Kwanini kuna feni, viyoyozi vinavyotoa upepo mkali kwenye milango ya maduka makubwa ya biashara?

Jamii Africa

Majengo mengi makubwa hasa yale ambayo milango yake hubaki wazi huwekwa feni au viyoyozi vikubwa kwenye milango ya kuingilia. Utausikia upepo huu mkali mara tu utakapoingia kwenye jengo husika.

Unapotoka kwenye hali ya joto na ghafla ukakutana na upepo mkali wa aina hii mwilini huwa ni jambo la kufurahisha na kuvutia.

Pamoja na kupulizwa na upepo huo mwanana, Je, umeshawahi kujiuliza kwanini feni au viyoyozi hivyo vipo hapo? Je, vipo hapo kuwapuliza na kuwafurahisha tu watu au vina kazi nyingine kubwa zaidi ya hiyo?.

Ni kweli, inafurahisha na kupendeza, lakini kabla hatujazungumzia sababu hasa za hali hiyo, tuangalie kwanza jambo muhimu linalotengeneza hali hiyo.

 

Uhakika wa upatikanaji wa umeme kwenye majengo
Umeme wa uhakika katika majengo makubwa umekuwa ni suala la lazima katika siku za hivi karibuni kutokana na umuhimu wake kwenye usambazaji wa hewa safi inayowafanya watumiaji wa huduma katika majengo hayo kujisikia vizuri.

Kutokana na ukuaji mkubwa wa idadi ya watu duniani na viwanda, kumekuwa na changamoto kwenye rasilimali asilia-kwamba zinaweza kutengeneza nishati inayoweza kukidhi mahitaji ya kibinadamu katika majengo makubwa duniani.

Uendelezaji wa majengo yenye nishati ya uhakika ni muhimu ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa hasa ongezeko la joto (global warming) ambalo lisipotafutiwa ufumbuzi wa kudumu linaweza kuathiri mwenendo wa shughuli katika majengo makubwa.

              Mfumo wa hewa katika majengo makubwa

Kwenye majengo na maduka makubwa, viyoyozi vinatumia sehemu kubwa ya umeme unaosambazwa katika majengo hayo. Kwa muktadha huo, wajenzi kabla ya kujenga jengo husika hufanya tathmini ya hali ya hewa kuzunguka jengo. Tathmini hiyo huwasaidia kufahamu mgawanyo wa umeme na jinsi utakavyotumika ili kuhakikisha jengo linaunganishwa na mfumo mzuri wa usambazaji hewa.

Moja ya eneo ambalo linatumia umeme mwingi katika majengo makubwa ni sehemu ya kuingilia au mlangoni ambako hufungwa viyoyozi au feni zinazosimamia hewa inayoingia na kutoka ndani ya jengo.

 

Hewa ya Mlangoni ni nini?
Hewa ya Mlangoni (Air door) ni kifaa kinachozuia hewa au kemikali chafu kusafiri kutoka eneo moja kwenda lingine. Kwa mujibu wa Chama cha Marekani cha Upashaji, Upozaji na Wakandarasi wa Viyoyozi (ASHRAE), hewa ya mlangoni kwenye majengo makubwa ni mfululizo wa tabaka la hewa la kiwango fulani ambalo linazunguka kwenye mlango wa kuingilia. Tabaka hilo la hewa huwa pembeni ya mlango na huambatana na nguvu ya upepo ili kuhakikisha hewa yoyote inayotoka nje haiingii ndani ya jengo.


Pia hutambulika kama zulia la hewa, ambalo hufanya kazi kama kizuizi cha hewa ya nje iliyochanganyika na uchafu isiingie ndani ya duka au jengo na ndio maana ikaitwa hewa ya mlangoni (air door).

Hewa ya mlangoni hutoka kwenye feni ya upepo au kiyoyozi (Air-condition), na mara nyingi huwekwa kuelekea mlango wa kuingilia kwenye maduka makubwa, majengo ya ofisi na mashirika.

Jambo la kukumbuka ni kuwa hewa ya mlangoni haitumiki tu kwenye milango ya majengo lakini kwenye sehemu yoyote ya wazi ambayo inakutanisha hali ya joto tofauti. Ndiyo sababu unaweza kugundua kuwa duka binafsi lililopo kwenye jengo kubwa linakuwa na feni yake ya upepo ambayo imefungwa mlangoni, ili hewa ya jengo kubwa isiingiliane na ile ya dukani.

Faida za Hewa ya mlangoni
Faida ya awali na muhimu inayotolewa na zulia la hewa mlangoni ni kuwa inazuia hewa ya nje isiingie ndani ya jengo lenye viyoyozi na kuilazimisha ibaki nje ili isiharibu mfumo wa hewa uliopo kwenye jengo.

Kwa kutimiza jukumu lake, hewa ya mlangoni inatenganisha kwa kiasi kikubwa hali hewa ya ndani ya jengo na ile ya nje. Ufanisi wa hewa ya mlangoni, linapokuja suala la kuzuia hewa ya nje kuingia ndani, hufikia asilimia kati ya 60 na 80.

Sasa utakuwa umefahamu kuwa kuweka vizuizi vya hewa kwenye mlango wa kuingilia kunahusiana moja kwa moja na kupunguza tatizo la matumizi makubwa ya umeme. Hewa ya mlangoni hufanya kazi nzuri ya kupunguza bili za umeme kwenye majengo hayo.

Hata hivyo, hewa ya mlangoni ina faida nyingi zaidi ya kupunguza matumizi ya umeme. Pia zinazuia uchafu na vumbi kutoka nje kuingia ndani ya jengo. Hiyo ndiyo sababu kwanini majengo hayo hayachafuki kama majengo mengine yasiyo na mfumo wa kudhibiti hewa. Pia vizuizi hivyo vya hewa vinaweza kuitoa nje hewa chafu na harufu mbaya inayotengenezwa ndani ya jengo.

Zaidi ya hapo, hewa ya mlangoni huzuia wadudu kuingia ndani ya jengo na kuepusha usumbufu kwa watu waliopo ndani.

Itambulike kuwa watu wanaojisikia vizuri kwasababu ya feni au viyoyozi vilivyopo kwenye maduka makubwa wanastahili zaidi huduma bora, heshima na furaha kuliko ile wanayoipata katika majengo hayo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *