Ni matarajio au matamanio ya kila mtu kusaidiwa kukamilisha jambo fulani. Iwe kazini au kwenye shughuli yoyote ya kijamii, utahitaji watu wenye ujuzi na maarifa tofauti tofauti kufanikisha malengo yako. Mfano, wachezaji wakiwa uwanjani wanacheza kwa kusaidiana kila mmoja katika nafasi yake ili kuifunga timu pinzani na kuibuka na ushindi.
Hakuna jambo lolote linaloweza kukamilika bila ya kuwa na usaidizi wa namna fulani. Lakini umewahi kujiuliza kwanini ni vigumu kwa watu kuomba msaada?
Jibu linatolewa na Mwanasaikolojia ya Jamii, Heidi Grant anaeleza kuwa, kilichopo nyuma ya kuomba msaada ni hofu ya kukataliwa ambayo imekita mizizi katika saikolojia ya uumbaji wa mwanadamu.
Katika kitabu chake kiitwacho, Reinforcements anaandika kuwa kuomba msaada ni jambo lisilopendeza linalomfanya mtu ajisikie mgonjwa.
Hilo linathibitishwa na Mtaalamu wa Saikolojia mwingine nchini Marekani, Stanley Milgram ambaye alifanya jaribio la utii na mamlaka ambapo aliwaelekeza wanafunzi wake ambao walikuwa wamesimama ndani ya treni kuomba nafasi ya kukaa kwenye viti. Anasema majibu aliyopata ni kwamba wengi wao waliogopa kuomba msaada huo. “Niliogopa ningesingeweza,” alisema mmoja wa wanafunzi.
Lakini Milgram aliamua kuomba siti na akakubaliwa , “ Kichwa changu kilizama katikati ya miguu yangu na nilihisi nimepigwa na butwaa,” anaandika. “Sikufanya wajibu wangu. Nilikuwa najisikia kama naenda kupotea.”
Muitiko huo ambao Grant ameuelezea unahusiana na tabia za kijamii ambazo zimeunganishwa kwenye ubongo wa mwanadamu tangu karne nyingi za uumbaji. Kama wanyama wengine, binadamu wameumbwa kupata msaada kutoka kwa familia na jamii zao ili waweze kuishi. Lakini inafika wakati tunaogopa kuomba msaada hata kama tuna shida.
Kwanini watu wanaogopa kuomba msaada?
Zipo sababu mbalimbali ambazo zinasababisha watu kuogopa kuomba msaada ni kupoteza hadhi na heshima katika jamii. Wapo baadhi ya watu wana hadhi fulani ambayo anahisi akiomba msaada kwa watu atadharaulika. Pia kukataliwa, siyo kila ombi linakubaliwa, mengine yanakatiliwa; hofu hiyo huwazuia watu kuomba msaada. Wakati mwingine ukiomba msaada inakuwa ni njia ya watu kufahamu matatizo yako na kuwaambia wengine; jambo linaloweza kutengeneza huzuni katika maisha.
Grant anaeleza kuwa kuomba msaada kunakuweka wazi zaidi na hatari za kijamii ambazo zinaweza kudhihirisha unyonge na kukaribisha maumivu.
Anaeleza zaidi kuwa inatengeneza huzuni, na kukaribisha uwezekano wa kukataliwa. “Hajalishi, ndiyo maana tunaogopa kuomba msaada kama tunavyogoopa maradhi,” ameandika. “Maradhi yanaweza kuwa na hatari ndogo kwetu ukilinganisha na kuomba msaada.”
Hata hivyo, ni mara chache sana matokeo hasi tuliyoyaona hapo juu kutokea mara tunapoomba msaada. Katika utafiti mwingine, Mwanasaikolojia Vanessa Bohns alichunguza sampuli ya watu 14,000 ambao walitakiwa kuomba msaada. Na alibaini kuwa idadi kubwa ya walioomba msaada walikuwa na uwezekano mkubwa wa kupata kuliko ambavyo walikuwa wanaamini awali.
Katika semina mbalimbali, Mhamasishaji, Antony Luvanda amekuwa akisisitiza kuwa kuomba msaada siyo ishara ya unyonge bali ni ishara kuwa umeimarika kimaisha.
Kwa maneno mengine, inaweza kuwa rahisi kupata msaada kuliko kuomba.