa kama taka mwili.

Vyakula vinavyochangia uongezekaji wa kilibetumbo ni pamoja na nyama (iwe ni ya kuchemsha, kukaanga au kuchoma), mafuta ya kupikia, (hasa yale yatokanayo na bidhaa za wanyama, kama siagi, na jibini), viazi ya kukaanga (chips), pizza, vyakula vyenye wanga mwingi kama ugali wa mahindi, mihogo, wali, mikate myeupe na pia viazi vya mviringo. Ndizi pia huchangia!

Sababu nyingine ni kuwa na chembe za urithi za unene kutoka kwa wazazi, pia kuna sababu za kimazingira. Ila pia kuna sababu nyingine zisizojulikana.

JINSI YA KUJUA KAMA UNA KITAMBI:

Kitambi kinaweza kuonekana kwa kirahisi kwa macho. Ila kujua ni kwa kiwango gani kitambi chako kipo inabidi kufanya vipimo vya kiuno(waist) na nyonga (hips). Mzingo wa kiuno ukiwa >102 cm au 40 in kwa wanaume na >88 cm au 35 in kwa wanawake, na uwiano wa kiuno na hips(Waist-Hip Ratio) ikiwa >0.9 kwa wanaume na >0.85 kwa wanawake.

BMI ya 30 au zaidi inaashiria 'Obese' uzito kuzidi kiasi. Kuwa na mzingo uliozidi kawaida ni kiashiria hatari cha matatizo ya kimetaboliki, kuliko hata cha BMI.

Kipimo kingine cha kitambi ambacho kimeonyesha uwezo zaidi kuliko BMI katika kutabiri uwezekano mkubwa wa magonjwa ya moyo ni Index Of Central Obesity(Waist-To-Height Ratio-WHtR) ambapo uwiano ukiwa sawa na 0.5 au zaidi, hii ikimaanisha mzingo wa kiuno angalau ni nusu ya kimo cha mtu.

Kipimo kingine ni Body Volume Index, kinachopima kitambi kwa kupima umbo la mtu na mgawanyo wa uzito wake.

NJIA ZA KUONDOA KITAMBI:

  • Mlo mzuri kiafya ndio ufunguo wa kupunguza uzito na kutoa kitambi. Kuacha kula vyakula vinavyotia nguvu sana, vyenye mafuta na sukari nyingi ndio msingi wa kuondoa kitambi. Hii husaidia mwili kutumia mafuta yaliyo mwilini kutengeneza nguvu hivyo kupunguza mafuta na kuondoa kitambi. Aidha, punguza matumizi ya vinywaji vyenye sukari kwa wingi na tumia samaki badala ya nyama.
  • Kufanya mazoezi ya mwili kila siku kwa dakika 30-60 walau siku 3 ndani ya juma (week) moja (Mfano kuendesha baiskeli na kukimbia).
  • Dawa ni muhimu tu kama una matatizo mengine kama kisukari, mfano dawa fulani za kisukari zinaweza kukusaidia kupunguza mafuta yanayozunguka ogani muhimu kama ini na kongosho.
  • Kufanya upasuaji mkubwa ili kupunguza mafuta, hii hufanyika kwenye nchi zenye teknolojia kubwa na hii hushauriwa endapo mafuta yaliyomwilini yamesababishwa na magonjwa yameshindwa kupungua kwa njia ya rahisi ya kawaida.

Imedhihirika pia kudhibiti 'Stress' inaweza kusaidia kwenye kupambana na kitambi.

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *