Kuwashusha walimu vyeo ni njia sahihi ya kutatua changamoto za elimu?

Jamii Africa

Mwishoni mwa mwaka 2017 wanafunzi wa darasa la nne na la saba walifanya mitihani ya kitaifa ili kupima ujuzi na maarifa waliyoyapata katika kipindi cha kusoma kwao ambapo waliofaulu waliendelea na madarasa ya mbele.

Matokeo ya mitihani hiyo yametangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA)na kuonyesha kupanda kwa ufaulu ukilinganisha na miaka iliyotangulia. Lakini baadhi ya shule hasa za serikali zimefanya vibaya.  

Matokeo mabovu katika baadhi ya shule yamesababishwa na sababu mbalimbali za kitaaluma ikiwemo uhaba wa walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Kutokana na matokeo hayo Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoa wa Manyara imejitathmini na kugundua kuwa walimu wakuu katika baadhi ya shule za msingi wamechangia kuferi kwa wanafunzi katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi. Tathmini hiyo imetoa mapendekezo ya kuwashusha vyeo walimu wakuu ambao shule zao zimefanya vibaya ili nafasi zao zichukuliwe na wengine wanaoweza kuwajibika.  

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Hamis Malinga amewashusha vyeo walimu wakuu 28 wa shule za msingi na waratibu 10 wa elimu wa kata ambao wanafunzi wa darasa la saba katika shule zao kutofikisha asilimia 50 ya ufaulu.

Halmashauri ya wilaya ya Babati ina shule za msingi 142 na ilishika nafasi ya tatu kati ya halmashauri saba za mkoa huo katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba wa mwaka jana. Sababu kubwa ni kushindwa kwa walimu wakuu na waratibu hao kuwasimamia walimu kutimiza majukumu yao ya kufundisha darasani

Amenukuliwa akisema, "Wanashindwa kusimamia elimu kwenye nafasi zao na hawachukui hatua yoyote ili kusaidia kwani mwalimu hafundishi, anachezacheza na mabinti shuleni, hawaandai maandalio ya masomo, tutaendeleaje kwa hivi?”.

Kauli ya Mkurugenzi huyo ni dhahiri kuwa ni kuwatwika walimu mzigo wa lawama ambazo hawakustaili kuzipata na kukwepa uwajibikaji ukizingatia kuwa walimu wamekuwa wakijitoa sana kufundisha wanafunzi licha ya mazingira magumu yanayowazunguka.

Ni vema uongozi wa halmashauri hiyo ungejiridhisha na kuangalia maeneo muhimu ya miundombinu, mazingira wanayosomea wanafunzi kwa kiasi gani yamekuwa kikwazo kwa wanafunzi kufaulu kuliko kuwaadhibu walimu wakuu ambao hawahusiki kuboresha miundombinu ya shule zaidi ya kusimamia sera na mitaala ya ufundishaji.

Changamoto ya muda mrefu ambayo imekuwa ikikwamisha ukuaji wa sekta ya elimu nchini ni mazingira yasiyoridhisha ya kufundishia na kujifunzia ambayo yamekuwa kikwazo kwa walimu kutimiza majukumu yao.

Zipo baadhi ya shule hazina mindombinu ya madarasa, nyumba za walimu, vifaa vya kufundishia. Ingekuwa vema Halmashauri ingeelekeza juhudi zake kutatua changamoto za msingi za shule husika ambazo wanafunzi wake wameferi.

Mathalani, shule zinazomilikiwa na watu binafsi zimekuwa zikifanya vizuri kwasababu zimefanikiwa kuweka mazingira mazuri ya ufundishaji ambayo yanavutia mwalimu kufundisha na kuhakikisha wanafunzi wake wanafikia kilele cha mafanikio ya elimu.

Wakati serikali inashughulikia miundombinu ya shule, isisahau maslahi ya walimu ambayo yamepuuzwa kwa muda mrefu ambapo baadhi ya walimu hutumia mwanya huo kutotimiza majukumu yao na kuathiri maendeleo ya wanafunzi darasani. Pia walimu wapewe motisha ya fedha, ujuzi, vitu ili  kuongeza hali ya kufundisha.

Utafiti wa Twaweza ulifanyika chini ya mradi wa ‘KiuFunza’ ambao unachochea kiu ya kujifunza katika shule za msingi kwa kutoa motisha ya fedha kwa walimu, unaeleza kuwa kuna uhusiano wa karibu katika ya motisha na ufanisi wa mwalimu katika ufundishaji.

“Pale ambapo bahshishi na ruzuku vilichanganywa, matokeo ya kujifunza katika madarasa ya I, II na III, yalikuwa ni mazuri: tulibaini kuwa viwango vya ufaulu wa Kiswahili na Hesabu viliongezeka kwa asilimia 20 katika kipindi cha mwaka mmoja”, anaeleza Mwalimu Mbando katika ripoti hiyo.

Kwa upande wake, Mshauri wa Elimu kutoka Ubalozi wa Canada nchini Tanzania, Beatrice Omari amesema  utoaji wa motisha jambo muhimu kutatua changamoto za elimu lakini ni muhimu serikali kutambua mchango wa mwalimu na kutafuta motisha zingine zitakazoongeza bidii ya walimu.  

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *