Kuporomoka majengo Dar: Tumekwama, tumeshindwa!

Ramadhani Msoma

Sherehe za pasaka ziliingia dosari hususan kwa wakazi wa Dar es Salaam kufuatia kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 mtaa wa Indira Gandhi katikati ya mji. Watu wengi wamejeruriwa na vifo vimefikia watu 36.

Hii si mara ya kwanza kwa jengo kuporomoka jijini Dar es Salaam. Miaka ya hivi karibuni ilitokea huko Chang’ombe manispaa ya Temeke kwa jengo la ghorofa  nne kuporomoka na kuua watu wanne, baadae jengo la ghorofa 10 katikati ya mji liliporomoka na kuua watu watatu na hivi karibuni huko Sinza na kadiri ya mwenendo inaonyesha halitakuwa jengo la  mwisho kuanguka.!

ghorofa laporomoka dar

Ghorofa lililoanguka, mitaa ya Indira Gandhi – Dar

Nakumbuka jengo lilivyoporomoka Chang’ombe-Temeke, Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa aliamuru watu wawajibishwe na ikaundwa timu ya ukaguzi wa majengo hapa Dar es Salaam sijui iliishia wapi! Tunarudi kwenye shida ile ile. Kiufupi majengo mengi yanayoota kama uyoga hapa Dar yananitia shaka. Hivyo, suala la ukaguzi wa majengo ni muhimu; iwe kwa majengo mapya na hata yale ya zamani.

ghorofa-laanguka-sinza

Ghorofa lililoporomoka mitaa ya Sinza – Dar

Tatizo kubwa linajidhihirisha kwa kushindwa kwetu kujenga taasisi bora na imara za usimamizi sio tu katika sekta ya ujenzi lakini kwenye usimamizi wa mambo mengi tu. Kuna taasisi za kiusimamizi na watu wanaolipwa kwa mfano wa kufanya ukaguzi wa majengo ‘’wataalamu’’ lakini haieleweki wanafanya nini na likitokea la kutokea wanaanza kurushiana mpira. Ili mradi wa ujenzi wa jengo kama hilo ufanyike kuna hatua nyingi za kufuata za kiukaguzi lakini wapi! Hayafanyiki na yanayotokea ndo hayo.

Kitu kingine kinachoshangaza, haya majengo yanajengwa kweupe kila mtu anaona mjini na sio vichochoroni ukaguzi unashindwaje kufanyika, hawayaoni? Rushwa nadhani ndo inayofanya hao wakaguzi wakaweka utaalamu wao pembeni (kama wanao) na kuacha mambo yakienda ndivyo sivyo kama sio rushwa ni nini hasa? Hii pia inafungua maswali mengine na hitaji la kusimamia kimadhubuti tabia ya vitendo vya rushwa katika usimamizi ambapo vibali hutolewa pasipo stahili alimradi mhitaji wa kibali anamudu kuhonga, kununua haki ambayo hastahili kuipata! Hakika ule usemi wa; “tamaa mbele mauti nyuma” kwani tamaa fedha ya wachache inasababisha mauti ya wengi.

Nilimsikia mhusika mmoja akisema vibali vya kujenga jengo vilionyesha ni ghorofa kumi tu lakini wajenzi walikuwa wameongeza nyingine sita ambazo hata kipofu angeziona mweh!

Kuna umuhimu wa kujenga taasisi za usimamizi hapa nchi zenye weledi, uwezo, na utashi wa kufanya kazi zao kiuadilifu ili tuweze kusonga mbele. Pia kuna umuhimu wa taasisi hizo kulazimishwa kufanya hivyo na uongozi wa juu (ambao nao unatupa mashaka, ila hatuna jinsi si tuliwachagua!) la sivyo huduma kutoka kwenye taasisi za usimamizi zitaendelea kutuletea vilio ambavyo hatuvistahili kabisaa!

Shida nyingine ninayoiona ya taasisi hizi za umma ni kutokujifunza kwa yale ambayo yamekwisha likumba Taifa letu. Mifano niliyoitoa hapo juu inaadhihirisha yameporomoka majengo matatu kabla ya hili la juzi lakini kulikuwa hamna kujifunza. Wahenga wanasema; “kosa si kosa, bali kosa ni kurudia kosa”!

Kwenye ajali za meli  ilianza ajali mbaya kabisa ya MV Bukoba mnamo mwaka 1996 zikafata ajali zingine za kutisha zote kubwa na zenye kupoteza uhai wa wananchi wetu. Tumekataa kujifunza.

makaburi-mv-bukoba

Yaliyaanza mabomu Mbagala hatukukujifunza ikaja Gongo la Mboto sijui mpaka tukumbwe na nini ndo tutaamka! Hii ndiyo jamii yetu!

Juzi juzi tu tumeona vikosi vyetu vya zimamoto vilivyohangaika kuuzima moto ulioanza kwenye ghorofa moja ya juu ya jengo la PPF tower pale mjini, Zimamoto wenyewe walikiri jinsi ukosefu wa vifaa ulivyowakwamisha katika zoezi hilo ingawa walifanikiwa kuzima moto. Lakini utashangaa hali ya kikosi hicho cha zimamoto itabaki hivyo hivyo bila kuboreshwa wakati huduma yao ni muhimu kwa usalama wa watu na mali zao.

ghorofa-likiungua-kariakoo

Ghorofa likiungua mitaa ya Kariakoo

Taasisi chache au wizara zizofanya vizuri ni kwa sababu ya watu tu ‘‘personality’’ wawili watatu wanaoziongoza lakini hamna uwezo wa kitaasisi kwa kweli. Na mara nyingi watu hao wakiondoka inakuwa ni bahati nasibu kwa taasisi hiyo au wizara kuendelea kufanya vizuri. Na kwa sababu kufanya vibaya ndo imekuwa kawaida katika medani za uongozi wetu wafanya vizuri wanapingwa, kuhujumiwa na mfumo wa kiutendaji na hata kuonekana watu wa ajabu.

Tumejiwekea sheria taratibu na kanuni sisi wenyewe lakini tunashindwa kuzifuata na hiyo ndo inasababisha kukwama. Ili kuwa na taasisi imara lazima watu watii sheria na taratibu zilizowekwa, mamlaka zetu za juu za uongozi kama wizara husika lazima lisimamie hili. Kama tunayataka maendeleo lazima pia tubadilike kwa kiasi kikubwa katika namna ambavyo  tunavyoyafanya mambo yetu la sivyo tutaendelea kushuhudia majanga yenye kuweza kuzuilika yakiikumba jamii yetu

Uwajibikaji na kuwajibishana serikalini pia kungesaidia kurekebisha madudu mengi yanayotokea na hii haijalishi hata kama Waziri wa wizara husika hahusiki moja kwa moja na mambo ya hovyo yanayotokea kwenye taasisi anazoziongoza. Hii ingewafanya wawe makini zaidi na kuwabana walio chini yao kufuata taratibu zinazoongoza taasisi zao. Jambo ambalo kwa sasa hilo halipo.

Ni muhimu sana kwa kila mtu afanye kazi yake ipasavyo na awajibike mambo yakienda mrama. Kwa upande mwingine kwetu wananchi, ni kama vile tuna mioyo ya chuma yenye kuhimili kushuhudia utendaji mbovu wa viongozi na watendaji mbalimbali katika taasisi husika bila kuchukua hatua stahiki. Tumechoka kuona baada ya mambo kwenda hovyo viongozi wetu kwenye vyombo vya habari na maelezo marefu ya kuunda tume na kuahidi huo uvurundaji hautatokea tena wakati wenyewe ni sehemu ya tatizo.

Mpaka hapo tutakapobadilika na tukayakataa madudu kwenye uongozi wetu, ndio tutajikwamua kutoka hapa tulipo. Hatuoni kama viongozi wetu wanajiona kama sehemu ya tatizo wanaamini kama bado wao ni sehemu ya sululisho kama inavyotakiwa iwe kitu ambacho sicho. Ni wakati sasa wa kuwaambia kwamba wao ni sehemu ya matatizo yetu makubwa.

Poleni wafiwa na Mungu awajalie wepesi katika kuyapokea haya!

3 Comments
  • kwa kweli kaka Rama tunakushukuru kwa kutoa changamoto, ni kweli kabisa katika Taifa letu watu wameendekeza sana manufaa yao kuliko kuangalia hasara itakayopatikana badaye.

    siyo kama hatuwezi kuyakabili majanga mbalimbali yanayojitokeza bali ni fikra potofu na kutowajibika kwa nafasi ya mtu aliyepewa dhamana kusimmamia eneo husika kwa misingi hiyo naungana na wewe kwa asilimia mia moja kwa kila mtu kusimamia na kuwajibika kwa eneo husika

  • nchi imekuwa nchi ya walarushwa na wanyanga’nyi. tatizo liko wazi badala serikali kuchukua hatua inaunda tume na kutumia fedha nyingi za walipa kodi, halafu hiyo tume inaenda kula rushwa kwa mtuhumiwa. sasa tunaenda wapi? mungu aingilie kati na kunusuru hii nchi

  • Naskia eti nondo zimenunuliwa chang’ombe zinaviwango duni. hii nchi cjui mwisho wake maana kila kitu kimechakachuliwa na viongozi waliopewa dhamana wapo wana take easy.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *