TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo imejiweka katika mazingira magumu ya kufuzu kwa fainali za Mashindano ya Afrika kwa wachezaji wa klabu za ndani (CHAN) baada ya kulazimishwa kwenda sare ya bao 1-1 na Rwanda katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza ilishuhudia wageni wakipata bao la kuongoza katika dakika ya 18 kupitia kwa winga wa kushoto Dominique Savio Nshuti.
Hata hivyo, nahodha wa Stars, Himid Mao Mkami, aliweza kuisawazishia timu yake katika dakika ya 34.
Matokeo hayo yanaifanya Stars iwe na kazi ngumu ya kutafuta ushindi katika mechi ya marudiano itakayofanyika kwenye Uwanja wa Stade Regionale Nyamirambo, jijini Kigali Jumamosi ijayo, Julai 22, 2017.
Mshindi baina ya Rwanda na Tanzania atakumbana na mshindi kati ya Uganda na Sudan Kusini katika raundi ya pili ya mashindano hayo, ambayo yamepangwa kufanyika Kenya kuanzia Januari 11 hadi Februari 2, 2018.
Hii ni mara ya saba kwa Tanzania kukutana na Rwanda ambapo imeshinda mechi moja tu, kutoka sare mbili na kufungwa mechi nne.
Sudan Kusini ililazimishwa kwenda suluhu na Uganda jana Ijumaa kwenye Uwanja wa Taifa wa Juba na mechi ya pili itafanyika Julai 22, 2017 kwenye Uwanja wa Star Times, Lugogo, jijini Kampala.
Katika mechi nyingine, Afrika Kusini imeilaza Botswana mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika mjini Francistown.
Akicheza kwa mara ya kwanza mechi ya kimataifa, kinda wa Kaizer Chiefs mwenye miaka 20, Ryan Moon, aliipatia Bafana Bafana bao la kuongoza dakika ya 28 kabla ya Gift Motupa kufunga la pili dakika ya 72 akiunganisha pasi ya Cole Alexander.
Ethiopia imetoa kipigo cha mbwa mwizi kwa Djibouti kwa kuifunga mabao 5-1 katika mchezo uliofanyika jijini Djibouti.
Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ethiopia, Getaneh Kebede anayechezea klabu ya Dedebit alicheka na nyavu mara nne na mwenzake Mulualem Mesfin akafunga bao la tano kwa Ethiopia.
Timu hizo zitarudiana katika mji wa Hawassa ulioko kusini mwa Ethiopia mnamo Julai 23, 2017.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndio mabingwa watetezi wakati Kenya wataingia moja kwa moja kwa kuwa ndio wenyeji.
Senegal nusura waadhiriwe ugenini leo hii baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 kwa Sierra Leone jijini Freetown.
Sierra Leone walifunga bao la kuongoza lakini wakashindwa kulilinda baada ya Senegal kusawazisha katika dakika za mwishoni mwa mchezo, hivyo kujiweka katika nafasi nzuri kwa mechi ya marudiano ambapo mshindi wa jumla atapambana na timu kati ya Guinea-Bissau na Guinea.
Guinea wana nafasi kubwa ya kusonga mbele baada ya kuicharaza Guinea-Bissau mabao 3-1 mapema leo Jumamosi.
Sierra Leone haijawahi kushiriki fainali za CHAN na inafanya kila jitihada kuhakikisha inafuzu safari hii.
Gambia na Mali zimetoka suluhu katika mchezo mwingine wa awali wa mashindano hayo ambao ulifanyika kwenye Uwanja wa Independence mjini Bakau leo Jumamosi.
Mshindi baina yao atakumbana na mshindi baina ya Mauritania na Liberia katika raundi ya pili.
Liberia itaikaribisha Mauritania kesho Jumapili.
Mali wameshashiriki mashindano hayo mara tatu na mwaka 2016 walipoteza kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenye fanali jijini Kigali, Rwanda.
Nayo Comoro imeichapa Lesotho mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Stade de Moroni hivyo kuiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele na kukumbana na mshindi kati ya Namibia na Zimbabwe.
Mabao ya Comoro yalifungwa na Mohamed Youssouf mabema katika kipindi cha pili na lile la ushindi lilipatikana dakika ya 78 kupitia kwa Raidou Boina Bacar.