Kombe la Shirikisho: Simba kutafuta tiketi ya ndege mjini Dodoma kesho. Ni fainali dhidi ya Mabo FC

Jamii Africa

WAKATI wakiendelea ‘kusubiria kudra za Mwenyezi Mungu’ zitende kazi kwenye rufaa yao waliyoipeleka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Simba kesho Jumamosi, Mei 27, 2017 watakuwa majaribuni mjini Dodoma kutafuta ‘akiba’ ya tiketi ya ndege  ili kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika watakapomenyana na Mbao FC ya Mwanza katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani mkali kwa timu zote mbili, ambazo kila moja ina majeruhi ya aina yake baada ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2016/2017.

Wachezaji wa Mbao FC na  Simba wakiwania mpira katika mojawapo ya mechi za Ligi Kuu 2016/2017.

FikraPevu inafahamu kwamba, Simba imekata rufaa FIFA kupinga hatua ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipoka ushindi wa pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar ambazo awali walikuwa ‘wamepewa mezani’ na inaamini kwamba, ikiwa rufaa yao itapita, basi wataipoka Yanga taji ambalo wamelichukua moja kwa moja baada ya kushinda kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Lakini matumaini hayo siyo kigezo cha Simba kubweteka kwenye mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, kwani tayari kocha msaidizi wa timu hiyo, Mganda Mayanja Jackson, ameshasema kwamba hataki kuona aibu ikiwapata kama ilivyotokea kwa mahasimu wao Yanga ambao walitolewa na Mbao FC kwenye nusu fainali ya mashindano hayo.

Simba ina usongo wa kushinda mechi hiyo na kunyakua kitita cha Shs. 50 milioni, lakini hamu yake kubwa  ni kushiriki mashindano ya kimataifa baada ya kuyakosa kwa miaka mitano mfululizo.

Wakati Simba ikiwaza hayo, Mbao nao ambao wamenusurika kushuka daraja baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 kutoka kwa Yanga, wana usongo mkubwa wa kutwaa taji hilo na kushiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya kimataifa na kuandika historia mpya ya timu za Mwanza tangu Pamba FC ilipofanya hivyo zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Kikosi cha Mbao FC.

Mbao iliponea chupuchupu kushuka daraja na ishukuru ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya Yanga ulioifanya ifikishe pointi 30 sawa na Ndanda FC iliyoteremka, ingawa vijana hao wa Mwanza walikuwa na uwiano ‘mzuri’ wa mabao ya kufunga.

Wakati Ndanda ilifunga mabao 21 na kufungwa 38, Mbao wenyewe walifunga mabao 29 na kufungwa 38 pia, hivyo wakaponea tundu la sindano kurudi Daraja la Kwanza na kuwaacha Ndanda, Toto African na JKT Ruvu Stars wakishuka.

Mchuano mkali tangu mwanzo

Tangu mwanzo wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam, ilionekana kulikuwa na mchuano mkali na Mbao FC walionyesha kudhamiria kufanya vizuri zaidi.

FikraPevu inatambua kwamba, Mbao walifuzu hatua hiyo ya fainali kwa kuichapa Yanga bao 1-0 kwenye nusu fainali iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wakati Simba wao walipata ushindi kama huo dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.

Simba na Mbao FC

Kabla ya hapo, Mbao walikuwa wameitoa Toto African pia ya Mwanza kwa mikwaju ya penalty katika Raundi ya 6 baada ya kutoka suluhu muda wa dakika 90, wakati Simba yenyewe iliifunga African Lyon 2-1.

Katika Robo Fainali, Mbao wakaitandika Kagera Sugar mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, na Simba ikapata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Madini FC ya Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Matokeo ya Ligi Kuu

Pengine Simba itajivunia matokeo mazuri dhidi ya Mbao FC kwenye Ligi Kuu msimu huu baada ya kushinda mechi zote mbili – kwanza ikiifunga bao 1-0 Oktoba 20, 2016 na baadaye mabao 3-2 Aprili 10, 2017.

Kikosi cha Simba.

Hata hivyo, FikraPevu inatambua kwamba Mbao FC, ambayo huu ndio msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu, imeonyesha kiwango kizuri licha ya matokeo ya mwishoni kuitia mashakani na kukaribia kushuka daraja.

Miongoni mwa matokeo ya ajabu ambayo Mbao ilionyesha kwenye msimu wa Ligi Kuu ni kuitandika Azam FC 2-1 Novemba 6, 2016, ikaifunga Ruvu Shooting 2-0 kabla ya kuichabanga Mtibwa Sugar mabao 5-0.

Haya yalikuwa matokeo ya kushangaza kwa mashabiki wengi wa soka ambao wanaamini hata katika mechi ya fainali dhidi ya Simba, timu hiyo inaweza kufanya maajabu makubwa na hata kunyakua taji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *